1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yathibitisha mateka walioachiliwa na Hamas

Sylvia Mwehozi
21 Oktoba 2023

Israel imethibitisha kuwa Hamas imewaachia huru mateka wawili iliokuwa inawashikilia raia wa Kimarekai, na tayari wamekabidhiwa kwa jeshi la Israel kwenye mpaka na Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4Xq4c
Mateka wa Kimarekani walioachiwa na Hamas
Judith Tai Raanan na Natalie Shoshana Raanan walioachiliwa na HamasPicha: Government of Israel via REUTERS

Kundi la wanamgambo la Hamas limetangaza kuwaachia huru Wamarekani wawili ambao ni miongoni mwa mateka inaowashikilia, ikitaja "sababu za kibinadamu" pamoja na kutuma ujumbe kwa rais Joe Biden ambaye kwa ameunga mkono kwa dhati Israel katika vita vyake dhidi ya kundi hilo.

Msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas Abu Ubaida ametoa taarifa ya kuachiwa kwa mateka wawili, ikiwa ni mara ya kwanza tangu wanamgambo wa kundi hilo walipoishambilia Israel Oktoba 7 na kuwaua watu 1,400 wengi wao wakiwa ni raia na kuwachukua watu wengine karibu 200 kama mateka. Kwenye taarifa yake hiyo Abu Ubaida amesema mateka hao wameachiwa huru kutokana na juhudi za upatanishi za Qatar.

Judith na Natalie Raanan
Wamarekani walioachiliwa na kundi la Hamas Judith Tai Raanan na Natalie Shoshana RaananPicha: Raanan family/AP Photo/picture alliance

Hamas yawachukua mateka mamia ya watu: Ni lipi kusudio la Hamas kuwachukua mateka raia wa Israel?

Ofisi ya waziri mkuu wa Israel imethibitisha taarifa za kuachiliwa mateka hao wawili jana usiku. Afisa wa Israel ambaye anashughulikia masuala ya mateka na watu waliopotea Brigedia Jenerali Gal Hirsch, amewapokea mateka hao katika mpaka wa Ukanda wa Gaza huku taarifa zaidi zikisema kwamba wanawake hao wawili walikuwa njiani kuelekea katika kambi ya kijeshi kuungana na familia zao. Daniel Hagari ni msemaji wa jeshi la Israel IDF na ameeleza kwamba, "Judith Tai Raanan na Natalie Shoshana Raanan, mama na binti, wameachiliwa kutoka kwa kundi la kigaidi la Hamas jioni hii, na sasa wako mikononi mwa askari wa IDF na vikosi vya usalama katika eneo la taifa la Israeli."

Hapo awali, jeshi la Israel lilisema kwamba watu wengi wanaoshikiliwa mateka bado wako hai.

Hayo yakiarifiwa, Israel imeyaonya makundi ya misaada ya kiutu yaliyoko Ukanda wa Gaza kuwaondoa watu katika hospitali kubwa na shule tano kutokana na kuwepo uwezekano wa shambulio kubwa. Hospitali ya Al-Quds iliyoko kaskazini mwa Gaza, imekabiliwa na mashambulizi makali ya anga ya Israeli tangu Hamas ilipofanya mashambulizi yao makubwa zaidi kuwahi kutokea dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7.

Waliouawa Gaza: Waliouawa kwa mashambulizi ya Israel wafikia 3,785 Gaza

Guterres atembelea Rafah
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika kivuko cha RafahPicha: picture alliance/dpa

Shirika la Hilal Nyekundu la Palestina limetoa "wito wa dharura" likisema kwamba limepokea kitisho kutoka mamlaka za Israel za uwezekano wa hospitali ya Al-Quds kushambuliwa. Shirika hilo limeongeza kwamba onyo la Israeli "lilitaka" watu kuondolewa kwenye hospitali hiyo, hatua ambayo ingeathiri zaidi ya wagonjwa 400 na watu elfu 12,000 waliokimbia makazi na kutafuta hifadhi.

Aidha shirika hilo limetoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za mara moja kuzuia mauaji mengine kama yaliyotokea kwenye hospitali ya Al-Ahli Baptist. Shambulio la roketi kwenye hospitali hiyo liliwaua mamia ya watu huku Hamas na Israel zikitupiana lawama kuhusu shambulizi hilo.

Wakati huo huo kazi ya ukarabati wa barabara imeendelea jana katika mpaka wa Rafah unaoungaisha Misri na Ukanda wa Gaza ambao umeharibiwa katika mashambulizi ya anga. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitembelea kivuko hicho na kuomba usambazaji wa haraka wa misaada ya kiutu kuingia Gaza.Viongozi mbalimbali duniani akiwemo Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas, watahudhuria mkutano wa kilele wa kusaka amani katika mzozo wa Mashariki ya Kati unaofanyika mjini Cairo leo Jumamosi.