Kura ya Maoni ya Uswisi Magazetini | Magazetini | DW | 10.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Kura ya Maoni ya Uswisi Magazetini

Kura ya maoni nchini Uswisi na juhudi za kupambana na ukosefu ajira nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti

Wananchi wa Uswisi wanatoa maoni yao kuhusu wahamiaji

Wananchi wa Uswisi wanatoa maoni yao kuhusu wahamiaji

Kura ya maoni nchini Uswisi ambapo asili mia 50.3 wameunga mkono kampeni ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya wahamiaji kutoka nchi za Umoja wa Ulaya imeitumbukiza katika hali ya mtafaruku serikali ya nchi hiyo na pia washirika wake wa Umoja wa Ulaya.Gazeti la"Nordwest-Zeitung" linaitathmini kura hiyo ya maoni na kuandika:"Matokeo hayo hafifu ya kura ya maoni yanaweza kuwa na madhara makubwa.Hata kabla ya kura hii ya maoni kuitishwa Umoja wa Ulaya ulionya utajibu vikali pindi Uswisi ikiamua kuleta mtengano.Kimsingi Uswisi ndio itakayoathirika zaidi-kwasababu itapoteza nafuu zote za kuingia katika soko la Umoja wa ulaya.Kila faranga moja kati ya tatu inapatikana kutokana na biashara pamoja na nchi za Umoja wa ulaya.Kupunguza idadi ya wahamiaji kutakuwa na madhara makubwa pia katika shughuli za kiuchumi ndani kwenyewe nchini Uswisi.Uswisi inategemea ujuzi na maarifa ya wahamiaji katika sekta ya ajira.Wahamiaji sasa watapima mara mbili kuona kama wanakaribishwa au la nchini humo.

Symbolbild Die Tafel

Mradi wa kuwahudumia wakosa ajira wa muda mrefu

Gazeti la "Darmstädter Echo" linaiangalia kura hiyo ya maoni kama onyo kuelekea uchaguzi wa Ulaya mwezi May ujao.Gazeti linaandika:" Kishindo sasa kitakuwa kwa upande mmoja kuepukana na balaa la kudhoofika uhusiano pamoja na Umoja wa ulaya,uhusiano ambao ndio nguzo ya shughuli za kiuchumi za Uswisi na kwa upande wa pili kutilia maanani hofu za wananchi wa Uswisi.Miaka mitatu inaonyesha itatosha kusaka njia ya kuleta uwiano katika masilahi ya kila upande.Tatizo moja lakini linabidi lishughulikiwe kuanzia sasa:Kura ya maoni nchini Uswisi ni sawa na kunyunyizia mafuta katika cheche za moto za vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vilivyodhamiria kushindana na umoja wa ulaya katika uchaguzi wa bunge la ulaya mwezi Mai mwaka huu.Wanasiasa wa Ulaya wanabidi wazingatie hofu za wananchi kuelekea umangi meza wa mjini Brussels na wayapatie ufumbuzi matatizo yaliyopo.Wakati huo Umoja wa Ulaya utaondokewa na wasi wasi."

Kishindo cha wasiokuwa na ajira kwa muda mrefu

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na juhudi za kupambana na hali ya kutokuwa na kazi nchini Ujerumani.Gazeti la "Südwest Presse "linazungumzia tarakimu za wasiokuwa na ajira na kuandika:"Tangu miaka miwili au zaidi iliyopita watu milioni tatu wanategemea msaada wa wasiokuwa na ajira kwa muda mrefu yaani Hertz nambari nne.Watu milioni moja kati yao wanaangaliwa kuwa ni shida kuwapatia kazi kwasababu ama ni wagonjwa kimwili au kiakili,hawakupata mafunzo ya kazi au hawazungumzi kijerumani.Kwasababu wanatokana na mazingira ya shida naiwe wanaotumia madawa ya kulevya na kadhalika.Watu hao hata mradi wa kubuni nafasi za kazi hautawasaidia kitu seuze tena soko la ajira hivi sasa limebadilika-ujuzi wa kazi za mikono pekee hautoshi.Lakini hiyo isiwe sababu ya kuwaacha kando watu kama hao na kusubiri wafikie umri wa miaka 58 ili wafutwe katika orodha ya wasiokuwa na ajira."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu