Kesi ya maharamia wa kisomali yaanza kusikilizwa Uholanzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kesi ya maharamia wa kisomali yaanza kusikilizwa Uholanzi

Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Rotterdam.

default

Picha ya kuchora ya maharamia wa kisomali wakiwa katika mahakama ya Rotterdam, Uholanzi.

Kesi ya kwanza kabisa barani Ulaya ya watu wanaotuhumiwa kuwa maharamia wa kisomali imeanza kusikilizwa hii leo huko Rotterdam nchini Uholanzi. Watuhumiwa hao watano wanaotuhumiwa kukata kuiteka nyara meli ya mizigo ya Uholanzi, wameendelea kusisitiza kwamba wao ni wavuvi wa kawaida ambao nao pia walizingirwa.

Watuhumiwa hao walikamatwa mwezi Januari mwaka uliopita baada ya kutuhumiwa kujiandaa kuiteka nyara meli ya mizigo iliyokuwa na bendera ya Uholanzi katika Ghuba ya Aden kwa kutumia silaha na roketi. Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya mashua yao kuzingirwa na meli ya Uholanzi. Amri ya kukamatwa ilitangazwa wiki tatu baadae na tangu wakati huo Wasomali hao wamekua wakishikiliwa nchini Uholanzi. Baada ya kuingia mahakamani, watuhumiwa hao waliwasalimu kwa tabasamu mawakili wao, huku wakisindikizwa na polisi na vyombo vya habari vya kimataifa vikiifuatilia kesi hiyo.

Jaji anayeongoza kesi hiyo, Jan Willem Klein Wolterink, aliwaambia watuhumiwa hao Farah Ahmed Yusuf, Jama Mohamed Samatar, Sayid Ali Garaar, Abdirisaq Abdulahi Hiesi na Osman Musse Farah kuwa kesi yao imeanza rasmi kusikilizwa baada ya kuwaapisha wakalimani watatu. Hata hivyo, Farah aliiambia mahakama ya wilaya ya Rotterdam kwamba lengo lao lilikuwa kuvua samaki na kwamba wakati wanajiandaa kuvua papa, injini ya meli yao iliharibika na hivyo wakataka msaada kutoka kwenye meli hiyo ya Uholanzi ya Samanyolu. Amesema yeye na wenzake hawakufyatua risasi za aina yoyote ile katika meli hiyo. Watuhumiwa hao wameendelea kusisitiza kwamba hawahusiki na madai hayo dhidi yao.

Upande wa mashitaka umedai kuwa kundi hilo la maharamia liliongeza mwendo wa boti yao ndogo kuelekea katika meli hiyo ya Uholanzi, huku ndani ya boti hiyo kukiwa na roketi na bunduki. Wakili mmoja wa watuhumiwa hao watano amesema wanapinga hatua ya kufikishwa mahakamani wateja wao nchini Uholanzi. Aidha, msemaji wa mahakama hiyo, Vincent de Winkel ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa kesi hiyo inatazamiwa kuendelea kwa siku tano mjini Rotterdam na hukumu itatangazwa Juni 16 mwaka huu. Iwapo watapatikana na hatia ya kutaka kuiteka nyara meli, watuhumiwa hao watano watakabiliwa na hukumu ya kifungo cha hadi miaka 12 jela.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la safari za baharini lenye makao yake makuu mjini London, Uingereza, maharamia waliziteka nyara jumla ya meli 215 za kibiashara katika pwani ya Somalia mwaka uliopita. Jumanne iliyopita, mahakama moja ya Yemen iliwahukumu maharamia sita wa Kisomali adhabu ya kifo na wengine sita kifungo cha miaka kumi jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuiteka nyara meli ya mafuta ya Yemen na kuwaua mabaharia wake wawili, mwezi Aprili, mwaka uliopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 25.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NWlg
 • Tarehe 25.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NWlg
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com