Jitihada za kujumuisha tamaduni tofauti hazikufanikiwa Ujerumani
17 Oktoba 2010Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema kuwa jitahada za kujenga jamii ya tamaduni tofauti nchini humo zimeshindwa vibaya. Merkel alitamka hayo alipokuwa akihutubia chama cha vijana wa chama chake cha kihafidhina CDU.
Kansela Merkel ametamka hayo baada ya mwanasiasa mwenzake wa kihafidhina Horst Seehofer, siku ya Ijumaa kusema kuwa Ujerumani sio nchi ya wahamiaji na kwamba kukosekana kwa wafanyakazi wenye ujuzi kusionekane kama kuwepo uhuru wa kile alichokiita "uhamiaji usiodhibitiwa."
Wakati huo huo, mwanasiasa wa chama cha Kijani, Jürgen Trittin ameliambia gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag kuwa Seehofer anachochea misimamo mikali kwa matamshi yake hayo. Trittin ameliambia gazeti hilo kuwa wafanyakazi wenye ujuzi wapaswa kutiwa moyo kuja Ujerumani na irahisishwe kwa watu hao kuja Ujerumani na kufanya kazi.