1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aelekea Ethiopia na Kenya.

4 Mei 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz siku ya Alhamisi ameanza ziara yake ya pili barani Afrika kama kansela wa Ujerumani. Mkondo wa kwanza wa safari yake unaanzia nchini Ethiopia halafu atakwenda Kenya.

https://p.dw.com/p/4QsqF
Kanzler Scholz reist nach Afrika
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika ziara hiyo kansela wa Ujerumani huko nchini Ethiopia atafanya mazungumzo na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kiongozi wa muda wa utawala wa eneo la Tigray, Gatchew Reda, na vilevile Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde. Scholz pia atakutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat. Kiongozi huyo wa Ujerumani na maafisa wa Umoja wa Afrika wanatarajiwa kujadili namna ya kudhibiti migogoro barani Afrika, ikiwa ni pamoja na mapigano ya sasa ya nchini Sudan.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: FABIAN BIMMER/REUTERS

Kansela wa Ujerumani ameandamana na wawakilishi wa makampuni ya Ujerumani. Baadae leo jioni, kansela Scholz atakwenda Kenya, nchi ambayo ni mshirika muhimu wa Ujerumani katika kanda ya Afrika Mashariki. Safari ya kansela wa Ujerumani inazingatia zaidi juu ya kutatua migogoro, majukumu ya kulinda amani, mabadiliko ya hali ya hewa, nishati safi, pamoja na athari ya vita vya Urusi nchini Ukraine.

Soma:Kansela wa Ujerumani kuzuru Kenya na Ethiopia

Scholz atatembelea mradi mkubwa zaidi barani Afrika wa nishati ya joto ardhi, mradi huo uko katika ziwa Naivasha. Naivasha ni mji ulio katika Kaunti ya Nakuru, iliyo umbali wa kilomita 92.8 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Kushoto: Rais wa Kenya William Ruto. Kulia: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.
Kushoto: Rais wa Kenya William Ruto. Kulia: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: Political-Moments/IMAGO

Kenya inazalisha sehemu kubwa ya umeme wake kutoka kwenye vyanzo mbadala na kwa sasa inatafuta kuongeza uwezo wake kwa lengo kuwezesha ukuaji wa haraka wa viwanda. Hata hivyo, nchi hiyo inakabiliwa na matatizo ambapo hakuna umeme wa kutosha wa kuweza kutumika viwandani na hali hiyo inasababisha ugumu katika kuvutia uwekezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu nchini Kenya.

Wakati ziara ya kansela wa Ujerumani nchini humo, Rais William Ruto anatarajiwa kuendelea kuitangaza nchi yake kama nchi ambayo wawekezaji wakubwa wa Ujerumani wanaweza kuwekeza katika sekta ya viwanda itakayoongeza chachu ya kukuza zaidi miundombinu itakayoleta faida kubwa kwa pande zote.

Soma:Umoja wa Ulaya yaahidi kuongeza uwekezaji nchini Kenya

Olaf Scholz alifanya ziara yake ya kwanza barani Afrika kama kansela mnamo mwezi Mei mwaka 2022, muda mfupi baada ya kuingia bara la Afrika kama mshirika muhimu wa kimkakati wakati ambapo kuna ushindani mkubwa wa ushawishi kati ya nchi za magharibi na wapinzani wao, Urusi na China.

Vyanzo: DPA/RTRE