Kombe la dunia 2010 kanda ya Ulaya na Afrika: | Michezo | DW | 09.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la dunia 2010 kanda ya Ulaya na Afrika:

Ujerumani na Urusi :Kamerun,I.Coast na Tunisia kuifuata Ghana ?

default

Kocha Loew na nahodha Ballack

KINYAN`GANYIRO CHA TIKITI ZA KOMBE LA DUNIA 2010:

Simba wa nyika,Kamerun,tembo wa Ivory Coast,Algeria na Tunisia zaqweza kukata tiketi zao mwishoni mwa wiki hii na kujiunga na Ghana katika kombe la dunia mwakani nchini Afrika Kusini.Ujerumani ina miadi leo na Russia kuamua nani anachukua tiketi ya kwanza ya kundi hilo kwa Kombe la dunia.

KANDA YA AFRIKA KOMBE LA DUNIA:

Algeria,Kamerun,Ivory Coast na Tunisia ni zamu yao leo (Jumamosi) na kesho (Jumapili )kujiunga na Black Stars-Ghana iliokwisha toroka na tiketi yake ya kwenda mwakani Afrika kusini:

Tembo wa Ivory Coast,wanahitaji pointi 1 tu kutoka Malawi, kufuzu kucheza Kombe lijalo la dunia kutoka kundi E.Na hii itakuwa kwa mara ya pili kwa Corte d'Iviore kulisakata dimba katika kombe la dunia baada ya 2006 nchini Ujerumani.Timu 3 nyengine zinahitaji msaada kutimiza ndoto yao ya kuandika historia katika kombe la kwanza kabisa la dunia barani Afrika 2010.

Algeria,iliocheza Kombe la dunia mara ya mwisho miaka 23 iliopita, inaweza nayo kuparamia kileleni mwa kundi C ikiwa kesho itatamba bora zaidi mbele ya Rwanda kuliko mabingwa wa Afrika, Misri, wanaokabili rissi kali za "Chipolopolo" mjini Lusaka,Zambia hii leo.

KAMERUN:

Simba wa nyika-Kamerun,walioimarika tangu kurejea kwa kocha wao mpya mfaransa Paul le Guen, watatia fora usoni kabisa katika kundi A wakiwalaza watogo nyumbani jioni hii na simba wa Atlas-Morocco, wakiishinda Gabon iliopo nafasi ya pili ya kundi lao leo.Kocha wao Le Guen,alieiongoza klabu ya Ufaransa, Lyon kutoroka na taji la ubingwa mara 4 nchini Ufaransa,ameijenga upya Kamerun na kuitundika kileleni mwa kundi A.

Simba wanyika, wameshinda nyumbani na ugenini dhidi ya Gabon mwezi uliopita.Miongoni mwa hatua alizochukua kocha huyo, ni kuwaweka ubaoni kupumzika nahodha Rigobert Song na kumvika unahodha stadi wa zamani wa FC Barcelona na "mchezaji bora wa mwaka wa Afrika" -Samuel Eto-o.Pia alimuita kujiunga na kikosi cha Taifa kutoka Spain, Achille Webo.

Tunisia waliotamba pia kama Ivory coast katika kombe lililopita la dunia Ujerumani, wanaweza kufuzu kwa mara ya 4 kucheza kom,be la dunia mradi tu wazime vishindo vya harambee Stars-Kenya katika patashika za kundi B.

Tunisia tzayari inaongoza kwa pointi 2 kuliko mahasimu wao Nigeria.Kwani, watunisia walithubutu kuzima vishindo vya Super eageles kwao Abuja na kuondoka sare ya mabao 2:2 na pointi 1. Harambee Stars, sasa inasindikiza tu na kocha wao mzaliwa wa ujerumani Antoine Hey,aliejipatia ushindi 1 tu katika kinyanganyiro hiki cha kufuzu kwa Kombe la dunia 2010,amempiga kumbo stadi maarufu wa "Harambee Stars",Denis Oliech kwa mpambano huu huko Rades,Tunisia.

BLACK STARS:

Tayari Ghana imekata tiketi yake baada ya stadi wa Chelsea, Michael Essien, kukomea mabao 2 katika lango la Sudan duru iliopita.

Tembo wa Ivory Coast,imekumbwa na majeruhi wengi kabla changamoto yao katika Kamuzu Stadium mjini Blantyre na Malawi.Ivory Coast, inabidi kucheza bila ya mlinzi wao mashuhuri kutoka Manchester City, Kolo Toure,mchezaji wa kiungo Cheik Tiote na mshambulizi Kader keita na hata mshambulizi wao Abobacar Sanogo anaecheza katika Bundesliga.Hatahivyo, mastadi wa Chelsea akina Didier Drogba na Salomon Kalou watakuwa uwanjani Tembo wa Afrika magharibi kuwakanyaga wa Malawi waliowatandika mabao 5-0 mwezi Machi,mwaka huu mjini Abidjan.

AFRIKA KUSINI:

Bafana Bafana au Afrika kusini, wanaocheza Jumamosi hii mpambano wa kirafiki na Norway na dhidi ya Iceland Jumaane hii ijayo, hawakuhitaji kufuzu kwa Kombe la dunia kwavile, ni wenyeji waingia bila kupingwa.Na hii inalipa bara la Afrika nafasi 6 katika timu 32 zitakazoteremka uwanjani Afrika kusini Juni, mwakani.Duru ya mwisho ya kuania kufuzu kwa kombe la dunia kanda ya Afrika itachezwa Novemba 14.Je, Nigeria itakosa tena kuwakilisha Afrika barani Afrika katika Kombe la dunia ?

