Maelfu ya wakaazi wa Dafur watumbukizwa utumwani | Masuala ya Jamii | DW | 17.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Maelfu ya wakaazi wa Dafur watumbukizwa utumwani

Wanajeshi wa serikali ya Sudan na wanamgambo wamewateka nyara kwa kutumia nguvu wanaume,wanawake na watoto kwa ajili ya kuwatumikisha na kuwafanya watumwa wa ngono katika jimbo lililokumbwa na vita la Dafur nchini Sudan.

Wakimbizi wa mzozo wa Dafur.

Wakimbizi wa mzozo wa Dafur.

Jeshi la Sudan limesema madai hayo yaliotolewa na muungano wa mashirika ya misaada ya Afrika hayastahiki kutolewa maelezo na msemaji wa serikali ya Sudan hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia taarifa hiyo.

Darfur Consortium Muugano wa mashirika ya misaada ya Afrika umesema umegunduwa ushahidi kwa mara ya kwanza kabisa kwamba wanaume wamekuwa wakitekwa nyara na kutumbukizwa utumwani kama watumishi wa kilimo wakati wa mashambulizi huko Dafur ya magharibi ambapo mzozo wa eneo hilo unaingia mwaka wake wa saba.

Kwa mujibu wa uchunguzi wao mashirika hayo wengi wanaotekwa nyara ni wanawake na wasichana ambao hubakwa na kufungishwa ndoa kwa nguvu na hata kutumiwa kama watumwa wa ngono na watumishi wa nyumbani na wanajeshi walioko Khartoum wakati wanaume hutumikishwa kwenye kazi za kilimo.

Repoti yao hiyo inasema utekaji nyara huo kwa ajili ya kutumikisha kazi na utumwa wa ngono unaotumiwa na wanamgambo wa Janjaweed,Jeshi la Ulinzi la Sudan pamoja na wanamgambo wenzao wengine unakwenda pamoja au sambamba na mateso,kuuwa raia,uharibifu wa vijiji na ukandamizaji mwengine wa haki za binaadamu kama sehemu ya sera ya makusudi ya kutokomeza kizazi cha makundi fulani kuwapotezea makaazi yao na kuinyakuwa ardhi ya makundi ya kikabila yasiozungumza lugha ya Kiarabu.

Eneo lao baadae hujazwa tena watu wenye kuzungumza Kiarabu yakiwemo makabila ya watu wenye kuishi maisha ya kutangatanga kutoka Chad, Niger,Mali na Cameroon.

Sawarmi Khaled msemaji wa jeshi la Sudan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba taarifa hiyo haistahiki kuzungumziwa wakati alipoulizwa juu ya madai ya repoti hiyo.

Uchunguzi huo uliotangazwa hapo jana unakuja wakati mahakimu wa Mahkama ya Kimataifa ya Jinai wakitafakari uwezekano wa kumfungulia mashtaka Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kwa madai 10 ya mauaji ya kimbari,uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Uamuzi wao yumkini ukatolewa mwezi wa Januari.

Repoti hiyo inasema inayumkinika kwamba maelfu ya watu hao wanatoka makabila ambayo Bashir anatuhumiwa na mwendesha mashtaka wa mahkama hiyo kuamuru vikosi yake viwahilikishe, kuwateka nyara na kuwatumikisha.

Kwa kuzingatia mahojiano kuhusiana na kesi 100 repoti hiyo inasema watu wa kabila la Fur,Zaghawa na makundi mengine yasiozungumza Kiarabu hunyakuliwa wakati wa mashambulizi kwa vijiji yanayofanywa na jeshi na wanamgambo wanaoitwa Janjaweed.

Repoti hiyo imemkariri mwanamke mmoja aliyetekwa kutoka kambini akisema kwamba huwa wanawatumia kama wake zao wakati wa usiku na wakati wa mchana wanafanya kazi kutwa nzima wakipika chakula,kukusanya kuni na kuteka maji.

Pia imemkariri mvulana mmoja akisema kwamba wamekuwa wakimpiga kila siku na kumuamuru achunge wanyama wao na kwamba wamekuwa wakiambiwa kila mara kuwa wao sio binaadamu.Mvulana huyo inadaiwa kuwa alikuwa akitumikishwa kazi na kundi la Janjaweed .

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kwamba takriban watu 300,000 wamekufa na wengine milioni mbili na nusu wameyakimbia makaazi yao tokea mwezi wa Februari mwaka 2003 wakati makundi mawili ya waasi wa Dafur yaliposimama dhidi ya serikali kudai rasilmali na madaraka.

Sudan ambayo serikali yake imekuwa ikishutumiwa vikali na mataifa ya magharibi kwa kujaribu kuzima uasi huo kwa kutumia ukatili na kuwachochea wanamgambo wa Kiarabu wanaounga mkono serikali inasisitiza kwamba idadi ya vifo kutokana na mzozo huo ni watu 10,000 tu na kutupilia mbali takwimu nyengine kuwa ni njama.

 • Tarehe 17.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GHvE
 • Tarehe 17.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GHvE
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com