1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamala Harris akamilisha ziara yake nchini Tanzania

Sylvia Mwehozi
31 Machi 2023

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ametangaza mpango wa kukuza biashara na Tanzania wakati alipokutana na mwenyeji wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kumsifu kama "bingwa wa demokrasia."

https://p.dw.com/p/4PXkz
Kamala Harris Tansania Samia Suluhu Hassan
Picha: via REUTERS

Kamala Harris, amesema kuwa Benki ya Exim, wakala wa mikopo wa Marekani, watasaini mkataba wa makubaliano ambao utawezesha kiasi cha hadi dola milioni 500 za mauzo ya nje ya Tanzania katika sekta za uchukuzi, miundombinu, teknolojia ya dijitali na miradi ya nishati safi. Katika mkutano wa pamoja na mwenyeji wake Rais Samia, Harris alisema kuwa shabaha ya Marekani ni "kushirikiana na kuongeza uwekezaji Tanzania pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi" wa nchi hizo mbili. Aidha, makamu huyo wa Rais wa Marekani alitangaza mipango zaidi ya kushirikiana na Tanzania katika sekta za teknolojia ya 5G na usalama wa mtandao.

Tansania Kamala Harris
Kamala Harris katika eneo la kumbukumbu la wahanga wa shambulio la bomu jijini Dar es salaam mwaka 1998.Picha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Harris alimuelezea Samia, rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania ambaye amekuwa akirudisha nyuma sera za kimabavu za mtangulizi wake hayati John Magufuli, kuwa ni "bingwa" wa demokrasia.

"Mheshimiwa Rais, chini ya uongozi wako, Tanzania imepiga hatua muhimu na za maana na mimi na Rais Joe Biden tunakupongeza. Umekuwa wazi kufanya kazi na wapinzani wa kisiasa, tumelijadili hilo. Umeondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mlifanya kazi kuboresha uhuru wa vyombo vya habari," alisema makamu wa Rais Harris.

Kwa upande wake, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliutaja mkutano huo kama "hatua ya kihistoria" na kumtaja Harris kama "dada" na mwanamke wa kwanza Mweusi kuchaguliwa kuwa makamu wa rais.

"Leo, Tanzania imepiga hatua nyingine ya kihistoria, ambapo viongozi wawili wa kike, Rais na Makamu wa Rais wamekutana hapa Ikulu jijini Dar es Salaam. Mkutano huu unafanyika wakati wa mwezi wa kihistoria wa kuwaenzi wanawake wa Machi. Ni msukumo na ushuhuda kwa wasichana wa Kitanzania! Karibu sana"

Kamala Harris Tansania Samia Suluhu Hassan
Kamala Harris akiwa amesimama na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle alipokuwa akizungumza na manusura wa shambulio la bomu mwaka 1998Picha: REUTERS

Harris yupo ziarani Afrika katika mataifa matatu ikiwa ni msukumo wa hivi karibuni wa Marekani wa kuimarisha ushiriki wake barani humo na kukabiliana na ushawishi unaozidi kuongezeka wa China na Urusi. Tanzania haijaegemea upande wowote katika vita vya Ukraine na kutoshiriki katika kura ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Urusi na kutaka mzozo huo kusuluhishwa kwa njia za kidiplomasia. Mnamo mwezi Novemba, Rais Samia aliitembelea Beijing na kufanya mazungumzo na Rais wa China, Xi Jinping.

Siku ya Alhamis, Harris aliweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu ya mashambulizi ya mabomu dhidi ya ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998. Makamu huyo wa Rais pia ameisifu serikali ya Tanzania kwa "hatua zake za uwazi" katika kushughulikia mlipuko wa virusi vya Marburg ambavyo viliwaua watu watano, na kutangaza kuwa shirika la misaada la Marekani USAID litatoa msaada wa dola milioni 1.3 kusaidia juhudi hizo. Wakati akikamilisha ziara yake nchini Ghana ambayo ilikuwa ndio kituo chake cha kwanza, Harris alitangaza mpango wa zaidi ya dola bilioni 1 wa kuimarisha uwezeshaji wa wanawake barani Afrika. Kiongozi huyo ameelekea Zambia siku ya ijumaa.

Soma pia: Kamala aanza ziara ya siku tatu nchini Tanzania

Rais Samia ambaye alitimiza miaka miwili madarakani mnamo Machi 19 mwaka huu, ameonekana kubadilisha sera za mtangulizi wake ambazo zilitoa dosari sifa ya Tanzania kuwa nchi yenye utulivu. Mapema mwezi huu, Samia aliapa kurejesha siasa za ushindani na kuharakisha mchakato uliokwama wa kupitia katiba, ambalo limekuwa hitaji la muda mrefu la upinzani.