Kampeni ya uchaguzi wa bunge yaanza nchini Angola | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kampeni ya uchaguzi wa bunge yaanza nchini Angola

Wasiwasi wajitokeza kwamba uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki

default

Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos

Uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika nchini Angola mnamo tarehe 5 mwezi ujao wa Septemba utakuwa mtihani mkubwa kwa rais wa sasa Jose Eduardo dos Santos, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1979. Mtihani wake wa pili ni uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka ujao ingawa bado rais huyo anasubiriwa kuthibitisha ikiwa atagombea wadhifa huo.

Chama cha rais dos Santos cha Popular Movement for the Liberation of Angola, MPLA, kimekuwa madarakani kwa miaka 33 na habari zinazoipongeza miradi ya ujenzi na kijamii zimekuwa mabango pekee yaliyobandikwa kando ya barabara kufikia hivi sasa. Picha za rais dos Santos na chama cha MPLC pia zimewekwa kila mahala katika miji mikubwa nchini kote, ambako asilimia 70 ya wakaazi wanaishi chini ya kiwango cha dola mbili kwa siku licha ya Angola kuwa na ushindani mkubwa na Nigeria kama mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika.

Mchambuzi wa maswala ya siasa, Ismael Mateus ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hii ni propaganda ya chama cha MPLA ikifanya kazi. Amesema chama hicho kina nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi nchini Angola kwa kuwa kimekuwa madarakani kwa mda mrefu, kina vyombo vyote na taasisi zote upande wake na kinaweza kuonyesha kazi nzuri kilichofanya nchini humo. Barabara zimekarabatiwa, daraja, shule na hospitali zimejengwa.

Katika mkutano wa hadhara mwishoni mwa juma hata kabla kampeni rasmi kuanza, chama cha MPLC, kiliahidi kufanya kazi kuijenga upya Angola kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mnamo mwaka wa 2002. Katibu mkuu wa chama cha MPLC, Juliao Mateus Paolo amewaambia wafuasi wa chama hicho kwamba wameanzisha mchakato wa kuijenga upya nchi hiyo katika kila pembe. Aidha kiongozi huyo alirudia ahadi zilizotolewa na rais dos Santos kujenga nyumba mpya milioni moja nchini kote. Hivi majuzi rais dos Santos ameahidi kufanya uchaguzi utakaokuwa mfano bora kwa ulimwengu.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na vuguvugu la zamani la waasi, UNITA, Isaias Samakuva, ameahidi Angola itazuia mgogoro wa kisiasa kama ile iliyotokea nchini Zimbabwe na Kenya.

Serikali itatoa kiasi cha zaidi ya dola milioni moja katika kudhamini kampeni za vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi huo wa bunge, lakini makundi ya upinzani yamesema bado yanasubiri kupokea fedha hizo. Joao Antonio wa chama cha upinzani cha Party for Democratic Progress na muungano wa kitaifa nchini Angola, amesema kiwango cha fedha kitakachopewa kila chama ni kidogo mno kiasi kwamba hakitatosha kugharamia kampeni.

Filomeno Vieira Lopes, mwenyekiti wa chama cha Front for Democracy, amesema ana matumaini fedha hizo hazitatolewa baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi kutangazwa kama ilivyofanyika mnamo mwaka wa 1992.

Waangalizi wa Umoja wa Afrika wamealikwa kusimamia uchaguzi wa Angola na Umoja wa Ulaya umeanza kupeleka ujumbe wa wanachama 90 nchini humo. Vyama kumi na miungano minne imeidhinishwa kushiriki katika uchaguzi huo wa bunge na kuanzia hii leo kila chama kitapewa dakika tano za matangazo kila siku kwenye runinga ya kitaifa na dakika 10 kwenye redio ili kutangaza sera zao.

Wagombea 5,198 watashindania viti 220 vya ubunge, huku Waangola zaidi ya milioni nane wakiwa wameandikishwa kupiga kura. Chama cha MPLA kitapambana na hasimu wake UNITA katika uchaguzi huo wa kwanza wa bunge katika kipindi cha miaka 16. Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulifanywa wakati wa usitishwaji mapigano kati ya chama cha UNITA na majeshi ya serikali.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ilifanyika wakati huo huo, lakini duru ya pili ikafutwa baada ya kiongozi wa UNITA Jonas Savimbi kudai kulikuwa na mizengwe wakati wa uchaguzi huo. Kifo chake mnamo mwaka wa 2002 kilidhihirisha kuwa na jukumu kubwa katika kumaliza mapigano yaliyosababisha vifo vya watu nusu milioni tangu vita vilipoanza mnamo mwaka wa 1975, mda mfupi baada ya Angola kujipatia uhuru wake kutoka kwa Ureno.

 • Tarehe 04.08.2008
 • Mwandishi Charo,Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EqJS
 • Tarehe 04.08.2008
 • Mwandishi Charo,Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EqJS
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com