Makubaliano ya kudhibiti biashara ya silaha yaanza kutekelezwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano ya kudhibiti biashara ya silaha yaanza kutekelezwa

Makubaliano ya kudhibiti biashara ya silaha duniani yanaanza kutekelezwa leo (24.12.2014), huku wanaharakati wakiapa kuwa watahakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa ipasavyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon

Makubaliano hayo ya kihistoria ya kudhibiti biashara ya silaha, ATT, yameweka sheria katika sekta ya viwanda vya kutengeneza silaha yenye thamani ya Euro bilioni 70 na yanataka kuziondoa silaha mikononi mwa wahalifu na watu wanaokiuka haki za binaadamu.

Wanaharakati wanaounga mkono makubaliano hayo wamefurahishwa na maendeleo hayo, wakisema wameyasubiri kwa muda mrefu. Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la muungano wa asasi za kudhibiti silaha, Anna Macdonald, amesema kwa muda mrefu silaha zimekuwa zikiuzwa, lakini maswali bado yanabaki kwa wale wanaoathirika na silaha hizo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zilizotia saini zinalazimika kuunda vitengo vya kitaifa vya kukagua bishara ya silaha zinazouzwa nje ya nchi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, nchi iliyosaini na kuridhia ATT

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, nchi iliyosaini na kuridhia ATT

Nchi hizo zinapaswa pia kufanya tathmini kuangalia kama silaha zinazouzwa nje zinaweza kukwepa vikwazo vya kimataifa, kutumiwa katika mauaji ya halaiki au katika uhalifu wa kivita, au kama zinaweza kuangukia mikononi mwa makundi ya ugaidi au ya kihalifu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema makubaliano hayo yanaonesha dhamira ya mataifa mbalimbali, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kuachana na biashara ya silaha. Ban amesema anaendelea kuyahimiza mataifa yote, hasa yanayouza silaha kwa wingi kusaini makubaliano hayo. Pia ameyataka mataifa yote yaliyoridhia makubaliano hayo kuanza kuyatekeleza mara moja bila ya kuchelewa.

Kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa azungumza

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, ameyapongeza makubaliano hayo kama mfumo wa kukomesha kutiririka kwa silaha ambazo zinaweza kutumika kufanya mauwaji, uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Wanaharakati wanasema kutekelezwa kwa makubaliano hayo kutasaidia kuifanya biashara ya silaha kuwa ngumu zaidi kuingizwa kwenye maeneo yenye mizozo duniani kama vile Syria, Sudan Kusini na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati pamoja na Afrika. Mkutano wa kwanza wa mataifa yaliyosaini makubaliano hayo utafanyika mwezi Septemba, mwaka ujao.

Rais Vladmir Putin wa Urusi, nchi ambayo bado haijasaini ATT

Rais Vladmir Putin wa Urusi, nchi ambayo bado haijasaini ATT

Tangu yalipoidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miaka miwili iliyopita, makubaliano hayo yamesainiwa na nchi 130, lakini yameridhiwa na nchi 60 tu, zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Italia, Uhispania na Uingereza pamoja na Israel ambayo imeridhia mwezi huu.

Marekani ambayo ndiyo mtengenezaji mkubwa na msafirishaji wa silaha duniani, imesaini makubaliano hayo lakini bado inasubiri ridhaa ya Baraza la Seneti. Mataifa mengine yanayotengeneza silaha kwa wingi kama vile China, Urusi, India na Pakistan bado hayajasaini makubaliano hayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com