Kundi kubwa la watu laadhimisha kuanguka kwa ukuta wa Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kundi kubwa la watu laadhimisha kuanguka kwa ukuta wa Berlin

Mamia kwa maelfu ya watu walijipanga katika njia kuelekea katika ukuta wa Berlin kwa ajili ya sherehe zenye hisia kali kuadhimisha miaka 20 tangu kuanguka kwa ukuta.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiangalia ramani ya Ulaya. Leo ameadhimisha miaka 20 ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiangalia ramani ya Ulaya. Leo ameadhimisha miaka 20 ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin.

Mamia kwa maelfu ya watu walijipanga katika njia ya kuelekea katika ukuta wa Berlin leo Jumatatu kwa ajili ya sherehe zenye hisia kali kuadhimisha miaka 20 tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin,na kansela wa Ujerumani akipita katika kivuko cha mpakani katika mtaa wa Bornholmer kuashiria kwa mara ya kwanza Wajerumani mashariki walipoonja hali ya kuwa huru. Lakini kansela Angela Merkel amesema kuwa Ujerumani bado inaendelea kuwa na makovu ya mgawanyiko.

Viongozi wa dunia wamejiunga na kundi kubwa la watu wakikumbuka muda ambapo utawala wa kikomunist ulifikia kikomo katika Ulaya, wakati serikali ya Ujerumani mashariki hatimaye lilipofungua mpaka Novemba 9 , 1989. Merkel ambaye alikulia katika taifa hilo la kikomunist , alihudhuria misa katika kanisa ambapo maandamano ya kudai demokrasia yalifanyika , wiki kadha kabla ya utawala wa kikomunist kufikia mwisho.

Umoja wa Ujerumani bado haujakamilika, Merkel amekiambia kituo cha taifa cha televisheni ARD, akidokeza jinsi Ujerumani mashariki kuwa bado iko nyuma kuliko upande wa magharibi katika ukuaji wa uchumi, wakati ukosefu wa ajira ukiwa juu karibu mara mbili. Tunapaswa kupambana na tatizo hili iwapo tunataka kufikia hali bora ya maisha kwa wote.

Akizungumza asubuhi ya leo katika misa hiyo amesema kuwa dunia wakati wa vita baridi iligawanyika katika sehemu mbili.

Kansela ametoa tahadhari hiyo kabla ya sherehe kubwa zitakazofanyika katika lango la kihistoria la Brandenburg akiwa pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown, rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na Dmitry Medvedev wa Urusi na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton.

Kiongozi wa zamani wa iliyokuwa Urusi ya zamani Mikhail Gorbachev, rais wa zamani wa Poland Lech Walesa na wapinzani ambao walisaidia kumaliza ukomunist katika Ulaya pia watakuwapo katika eneo hilo lililopewa jina la ukanda wa kifo ambapo walinzi wa mpakani walikuwa wamepewa amri ya kuuwa.

Merkel pamoja na viongozi wengine walipita katika kivuko cha zamani katika mtaa wa Bornholmer, jioni hii ambako mamia ya Wajerumani mashariki walipata nafasi yao ya kwanza ya kuwa huru. Sherehe hizo zilihamia baadaye katika eneo la lango la Brandenburg ambako kutafanyika tamasha la wazi la muziki pamoja na tukio linaloashiria kuanguka kwa ukuta.

Kumbukumbu ya miaka 20 ya kufunguliwa kwa ukuta wa Berlin leo Novemba 9 inaingiliana hata hivyo na matukio mengine ya karne ya 20 kwa Ujerumani.

Novemba 9, 1918 wakati vita vya kwanza vya dunia vikikaribia kwisha na Ujerumani ikiwa inakaribia kushindwa, mfalme Wilhelm 11 alijing'atua kutoka majukumu ya kifalme na Philip Scheidemann kutoka chama cha Social Democratic alitangaza jamhuri ya kwanza ya Ujerumani kutoka katika dirisha la bunge la Ujerumani Reichtag. Ikijulikana kama Weimar Republic iliporomoka mwaka 1933 wakati Adolf Hitler na chama chake cha NAZI kilipotumia udhaifu wa jamhuri hiyo kuchukua madaraka.

Novemba 9, 1923, juhudi za kwanza za Hitler kunyakua madaraka, juhudi hizo zilianzia katika baa mjini Munich. Novemba 9, 1925 kikosi cha ulinzi wa viongozi SS kilianzishwa kumlinda Hitler na viongozi wengine. Novemba 9,1938, wauaji wa kundi la NAZI walifanya ghasia dhidi ya Wayahudi na mali za Wayahudi. Novemba 9, 1989, utawala wa kikomunist wa Ujerumani mashariki ukafungua milango ya ukuta wa Berlin.

Ni ajabu kuwa tarehe hii 9 inahistoria ya kufurahisha na kusikitisha kwa Ujerumani.

Mwandishi: Sekione Kitojo/ RTRE / AFPE

Mhariri : Sekione Kitojo.

 • Tarehe 09.11.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KS5j
 • Tarehe 09.11.2009
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KS5j
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com