Juhudi za kuuokoa mfumo wa fedha wa Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Juhudi za kuuokoa mfumo wa fedha wa Marekani

Mfumo wa fedha wa Marekani angalau umeokolewa kwa sasa

Kishindo kikubwa katika Soko la Hisa la Wall Street, mjini New York, Marekani

Kishindo kikubwa katika Soko la Hisa la Wall Street, mjini New York, Marekani

Mtu yeyote anapoweka akiba yake ya fedha benki, hujihisi hana wasiwasi, fedha hizo ziko salama salimina; ni salama zaidi kuliko vile angezificha chini ya godoro analolalia. Zaidi ni kwamba huko benki, si tu zinalindwa vya kutosha, lakini zinajipatia faida ya riba, na kama unashawishiwa na wenye mabenki, unaweza ukajitumbukiza katika biasahara ya kununua hisa za makampuni. Mchezo wa pata potea. Lakini mambo sio rahisi hivyo hivi sasa. Ni tu wiki iliopita nilipowaona wanasiasa wakuu wa serekali za hapa Ulaya wakichomoza kwenye televisheni na kuwahakikishia wananchi wao kwamba fedha zao kwenye mabenki ni salama. Na yote yameanzia katika nchi kubwa inayoongoza katika mfumo wa masoko huru na ubepari, Marekani, pale mabenki makubwa yalipoanza kufilisika na serekali ikabidi isiwe na njia nyingine ila kuvunja mwiko wa msingi wa ubepari na masoko huru, dola kujiingiza na kuyanusuru mabenki yaliokuwa yanafiliska. Ilikuwa sio kazi rahisi. Mpango wa rais Bush kwa serekali kutoa dola bilioni 700 kuyapiga jeki mabenki ya Marekani ulipata upinzani mkali katika baraza la wawakilishi na mwanzoni uliwekewa guu na wabunge waliohisi kwamba jambo hilo linakwenda kinyume na hisia za kibepari na ni mzigo kwa walipa kodi. Wabunge 228 wa Baraza la wawakilishi waliupinga na 205 kuupendelea, hivyo kuuingiza si tu uchumi wa Marekani katika hali ya wasiwasi, lakini wa dunia nzima.

Rais George Bush, akivunjika moyo, alisema hivi:

"Bahati mbaya hatua hiyo imeshindwa kwa kura chache. Nimevunjika moyo na matokeo hayo. Lakini na hakika raia wetu na raia duniani kote kwamba huu sio mwisho wa mwenendo huu wa kuijadili bungeni. Kuwa na sheria ni zoezi gumu na linaweza kuwa na mabishano. Sio muhimu njia gani mswada huo unapitia kuwa sheria. Cha muhimu ni kwamba tunakuwa na sheria. Tuko katika hali ngumu katika uchumi wetu na tunahitaji sheria ambayo itakabiliana vilivyo na akiba ambazo zina shida na ambazo zinaukwamisha mfumo wetu wa fedha. Tunahitaji kuwawezesha wakopeshaji waanze kutoa mikopo kwa wateja na wafanya biashara na kuuruhusu uchumi wa Marekani uanze kusonga mbele tena."

Wiki moja baadae, serekali ya Rais Bush ilifanya jaribio lengine kuuleta tena mbele ya bunge mpango huo uliofanyiwa marekebisho kwa kuwapa nafuu zaidi ya kodi wafanya biashara wa kati na kati. Mara hii uliungwa mkono kwa kura 268 zilizouunga mkono na 171 zilipinga. Sio tu Marekani lakini dunia nzima ilipumua kutokana na ujiingizaji huo wa kiuchumi, ulio mkubwa kabisa kutoka upande wa serekali ya Marekani tangu miaka ya thalathini. Mtetezi wa urais wa Chama cha Republican, John McCain, aliuita mpango huo wa uokozi kuwa ni hasara ya lazima na akala kiapo kwamba atayasafisha masoko ya hisa ya Wall Street huko New York pindi atachaguliwa. Baraza la Senate nalo hapo kabla liliupitisha mpango huo kwa kura 74, huku kura 25 zikiupinga. Mpango huo unaipa mamlaka wizara ya fedha ya Marekani kuinunua mikopo isiokuwa ya faida ambayo imekuwa ikizuwia sekta ya fedha isiweze kufanya kazi.

Rais Bush, akipumua kidogo, baada ya kuitia saini sheria inayohusiana na mpango huo wa kuuokoa uchumi, alisema:

"Kiliomo ndani ya mpango huu wa uokozi ni kuwachia mikop itolewe, kuzifanya fedha zitembee. Na itachukuwa muda. Nimeutia saini mswaada huo na kuwa sheria wiki iliopita, lakini itachukuwa muda kuweza kufanya kazi vizuri. Hilo moja. La pili mpango huo haupotezi fedha za walipa kodi, hatutaki kuharakisha mambo na kuufanya mpango huo usiweze kufanya kazi vizuri. Itachukuwa muda kurejesha imani katika mfumo wa fedha. Lakini jambo moja watu wanaweza kuwa na hakika nalo ni kwamba mswada nilioutia saini ni hatua kubwa ya kuutanzua mzozo huu."

Na japokuwa imani ya wananchi kwa mfumo wa uchumi na wa fedha wa Marekani ilianza kurejea, hata hivyo, somo hilo lilionekana wazi linatokana na jambo la kusikitisha la uongozi mbovu. Kuwasilisha siasa ilio na utata, tena ilio ya gharama kubwa ambayo huenda sana isipendelewe na wapiga kura, tena wiki chache kabla ya kufanyika uchaguzi, siasa inayohitaji pia iungwe mkono na upande wa upinzani, kulihitaji moyo, jambo ambalo linakosekana katika serekali ya Rais Bush. Rais huyo, ambaye pia amepoteza heba hata ndani ya chama chake mwenyewe cha Republican, alimwachia waziri wa fedha, Henry Paulson, aongoze kuutetea mpanga huo.

Kama alivosema mwenyewe George Bush, mpango wake huo sio dawa, kwani kwa vyovyote Marekani inaelekea katika hali ya uchumi wake kukwama. Wachunguzi wanasema kutia dola bilioni 700 katika mishipa ya mfumo wa fedha wa nchi hioyo sio suluhisho. Mabenki yameacha kukopeshana fedha na pia kwa wateja wao, zikihofia kwamba rasil mali zao ziko hatarini, jambo lililosababisha mzozo huu hata serekakli ikajiingiza kudhamini mikopo mibaya. Japokuwa waziri wa fedha wa Marekani, Henry Paulson, aliahidi kwamba sasa atasonga mbele kwa haraka kuutekeleza mpango huo na viongozi bungeni walikula kiapo kwamba watahakikisha fedha za walipa kodi zinatumiwa vizuri, bado kuna ati ati.

Mzizi wa fitina ni tatizo lilokuweko katika soko la mikopo ya kununua majumba. Ili kurejesha imani na kuwachia mikopo itolewa, wenye majumba watahitaji msaada zaidi ili waandaliwe utaratibu mpya wa kugharamia mikopo yao ili kuzuwia mawimbi ya watu nyumba zao kupigwa tanji. Pia bunge la Marekani lichunguze nani wa kulaumiwa kutokana na mzozo huu na kipi kilichokwenda kombo ili kwamba kisikaririwe.

Mzozo huu wa kifedha sio tu umebadilisha uso wa uchumi wa Marekani, lakini umegeuza wizani katika mchuano wa uchaguzi wa urais katika nchi hiyo. Mtetezi wa chama cha Democratic, Barack Obama, anazaidi kuungwa mkono zaidi kumshinda mpinzani wake wa Chama cha Republican, John McCain, huku wapiga kura wakionekana wanamuamini zaidi Obama kwamba anaweza kuuongoza uchumi kwa njia ilio bora zaidi.

Naam. Dola bilioni 700 zitatumiwa na serekali huko Marekani kuinunua mikopo ya benki ambayo thamani yake hamna mtu anayeijuwa na ambayo sehemu kubwa ya mikopo hiyo haina thamani. Makosa yamefanywa na wale wenye uroho katika masoko ya hisa na mameneja wa mabenki, na cha ajabu ni kwamba hawataadhibiwa, lakini watazawadiwa. Mara hii watazawadiwa na dola itakayonunua hasara iliosababishwa na mabenki kama lile la Lehmann utaratibu mpya katika uchumi, mfumo wa ujamaa kwa matajiri. Faida za mabenki huwa za binafsi kwa mabenki hayo, lakini mabenki hayo yanapopata hasara. ni serekali ndio inayobebeshwa mzigo, na mwishowe ni mlipaji kodi anayeumia.

Lakini Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, nchi ambayo ni injini ya uchumiwa Ulaya alisema hivi:

"Ujerumani maisha itataka ichukuliwe hatua ya nchi mbali mbali kushirikiana kwa pamoja. Na kuna sehemu mbili katika mzozo huu wa fedha na namna ya kuusimamia hivi sasa. Usimamizi lazima uweko , jambo ambalo kwa upande momoja litaleta usalama na sio kuzidisha hali isiokuwa ya usalama. Lakini kwa upande mwengine, sio kuyaachia mabenki yawe huru kabisa na pia sio kuyaachia yawe chini ya usimamizi kamili wa dola."

Na la ajabu ni kwamba yule mzima moto katika mpango huu wa kuuokoa mfumo wa fedha wa Marekani, waziri wa fedha Henry Paulson, aliwahi kuwa mkuu wa benki ya Goldman Sachs, moja ya mabenki ya kutoa mikopo ilofanikiwa sana. Sasa, kama waziri wa fedha , anajaribu kuuokoa ubepari wa kifedha wa Marekani. Jambo moja ni wazi kwamba bila ya mpango huo wa dola bilioni 700, basi mfumo wa fedha duniani ungeporomoka, mfano wa mkasa uliotokea mwaka 1929.
 • Tarehe 07.10.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FVYW
 • Tarehe 07.10.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FVYW
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com