Kumalizika enzi za Obama na Hatua za Usalama Magazetini | Makala | DW | 10.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Makala

Kumalizika enzi za Obama na Hatua za Usalama Magazetini

Kumalizika enzi za rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Hollywood yadhihirisha kutokubaliana na sera za rais mteule wa Marekani Donald Trump na mjadala kuhusu hatua za usalama nchini Ujerumani magazetini.

Tunaanzia Marekani ambapo siku kumi kutoka sasa Barack Obama ataihama ikulu ya White House baada  kuiongoza kwa muda wa miaka minane kama rais wa 44 wa Marekani. Gazeti la  Märkische Oderzeitung linaandika: "Kile ambacho Marekani, na kile ambacho ulimwengu wamekirithi kutoka kwa Obama, thamani yake itajulikana ikiwa rais mteule hatoutumia mtandao wa twitter tu, bali atatawala hasa. Yakiachwa kando yote  yale ambayo kiongozi wa ikulu ya rais, White House hawezi kuyashawishi, basi mtu anaweza kutamka kwamba mihula miwili ya rais wa kwanza wa Marekani mwenye asili ya Afrika, imefana. Na pengine hayo ndio yanayowasumbuwa wale wanaompinga."

Hollywood haikubaliani na Trump

Huko huko Marekani, wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika pia hotuba ya mcheza filamu wa kimarekani Merlyl Streep katika sherehe za kutunukiwa wasanii wa filamu tuzo ya Golden Globe huko Hollywood. Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anaandika: "Siku kumi na mbili kabla ya Donald Trump kuapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani, mliberali Meryl Streep amejitokeza kua sauti ya nguvu ya wanademokrasia ambao hawako tayari kumuunga mkono rais ambae hachelei kutumia visa vya udanganyifu, kuwakosoa wasomi na kuchochea hisia za chuki, kama njia halali za malumbano ya kisiasa. "La" ndio wito wa sekondi 347 wa Streeps katika sherehe za Golden Globe. Hayo hayataki anasema. Abadan. Sio katika nchi ya Marekani anayoijua yeye. Na sio pamoja nae. Trump huenda ameshinda uchaguzi wa rais, lakini hakushinda bado mapambano ya utamaduni ya wenye vipaji na imani nchini Marekani. Kwa mara nyengine tena Hollywood inajitokeza kama taasisi inayopigania haki katika jamii, kitovu cha siasa za kiliberali na amani licha ya nguo za ming'aro na urembo

 

Mada ya usalama yahanikiza

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mjadala unaoendelea nchini kuhusu hatua za kuimarisha usalama. Gazeti la Sächsische Zeitung linaandika: "Kufumba na kufumbua suala la usalama wa ndani limegeuka kuwa mada muhimu ya kampeni zinazokuja za uchaguzi mkuu. Mjadala unazidi kuhanikiza. Shauri la watu kufungwa chuma mguuni ni ufumbuzi wa dharura tu kuweza kuwachunguza wanapokuwa mbali, lakini halitozuwia mashambulio kutokea. Litakalosaidia zaidi ni kuzidishwa idadi ya vituo vya kuwashikilia wale wanaobidi kurejeshwa makwao, ikiwa litafanyika kuambatana na sheria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Grace Patricia Kabogo