1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari wa Zimbabwe waendelea na mgomo wao

Kabogo Grace Patricia14 Agosti 2009

Madaktari hao wamesema mgomo huo utasitishwa kama watapewa nyongeza ya mshahara.

https://p.dw.com/p/JBMc
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Madaktari wa hospitali za taifa nchini Zimbabwe wamekataa kusitisha mgomo wao, hadi hapo watakapoahidiwa nyongeza ya marupurupu yao ya mshahara. Mgomo huo wa madaktari unarudisha nyuma jitihada za serikali ya umoja wa kitaifa ambayo hadi sasa imeshindwa kupata msaada toka kwa wahisani wanaotaka mageuzi ya haraka ya kisiasa na kiuchumi.

Mgomo huo wa madaktari ulianza wiki hii wakidai nyongeza za mishahara na kurejeshwa kwa marupurupu yaliyoondolewa na serikali na mashirika mengine ya misaada mwezi uliopita. Rais wa Chama cha Madaktari wa Zimbabwe, Brighton Chizhande amesema madaktari hao bado wanagoma, lakini majadiliano bado yanaendelea kati yao na Bodi ya Huduma za Afya ya nchi hiyo.

Bodi hiyo imesema kuwa marupurupu kwa ajili ya nyumba, sare za kazi na malipo ya kazi za usiku hayajahusishwa katika mishahara yao ya mwezi kwa bahati mbaya na kwamba kasoro hiyo itarekebishwa. Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Lovemore Mbengeranwa amesema yalifanyika makosa katika kuondoa marupurupu hayo na kwamba hazina imekubali kasoro hiyo kwa upande wake.

Aidha, Agostino Zacharias, msemaji wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), linalotoa msaada mkubwa katika sekta ya afya nchini Zimbabwe, amesema shirika hilo linafanya kila liwezalo kuhakikisha misaada hiyo inatolewa. Zacharias amesema kuna kazi inayobidi kumaliziwa, lakini katika kipindi cha wiki mbili kazi hiyo itakamilika na fedha zitatolewa.

Hata hivyo, madaktari katika hospitali za wilaya bado hawajajiunga kwenye mgomo huo kutokana na wao kulipwa mishahara mikubwa kupitia mradi wa duniani wa kupiga vita magonjwa ya Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria.

Sekta ya afya ya Zimbabwe imekuwa katika mzozo kwa muda sasa, huku madaktari na wauguzi wakifanya migomo ya mara kwa mara wakitaka kuongezwa mishahara, huku serikali yao ikiwa ina matatizo makubwa ya uchumi kabla ya kuanzishwa kwa serikali mpya ya umoja ya kitaifa mwezi Februari, mwaka huu. mzozo huo pia ulisababisha kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu, uliosababisha vifo vya watu wapatao 4,000. Ugonjwa huo ulidhibitiwa hivi karibuni baada ya mashirika ya misaada ya kimataifa kuingilia kati.

Mageuzi ya uchumi yaliyoanzishwa na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Tendai Biti, yalionyesha matokeo mazuri ambapo madaktari walikubali kurudi kazini kwa makubaliano ya malipo madogo, lakini hapo baadaye mishahara yao ingeongezwa. Chizhande anasema kuwa serikali haiko makini, akisema kuna uwezekano wa nchi hiyo pia kukumbwa na ugonjwa wa homa ya nguruwe au hata kuzuka tena ugonjwa wa kipindupindu. Anasema hilo ni suala la kifo au uhai kwa wagonjwa.

Migomo hiyo inaonekana kuwa tishio kwa serikali ya umoja wa kitaifa, ingawa hakuna dalili ya hatari kwa serikali hiyo kuvunjika.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/DPAE/AFPE)

Mhariri:M. Abdul-Rahman