Je, Museveni ni rais wa maisha wa Uganda? | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Je, Museveni ni rais wa maisha wa Uganda?

Leo Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameapishwa tena kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula wa nne mfululizo, huku kukiwepo na maandamano ambayo Museveni amejaribu kuyakandamiza kwa nguvu wiki zilizopita.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

"Nitabakia rais milele." Hiyo ilikuwa kauli mbiu ya Museveni katika kampeni yake ya uchaguzi. Hata madikteta wengine katika nchi za Afrika Kaskazini walitamka hivyo na wakajirundikia mali ya serikali kwa miongo kadhaa. Hatimae wakatimuliwa madarakani.

Rais wa Uganda Museveni anang'ang'ania madarakani kwa miaka 25 sasa. Kiongozi huyo anatuhumiwa na wengi kuwa ameshinda uchaguzi uliopita kwa sababu ya kutoa zawadi ya fedha kwa wapiga kura katika kampeni iliyogharimu fedha nyingi mno za serikali.

Museveni ni mmojawapo wa viongozi wa Kiafrika waliopigania haki za wananchi, lakini sasa nguvu na madaraka yanaonekana kumlevya na hivyo kuingia katika kundi la viongozi mafisadi kinyume na malengo yake ya hapo mwanzoni.

Tangu uchaguzi uliofanyika mwezi wa Februari, serikali inatumia mabavu na vitisho dhidi ya waandamanaji na wapinzani wanaoandamana kwa amani.

Polisi wa Uganda wakiwa mitaani kuzuia maandamano ya wapinzani

Polisi wa Uganda wakiwa mitaani kuzuia maandamano ya wapinzani

Vikosi vya polisi vinatuhumiwa na mashirika ya haki za binaadamu kutumia mabavu, ukatili na kuwakamata watu kinyume na sheria. Hata vyombo vya habari vinazidi kubanwa.

Je, nini kilichoikumba nchi iliyojulikana kama "Lulu ya Afrika"? Je, inaelekea wapi chini ya uongozi wa rais aliyechaguliwa tena? Kwa nini anang'ang'ania madaraka na kutumia mabavu kuyakandamiza maandamano ya amani yanayopinga kuongezeka kwa bei za vyakula?

Labda yeye kama viongozi wenzake katika Kaskazini mwa Afrika, hajui hali ya ukweli inayowakabili wananchi katika maisha yao ya kila siku. Hafahamu jinsi ilivyokuwa vigumu kwa familia nyingi za Uganda kupata mlo wa siku moja.

Wakati huo huo kuna uvumi kuwa kiongozi huyo anataka kujitajirisha kwa pato la mafuta yanayotegemewa kuchimbuliwa nchini Uganda.

Wataalamu wanatathmini kuwa akiba ya mafuta inafikia mapipa bilioni kadhaa. Tayari inaripotiwa kuwa watu wanahamishwa kwa nguvu kutoka maeneo yenye utajiri wa mafuta. Mafuta hayo yataweza kusaidia kuwatoa wananchi kutoka maisha yao ya dhiki, ikiwa wao pia wataruhusiwa kufaidika.

Kwani katika nchi zingine kama Nigeria na Chad, utajiri wa mafuta umedhihirika kuwa kama mkosi kwa wanaanchi na mazingira.

Ndoto ya Museveni ni kubakia rais kwa milele. Lakini hilo ni jinamizi kwa vijana wengi wa Uganda wasiomjua rais mwengine isipokuwa Museveni tangu walipozaliwa.

Mwandishi: Andrea Schmidt/ ZPR (DW-Kiswahili)
Tafsiri: Prema Martin
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com