Iran na Mpango wake wa nyuklia | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 09.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Iran na Mpango wake wa nyuklia

Shirika la atomiki la Umoja wa mataifa, IAEA limechapisha ripoti inayosema kuwa Iran inafanya kazi kutengeneza silaha za nyuklia

default

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, akitembelea mojawapo ya vinu vya nyuklia nchini

Shirika la IAEA limesema lina ushahidi kuwa Iran inafanya utafiti kuhusu muundo wa silaha za nyuklia, ukaguzi ambao ni wenye ufafanuzi wa ndani uliyotolewa mpaka sasa, na ambao Iran imeukanusha kuwa tuhuma za uongo na zisizokuwa na msingi.

Internationale Atombehörde IAEA

Makao makuu ya shirika la atomiki la Umoja wa mataifa, mjini Vienna Austria

Shirika hilo la atomiki limesema katika ripoti yake kuwa lina wasiwasi mkubwa unaotokana na taarifa za kuaminika zinazoashiria kuwa nchi hiyo ya kiislamu imetekeleza shughuli zinazoambatana na kuunda silaha ya nyuklia.

Kwa kutumia taarifa kutoka vyanzo 10 vya mashirika ya upelelezi ya nchi za nje pamoja na taarifa zake, IAEA imeorodhesha yaliomo kwenye mpango huo wa Iran katika maeneo 12 ambayo yanagusia kila sehemu inayohitajika katika utengenezaji silaha.

Shirika hilo ambalo bodi yake huenda ikaamua kuishtaki Iran kwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa wiki ijayo, imetoa wito kwa Iran kushirikiana nalo bila ya kuchelewa ili kutoa maelezo zaidi.

Kufuatia kutolewa ripoti hiyo, Marekani imesema kuwa ripoti hiyo imeonyesha kuwa Iran ilidanganya na imesema itatafuta kushinikiza mbinyo na pengine vikwazo vipya, lakini wachambuzi wanasema ripoti hiyo haitoshi kupata uungwaji mkono wa kutoka China na Urusi.

Kwa upande wake Urusi, imeshutumu uchapishaji wa ripoti hiyo ikisema itadidimiza matumaini ya majadiliano na Tehran, na huedna ikasitisha kufikiwa suluhu ya kidiplomasia.

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema ripoti hiyo imekuwa chanzo cha kuongezeka upya wasiwasi kuhusu mpango wa Iran, hata pia kabla ya kuchapishwa kwake.

Urusi ambayo ni mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa, na iliyo na kura ya turufu, inajaribu kuzuia kuharibu uhusiano wake na Iran na wakati huo huo inajaribu kuonyesha umuhimu wake kwa mataifa ya magharibi katika diplomasia, inaitisha mpango wa hatua baada ya hatua, ambapo vikwazo vilivyopo dhidi ya Iran vitapunguzwa ili Iran kwa upande wake ithibitishe kuwa mpango wake huo wa nyuklia, ni wa amani kama inavyodai.

Miongoni mwa wengine waliotoa hisia zao kuhusu kuchapishwa ripoti hiyo, alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle aliyesema kuwa iwapo suala hilo litazidi kuwa kubwa, na Iran itasemekana kuendeleza mpango wake, basi Ulaya itaidhinisha awamu nyengine ya vikwazo.

Außenminister Westerwelle vor EU-Gipfel in Brüssel

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle


Ripoti hiyo imetolewa baada ya fununu za vyombo vya habari vya Israeli zilizoeleza kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulio dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran, jambo ambalo Urusi imelipinga mara kwa mara.

Israel kwa upande wake haikutoa tamko la mara moja baada ya kutolewa ripoti hiyo, huku msemaji wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu akieleza kuwa huenda ikafanya hivyo baada ya kuyapitia yaliomo ndani ya ripoti hiyo.

Hapo awali rais wa Israel, Shimon Peres, alionya kuwa shambulio dhidi ya Iran huenda linakaribia kutekelezwa, badala ya kutumia njia za kidiplomasia.

Mwandishi Maryam Abdalla/Afpe/Rtre/Dpae
Mhariri: Mohammed Khelef

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com