Wakati washindi 5 kutoka makundui 2 mbali wataelekea kombe la dunia Juni 11, hadi finali Julai 11 mwakani,timu zilizomaliza nafasi ya 3 kutoka kila kundi zitafuzu kwa kombe la Afrika la mataifa linaloanza Januari 10 hadi 31,2010 nchini Angola.Macho ya mashabiki wa bara zima la Afrika kwahivyo, yanakodolewa wikiendi hii barani Afrika:

KANDA YA ULAYA: UJERUMANI NA URUSI:

Jioni ya leo, sio tu kanda ya Afrika inaania kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia, bali hata ile ya Amerika Kusini na Ulaya.Wakati katika kanda ya Amerika Kusini, hatima ya Argentina na kocha wake Diego Maradona, imo mashakani, mashabiki wa Ujerunmani wananinginiza wakati huu roho kujua iwapo leo timu yao ikiongozwa na nahodha Michael Ballack itamudu alao sare na kukata na mapema tiketi ya Afrika kusini.

Urusi,lazima ishinde ikiwa iparamie kileleni mwa kundi hili. Mohammed Abdulrahman anawafunulia kawa kanda ya Ulaya:Urusi imeandaa mtego wa kuinasa Ujerumani-jioni hii -nao ni uwanja wao usio na majani ya kawaida-artificial pitch- pamoja na mkuki na nahodha wao Andrei Arshavin. Kwani, warusi wakicheza nyumbani, wanahitaji leo ushindi kutoka kundi hili la 4.Wakitoka sare, wanaweza kubakia usoni mwa kundi hili mraditu, waitimue Finland katika mpambano wao wa mwisho mjini Hamburg.Kwa ufupi, Russia, inahitaji ushindi katika mapambano yote 2 hii leo na hata Jumatano ijayo ili kwenda Afrika kusini. Na nahodha wa Russia, Arshavin, ametia mabao 2 katika mapambano ya Arsenal, huko Uingereza na wajerumani wamezisikia salamu hizo alizowatumia. Wajerumani leo kazi yao itakuwa kujilinda,kwani walishinda duru iliopita nyumbani kwa mabao 2:1.

Warusi hawakuwahi kuishinda Ujerumani katika mashuindano nje ya yale ya kirafiki, na hivyo leo, uwanja wa LUZHNIKI STADIUM, mjini Moscow,eti ni kaburi walilowachimbia wajerumani kuwakumbusha kile kilichowakuta katika vita vya pili vya dunia walipojaribu kuuteka mji wa Moscow. Warusi wanaamini: "kila kitu kina mwisho wake". Na leo zamu ya wajerumani imewadia.

Hata warusi lakini, hawakucheza katika uwanja huu wa Luzhniki tangu walipowakomea waingereza mabao 2-1 katika Kombe la ulaya la 2008.Lakini, kocha wao mholanzi Guus Hiddink, ni mchawi katika kuziongoza timu zaTaifa katika kombe la Dunia.Alifanya hivyo na Korea ya kusini alioiongoza hadi nusu-finali 2002.Kwahivyo, wajerumani wachunge leo.

UFARANSA:

Ufaransa na Ureno zina wasi wasi wa kukosa tiketi za Afrika kusini.Alao leo, wafaransa bila ya jogoo lao Franck Ribery, watazamiwa kuwika mbele ya visiwa vidogo vya Faroe Islands wakati Ureno na stadi wao Cristiano Ronaldo ,hatima yao si nzuri lakini Afrika Kusini bila ya Cristiano Ronaldo au Kaka itakuaje ? Ureno hajakata bado tamaa.

Ufaransa lakini, inajikuta katika kundi linalojumuisha pia Austria,Rumania na Lithuania.Ufaransa, ilianza vibaya kinyanganyiro chake cha kwenda Afrika kusini.Ilikandikwa mabao 3-1 na Austria na ingawa Ufaransa imepata nguvu kidogo hivi sasa ,haioneshi ni timu inayoweza kutawazwa tena mabingwa wa dunia huko Afrika kusini.Le Blues iko nafasi ya pili katika kundi lake na pointi 4 nyuma ya viongozi Serbia.

Mabingwa wa dunia Itali, hawana wasi wasi ,kwani kikosi cha kocha Marcello Lippi, kikiitimua leo Ireland ,tiketi yao itakua mfukoni.Waireland alao wamudu sare kubakia hayi mashindanoni.

UINGEREZA:

Kocha wa Uingereza ,mtaliana Fabio Capello, ameionya timu yake isifanye uzembe ikiwa njiani kwenda Afrika Kusini.Ushindi katika mpambano wake wa mwisho leo huko Ukraine na baadae, nyumbani dhidi ya Belorusia Jumatano ijayo, utakamilisha ufanisi wa mechi 10 kwa kikosi cha Capello na kufuta madhambi ya kutoshiriki katika kombe la ulaya 2008 kwa kutolewa na Russia.

Mabingwa wa ulaya Spain na Holland tayari zimeshafuzu kwa Kombe lijalo la dunia.Zinasubiri tu firimbi kulia Juni 11 hadi finali Julai 11,2010 mjini Johannesberg.

Muandishi: Ramadhan Ali /AFPE/DPAE

Mhariri: M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com