Kamishna wa masuala ya uchumi wa Umoja wa ulaya ziarani nchini Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kamishna wa masuala ya uchumi wa Umoja wa ulaya ziarani nchini Ugiriki

Ugiriki yatazamiwa kutangaza hatua ziada ili kujikwamua toka mgogoro wa kiuchumi

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya kiuchumi Olli Rehn (kushoto) na mwenyekiti wa zoni ya yuro Jean-Claude Juncker

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya kiuchumi Olli Rehn (kushoto) na mwenyekiti wa zoni ya yuro Jean-Claude Juncker

Kamishna wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya kiuchumi Olli Rehn na Jürgen Stark,ambae ni mwanachama wa bodi ya magavana wa benki kuu ya Ulaya wamekwenda Athens hii leo kuzungumzia matatizo ya bajeti ya Ugiriki.

Ripota wa shirika la habari la Reuters amewaona madhamana hao wawili wa Ulaya ndani ya jengo la wizara ya fedha ya Ugiriki.Benki kuu ya Ulaya ikathibitisha baadae ziara ya bwana Jürgen Stark ambayo haikutangazwa hapo awali kinyume na ile ya kamishna wa masuala ya kiuchumi Olli Rehn.

Ugiriki imepewa muda wa hadi March 16 ijayo kuwatanabahisha mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya kuhusu hatua za kutosha ilizochukua ili kupunguza kwa asili mia nne nakisi ya bajeti yake kwa mwaka huu.

Olli Rehn ameanza ziara yake kwa kuzungumza ana kwa ana na waziri wa fedha Georges Papaconstantinou.Viongozi hao wawili wamepangiwa baadae kukutana na Jürgen Stark na viongozi wengine wa Ugiriki.

Kamishna huyo wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya kiuchumi amepangiwa pia kukutana na waziri wa uchumi Louka Katseli,waziri wa ajira Andrea Loverdos na mkuu wa benki ya Ugiriki George Provopoulos.

"Nnaitaka serikali ya Ugiriki ipitishe hatua ziada siku zijazo" amesema Olli Rehn baada ya mazungumzo pamoja na waziri wa fedha wa Ugiriki George Papaconstantinou aliyeahidi kwa upande wake "hatua ziada zitachukuliwa ikihitajika.

Waziri wa uchumi,Louka Katseli alisema jana Ugiriki huenda ikatangaza hatua ziada hivi karibuni ili kupunguza nakisi ya bajeti,katika wakati ambapo makubaliano kuhusu mpango wa kuisaidia Ugiriki yanakurubia kufikiwa kati ya Athens na washirika wake wa Ulaya.

Griechenland Finanzkrise Ministerpräsident George Papandreou

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou

Waziri mkuu George Papandreou amewalaumu wanaorahisisha mitindo ya rushwa na hisia za kutojali kitu ,akiwatolea mwito wagiriki waunge mkono mpango wake wa kufunga mkaja ili kuikwamua Ugiriki toka shida za kiuchumi.

Mgogoro wa kiuchumi wa Ugiriki ulisababisha kupungua kwa pointi 322 thamani ya hati za serikali ya nchi hiyo katika soko la hisa la mjini New-York ijumaa iliyopita.

Thamani za hati za serikali za Ureno na Hispania nazo pia zimeathirika kutokana na hali hiyo.

Hata hivyo thamani ya hati za benki za ugiriki imepanda kwa asili mia 3 leo mchana ikilinganishwa na zile za Ulaya zilizopungua kwa kadiri asili mia 1.28.

Mwenyekiti wa umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya Yuro-Jean Claude Juncker amesema huenda Umoja wa Ulaya ukachukua hatua ili kuwazuwia walanguzi wanaobahatisha katika masoko ya hisa.

Mhariri:Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na :Othman Miraji

 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MG8s
 • Tarehe 01.03.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MG8s
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com