1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamala Harris aisifu Tanzania kuwa bingwa wa demokrasia

George Njogopa 30 Machi 2023

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amekaribisha hatua zinazochukuliwa na Tanzania za kujenga ustawi bora wa kidemokrasia na ameahidi kuendelea kushirikiana na taifa hilo katika kukuza fursa za uchumi na maendeleo.

https://p.dw.com/p/4PWJJ
Tansania Kamala Harris
Picha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Kamala amesema ustawi bora wa demokrasia kwa nchi za Afrika ndiyo msingi na imani ya serikali ya Marekani na kwa maana hiyo utawala wa Rais Joe Bieden utaendelea kuonyosha  mkono wake na mataifa yanayozingatia dhamana hiyo.

Amesema Tanzania imechukua mkondo mpya unaotoa matumaini yanayoonyesha ni kwa kiasi gani matakwa ya kuheshimu demokrasia ya raia inavyopaswa kuzingatiwa hivyo Washington inakaribisha hatua zote za mabadiliko ya kidemokrasia yanayoendelea kutekelezwa.

Kamala Harris atangaza mipango ya kuimarisha biashara na Tanzania

Mbali ya eneo hilo, kiongozi huyo wa Marekani aliyeko nchini kwa ziara ya siku tatu amejadili umuhumu wa kuendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake akisema mwanamke anapofungulia njia jamii inakombolewa katika minyororo yote ya ukandamizaji.

Ama amedokeza ni kwa nini pande hizo mbili zinavyopaswa kuwa na sera  madhubuti katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa kwa kutilia maanani vita vya Urusi na Ukraine vilivyovuruga mchororo wa utegemezi wa  bidhaa kama ngano na mbole zinazozalishwa kwa wingi kutoka katika eneo hilo lenye vita.

Tanzania na Marekani kuenzi uhusiano wao

Kamala Harris Tansania Samia Suluhu Hassan
Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris akiwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhusu HassanPicha: via REUTERS

Yeye na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan wamekubaliana pia namna wanavyopaswa kuendelea kuenzi uhusiano wa kihistoria kwa mataifa hayo mawili na kwamba Rais Samia amedokeza shabaha ya Tanzania ya kutaka kuona uhusiano huo ukigeukia zaidi maeneo ya uwekezaji na utalii.

Kamala aanza ziara ya siku tatu nchini Tanzania

Amesema hivi karibuni nchi hizo mbili zinatarajia kuwa na mazungumzo ya kina kuangazia maeneo yatayowezesha mazingira bora ya uimarisha ushirikiano wa kibiashara na eneo mojawapo linalokusudiwa kutupiwa macho ni lile linalohusu kupanua wigo wa utoaji wa visa.

Ziara ya Kamala barani Afrika, inatazamwa na wengi kama juhudi za Marekani kuimarisha ushawishi wake barani humu, bara ambalo linamulikwa kwa karibu na mataifa yaliyoendelea, yakikodolea macho rasilimali zilizopo.

Kwa ujumla, Marekani inajaribu kuimarisha ushirika wake na Afrika, katikati ya ushindani mkali na nchi nyingine hususan China. China imewekeza pakubwa barani Afrika lakini Marekani inajipanga kama mshirika bora kuliko China.

Mwandishi: George Njogopa