Macron azikosoa Uturuki, Urusi mzozo wa Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Macron azikosoa Uturuki, Urusi mzozo wa Libya

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameishutumu Uturuki kwa kupeleka wapiganaji wa jihadi nchini Libya, na kuelezea uingiliaji kati wa Uturuki , kuwa ni uhalifu, huku akimshutumu rais wa Urusi Vladimir Putin kwa unafiki.

Mahusiano baina ya mataifa hayo washirika katika jumuiya ya NATO yamechafuka katika wiki za hivi karibuni kuhusiana na suala la Libya, kaskazini mwa Syria na utafutaji mafuta na gesi katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterania.

Uturuki imeingilia kati katika wiki za hivi karibuni nchini Libya ikitoa usaidizi wa anga, silaha na wapiganaji kutoka katika makundi ambayo ni washirika wake kutoka Syria kusaidia serikali inayotambuliwa kimataifa mjini Tripoli kurudisha nyuma mashambulizi ya karibu mwaka mmoja yaliyokuwa yakifanywa na kiongozi wa kijeshi upande wa mashariki Khalifa Haftar.

"Nadhani ni jukumu la kihistoria la kihalifu kwa kwa nchi ambayo inadai kuwa mwanachama wa NATO," rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema.

Frankreich Türkei Präsidenten Emmanuel Macron und Recep Tayyip Erdogan

Rais Macron akiwa na rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan kabla ya uhusiano kati yao kuanza kudorora.

Bila ya kutoa ushahidi wowote kuhusu wanakotoka wapiganaji, alisema Uturuki ilikuwa 'inaingiza kwa wingi' wapiganaji wa jihadi kutoka Syria.

Ufaransa yenyewe yakana kumuunga mkono Haftar

Ufaransa imekuwa ikishutumiwa kumuunga mkono kisiasa Haftar, kwa kumpa msaada wa kijeshi hapo kabla kupambana na wanamgambo wa Kiislamu.

Ufaransa inakana kumuunga mkono Haftar lakini imeshindwa kuwakaripia washirika ewake, hususan Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, ambayo nayo imetajwa na Umoja wa Mataifa kwa kukiuka vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya Libya. Jeshi la Haftar la Libyan National Army linaungwa mkono na UAE, Misri na Urusi.

Vladimir Putin und Emmanuel Macron

Macron (kulia) na rais wa Urusi Vladmir Putin (kushoto).

Katika wiki za hivi karibuni maafisa wa Ufaransa wamesema mara kwa mara kuwa uingiliaji kati wa Uturuki unasababisha Urusi kupata ushawishi mkubwa ndani ya Libya.

Shirika la mafuta la Libya limesema siku ya Ijumaa kwamba wapiganaji mamluki kutoka Urusi wameingia katika eneo la visima vya mafuta. Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwezi wa Mei ilisema kuwa mkandarasi wa binafsi wa kijeshi wa Urusi wa kundi la Wagner lilikuwa na watu 1,200 nchini Libya.

Macron alizungumza na Putin siku ya Ijumaa , lakini alishindwa kuishutumu Moscow kama anavyofanya dhidi ya Uturuki. Alisema kwamba viongozi hao wawili wamekubaliana kufanyakazi kuelekea lengo la pamoja la makubaliano ya kusitisha mapigano.

Chanzo: rtre