Maelfu waandamana Ulaya kupinga vizuizi vya Covid-19 | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 25.07.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Maelfu waandamana Ulaya kupinga vizuizi vya Covid-19

Maelfu ya raia kwenye mataifa kadhaa ya Ulaya waliandamana siku ya Jumamosi kupinga vizuizi vya kudhibiti kusambaa ugonjwa wa Covid-19 na sera za kuwalazimisha kudungwa chanjo.

Frankreich I Anti-Corona Proteste in Paris

Maandamano mjini Paris

Raia hao kwenye mataifa ya Ufaransa, Italia na Ugiriki walimiminika mitaani hususani katika miji mikuu ya nchi hizo kupaza sauti ya kupinga kulazimishwa kuchoma chanjo za Covid-19 pamoja na cheti cha kidijitali kwa wale waliopatiwa chanjo.

Wengi walioandamana wanadai sera hizo zinatishia uhuru wa raia katika wakati serikali barani Ulaya zinazidisha shinikizo dhidi ya watu amabo hawajapatiwa chanjo.

Nchini Ufaransa, kiasi watu 160,000 walijitokeza kuonesha ghadabu zao dhidi ya rais Emmanuel Macron na serikali yake mjini Paris na katika miji mingine.

Muswada mpya wa sheria chanzo cha maandamano

Frankreich I Anti-Corona Proteste in Paris

Mjini Paris maandamano yaligeuka kuwa vurugu

Waandamanaji hao wamekasirishwa na muswada mpya wa sheria unaowalazimisha raia kuwa na hati maalumu ya kudhibitisha kuwa wamechanjwa au kuonesha kwamba  hawana maambukizi ya virusi vya Corona ili waweze kuruhusiwa kuingia kwenye mikahawa na maeneo mengine ya umma.

Muswada huo ulipitishwa na Baraza la Wawakilishi siku ya Ijumaa lakini bado unajadiliwa na Baraza la Seneti.

Waandamanaji nchini Ufaransa walitumia kaulimbiu kama "Tunapinga cheti cha aibu" na wengine walibeba mabango yaliyomtaja rais Macron kuwa "mtawala wa mabavu"

Polisi ililazimika kutumia gesi ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji mji Paris baada ya kutokea makabiliano.

Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Gerald Darmanin amelaani vitendo vilivyofanywa na waandamanaji dhidi ya polisi.

Maandamano yafanyika pia Italia, Ugiriki na Ujerumani

Maandamano mengine yamefanyika nchini Italia tangu kwenye mji mkubwa wa Turin ulio kaskazini mwa nchi hiyo mji mwingine wa Naples ulio upande wa kusini.

Griechenland Athen | Protest von Impfgegnern

Waandamanaji kwenye mji mkuu wa Ugiriki, Athens

Zaidi ya watu elfu 3 walishiriki maandamano hayo ya  cheti cha kidigitali cha Corona cha Umoja wa Ulaya kinachojulikana nchini humo kama pasi ya kijani .

Hivi karibuni, serikali ya Italia imeimarisha hatua za kupambana na ongezeko la visa vya maambukizo ya virusi vya corona huku ikiweka masharti makali kwa mikusanyiko hasa kwenye viwanja vya ndani.

Kuanzia  Agosti 6, watu watahitajika kutoa uthibitisho wa chanjo, matokeo yanayothibitisha kutoambukizwa virusi hivyo ama ushahidi wa kupona baada ya maambukizo ili kuweza kushiriki katika dhifa za chakula za ndani ama kuingia katika makavazi na mabwawa ya kuogelea miongoni mwa maeneo mengine ya umma.

Mjini Athens, Ugiriki pia maelfu ya watu walijitokeza kupinga vizuizi vya kupambana na corona huku nchini Ujerumani, waandamanaji walijitokeza kwenye miji kukosoa masharti hayo ya kudhibiti kuenea kwa virusi.