Israel yakanusha kuhusika na mauaji ya kiongozi wa Hamas | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Israel yakanusha kuhusika na mauaji ya kiongozi wa Hamas

Kauli ya kukanusha kuhusika huko imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman.

default

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman amekanusha taarifa kuwa shirika la upelelezi la Israel la Mossad lilihusika katika mauaji ya kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Mahmoud al-Mahbouh. Avigdor amesema kuhusishwa kwa Waisraeli waliozaliwa nje ya nchi yao katika mauaji hayo haidhihirishi kwamba Mossad ndiyo ilitekeleza mauaji hayo.

Akizungumza leo kwa mara ya kwanza kujibu tuhuma hizo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman, alisema siyo jambo sahihi kuhisi kuwa Israel inahusika na mauaji ya Mahmoud al-Mahbouh yaliyofanyika mwezi uliopita katika hoteli moja huko Dubai. Amesema hakuna haja ya kudhania kwamba Mossad ndiyo ilihusika na mauaji hayo na sio shirika lingine la kijasusi au nchi nyingine. Akizungumza katika Radio ya Jeshi la Israel, waziri Lieberman amesema hajui ni kwa nini Israel inahusishwa na mauaji hayo, ilhali pasi za kusafiria zilizotumiwa na wahalifu hao zilikuwa ni bandia.

Polisi katika Umoja wa Falme za Kiarabu imewataja watu 11 walioingia Dubai wakiwa na uraia wa nchi za Ulaya kama watuhumiwa wa mauaji hayo. Miongoni mwao wakiwemo raia watatau wa Ireland na sita wakiwa ni raia wa Uingereza waliohamia Israel. Pia yumo mwanamke mmoja na mwingine alikuwa na pasi ya kusafiria ya Ujerumani na mwingine ya Ufaransa. Lakini serikali za mataifa hayo zimesema hazikutoa pasi za kusafiria zenye udanganyifu. Wanaume wawili raia wa Uingereza ambao wamekuwa wakiishi Israel kwa miaka kadhaa wameripotiwa kushtushwa na utumiwaji wa majina yao.

Wasemavyo wachambuzi

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya upelelezi nchini Israel wamesema kuwa shirika la Mossad litakuwa limevurunda kama kweli linahusika na mauaji hayo na kufanya ushiriki wake kuwa wa siri kwa kuwatumia watu ambao wanaweza wakatafutwa na kupatikana nchini Israel. Kundi la Hamas la Palestina limeishutumu Israel kwa kuhusika na mauaji hayo na polisi wa Dubai wamesema hawawezi kuthibitisha ushiriki wa Israel katika mauaji hayo. Mkuu wa polisi wa Dubai, Luteni Kanali Dhafi Khalfani Tamim amesema majina ya watuhumiwa hao yamepelekwa kwa polisi wa kimataifa-Interpol, ili hati ya kimataifa ya kukamatwa kwao iweze kutolewa. Chanzo cha habari cha serikali kimeeleza kuwa watu wengine sita ambao bado hawajatambuliwa wanadaiwa kuhusika katika mauaji hayo.

Al-Mahbouh, mwenye umri wa miaka 50 ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa tawi la kijeshi la Hamas la al-Qassam Brigades, alikutwa amekufa katika chumba chake hotelini Januari 20, mwaka huu siku moja baada ya kuwasili Dubai. Chanzo cha habari cha usalama nchini Israel kimeeleza kuwa Al-Mahbouh alikuwa akishutumiwa kuhusika na uuzaji kimagendo silaha zilizofadhiliwa na Iran kwenda kwenye eneo la wanamgambo wa Kiislamu katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 17.02.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M438
 • Tarehe 17.02.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M438
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com