Kombe la UEFA katika hatua ya robo fainali | Michezo | DW | 09.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la UEFA katika hatua ya robo fainali

Kocha wa Bayern Munich anamatumaini ya kushinda robo fainali

default

Kocha wa Bayern Munich Ottmar Hitzfeld

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10 uwanja wa Coliseo Alfonso Perez utakuwa umefurika mashabiki 17,000 tayari kwa robo fainali ya kombe la UEFA Bayern Munich kutoka Ujerumani na Getafe kutoka Uhispania ambao watakuwa wanachezea uwanjani mwao.


Getafe wana hamu ya kufika nusu fainali ya UEFA baada ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini Munich Ujerumani.


Wakati huo huo PSV Eindhoven inaikaribisha Florentina katika robo fainali nyingine ya UEFA.


Getafe ambayo haijawahi kushinda kombe lolote la ligi kuu imeonyesha mchezo mzuri msimu huu. Kocha wa timu hiyo Michael Laudrup ana kibarua kigumu haswa ikiangaziwa kwamba wachezaji wake wawili mlinzi Mario Alvarez na mchezaji wa kiungo cha kati Pablo Hernandez wana majereha yanayotarajiwa kupoa baada ya wiki tatu au nne.


Wachezaji wengine wa timu hiyo wenye majeraha ni wa-Agentina Oscar Ustari na Cata Diaz isitoshe mchezaji mwengine wa kiungo cha kati Esteban Granero alipigwa adhabu ya kukosa mechi inayomyima nafasi katika orodha ya wachezaji leo.


Kocha wa Bayern Ottmar Hitzfeld anaimani kwamba wachezaji wake wako katika hali nzuri zaidi ya kushinda robo fainali hiyo huku mshambulizi wa Getafe aliekomboa timu yake mjini Munich Cosmin Contra akiahidi kuipatia timu hiyo kibarua cha ziada.


Kwa upande mwengine PSV Eindhoven itaikaribisha Fiorentina katika awamu nyingine ya pili ya robo fainali ya kombe la UEFA baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya 1-1 katika awamu ya kwanza.


Mchezaji wa kiungo cha kati wa timu hiyo Ibrahim Afellay atakosa mechi ya leo kutokana na jeraha la kiwiko katika mechi ambapo timu hiyo ya Uholanzi iliichapa Heracles Almelo 2-0 na kuongoza katika ligi ya nyumbani.


Mchezaji mwengine ambaye atakosa mechi hiyo uwanjani Philips ni mshambulizi Jefferson Farfan ambaye ana adhabu ya kukosa mechi naye Danny Koevermans anaonekana akinawiri tena baada ya kuikomboa timu yake huko Florence katika awamu ya kwanza.


Fiorentina nayo inaendelea kusonga mbele baada ya kuicharaza Reggina mabao 2-0 na kuchukua nafasi ya nne ambayo itaipatia nafasi ya kushiriki katika Champions League msimu ujao.


Mchezaji wa kimataifa wa Romania Mutu aliefunga bao katika dakika za waganda wikendi iliyopita anatarajiwa kushirikiana na Claudio Prandelli kuishambulia PSV Eindhoven uwanjani mwao.


Vile vile Giampaolo Pazzini alietikisa wavu wa Reggina lakini ambaye hajafunga bao lolote katika UEFA anatarajiwa kushirikiana na Mutu katika ushambulizi.


Akihojiwa na wanahabari Mutu amesema anatarajia timu yake iliyofika katika nafasi ya nne katika siria A iingie katika fainali ya kombe la UEFA.


Wakati huo huo Mlinzi wa Rangers Carlos Cuellar anatarajia kupata nafuu na kuchezea timu yake katika robo fainali yao na Sporting Lisbon.


Mchezaji mwengine wa timu hiyo ya Scotland ambaye huenda akawa amepoa jeraha ni Daniel Cousin alieumia mdomo katika mechi dhidi ya Werde Bremen.


Bayer Luverkusen inaelekea Zenit St. Petersburg ikiwa na matumaini machache baada ya kucharazwa mabao 4-1 katika awamu ya kwanza iliyochezwa Ujerumani.


Cocha wake Michael Skibbe anasema licha ya kuwa na matumaini machache timu yake inatarajia kujifuta machozi na kuondoa aibu iliyopata nyumbani.


Hata hivyo Michael amedokezea kwamba timu hiyo inatazama Bundesliga wikendi ijayo dhidi ya Stuttgart kwasababu iko nambari sita nyuma ya Stuttgart katika msimamo wa ligi hiyo.

 • Tarehe 09.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Df3r
 • Tarehe 09.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Df3r
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com