1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yakumba maeneo ya Kusini mwa Afrika

27 Januari 2011

Tahadhari ya kutokea mafuriko imetolewa katika baadhi ya maeneo ya Msumbiji, wakati huduma za kusimamia majanga ikiwahamasisha wananchi kukabiliana na uwezekano wa kuzuka mafuriko mabaya kama yale maafa ya mwaka 2000.

https://p.dw.com/p/105Rt
Kimbunga Gustavo
Kimbunga GustavoPicha: AP

Baadhi ya watu wanaoishi karibu na bonde la Mto Limpompo nchini Msumbiji wameanza kuyahama makaazi yao na kuelekea katika maeneo yenye usalama zaidi, baada ya tahadhari kutolewa kwamba kiasi watu 7,000 huenda wakaathiriwa iwapo mto huo utajaa na kufikia mita mbili zaidi ya viwango vilivyotolewa tahadhari. Mkurugenzi wa Kituo cha Operesheni za Dharura nchini Msumbiji-CENOE, Dulce Chilundo ameliambia shirika la habari la IPS kuwa iwapo mvua zitaendelea kunyesha maji yatajaa na kusababisha mafuriko.

Chilundo anasema maji hayo yanaweza yakajaa pengine kufikia uwiano sawa na maafa ya mwaka 2000 ambapo karibu watu 700 waliauwa na kusababisha uharibifu wa mali za Dola milioni 419. Watu kadhaa wamekufa kutokana na vimbunga katika msimu huu wa mvua, lakini havihusishwi moja kwa moja na mafuriko. Joao Ribeiro, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Majanga ya Kitaifa ya Msumbiji-INGC, amesema ni mapema mno kueleza iwapo mafuriko yatawaathiri watu milioni 1.3 ambao wako katika hatari ya kukumbwa na mafuriko. Ribeiro amesema msimu wa mvua haujakwisha, utafikia kiwango chake cha juu mwezi ujao wa Februari.

Mchanganyiko wa mvua na mito kutoka nchi jirani inaweza kusababisha matatizo. Bwawa la umeme nchini Msumbiji la Cabora Bassa limejaa kwa asilimia 60, lakini Mto Zambezi ambao unaingia katika bwawa hilo hubeba maji kutoka nchi nyingine tano katika njia yake yenye urefu wa kilometa 2,700. Wakati bwawa la umeme la Kariba lililopo katika mpaka wa Zambia na Zimbabwe litaanza kumwaga maji kwa nguvu mwezi Februari, mtiririko wake unaweza kulazimisha bwana la Msumbiji kufanya hivyo.

Chilundo anasema kuwa INGC imezihamisha familia 24,000 zilizo karibu na bonde la Zambezi katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kuwapeleka kwenye maeneo yenye miinuko, lakini mashamba yao bado yako katika maeneo ya mabondeni, ambako yataendelea kuwa katika mazingira magumu. Imeelezwa kuwa Msumbiji imejiandaa vilivyo kukabiliana na mafuriko hayo.

Wakati huo huo, wiki iliyopita Afrika Kusini ilitangaza janga la kitaifa kutokana na mafuriko, nchi nyingine katika ukanda huo zinajizatiti wakati viwango vya maji vinazidi kupanda. Marufiko hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 123 na kuwaacha wengine kiasi 20,000 wakihitaji msaada wa mahitaji muhimu ya haraka. Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii ya Afrika Kusini, Abram Phahlamohlaka, amesema manispaa 33 katika majimbo manane ya nchi hiyo yalitangazwa kuwa maeneo ya maafa.

Afrika Kusini inatarajia mafuriko makubwa katika miaka mingi. Mto Orenge ambao unaenda umbali wa kilometa 2,300 kutoka Lesotho kwenda mashariki mwa Bahari ya Atlantic nchini Namibia. Maria Amakali, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimali ya Maji nchini Namibia amesema mafuriko ya safari hii yamewahi kuliko miaka iliyopita. Van Langenhove, Mkurugenzi wa masuala ya maji katika Wizara ya Kilimo nchini Namibia, anasema kuwa Mto Zambezi kwa kawaida hujaa ifikapo mwezi Machi au Aprili, lakini kuna dalili kwamba mafuriko yatatokea mapema zaidi, kulingana na mvua zitakazonyesha katika miezi ijayo.

Mmwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman