Hatua za kufunga mikaja nchini Ujerumani | Magazetini | DW | 22.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Hatua za kufunga mikaja nchini Ujerumani

Mbinu za uchaguzi kutuliza nyoyo za wapiga kura kabla ya hatua za kufunga mikaja

default

Waziri wa fedha Wolfgang Schäuble akizungumza na waandishi habari

Mipango ya serikali kuu ya kupunguza nakisi ya bajeti na kifo cha mkosoaji mkubwa wa utawala wa Mamullah nchini Iran ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini Berlin ambako serikali kuu inajiandaa kupunguza matumizi. Gazeti la "MÜNCHNER MERKUR linaandika

Mnaona! Hata muda haujapita baada ya serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na FDP hapa Ujerumani kupitisha sheria za kupunguza kodi za mapato bungeni,waziri wa fedha, Wolfgang Schäuble, anatangaza azma ya kupunguza mabilioni ya Euro.Kitita cha Euro bilioni kumi anapanga kukusanya baada ya uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westfalia.Mtu anaweza kusema: kwa mtazamo wa sera za kodi ,mpango huo si sawa na kwa mtazamo wa sera za ukuaji ndio vivyo hivyo. Ni kwa mtazamo wa mbinu za uchaguzi tuu ndipo mtu anapoweza kusema mpango huo unaingia akilini. Merkel anataka kuhakikisha uchaguzi unapita vizuri kwa chama chake katika jimbo la North Rhine westfalia.Unaweza kuuita hadaa za uchaguzi-lakini nchini Ujerumani hakuna serikali yoyopte iliyoingia madarakani kwa kutoa ahadi za kufunga mikaja na kutia njiani mageuzi.

Maoni sawa na hayo yametolewa pia na mhariri wa gazeti la "Westfalen-Blatt" la mjini Bielefeld anaeandika:

Waziri wa fedha, Wolfgang Schäuble, anazungumzia juu ya mpango wa kupunguza matumizi-lakini hatoi maelezo zaidi. Anataka kuweka siri hadi July mwakani au angalao baada ya May tisaa mwaka 2010.Katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westfalia,serikali ya muungano wa nyeusi na manjano inataka kupigania kuendelea kuwepo madarakani mjini Düsseldorf. Kwa hivyo wakisema ukweli unaweza kuwageukia wenyewe.Kilichosalia ni kuvuta wakati.Lakini mpaka lini? Kisheria, serikali kuu ya shirikisho ina muda wa hadi mwaka 2011 kuitia njiani hatua kali za kupunguza nakisi ya bajeti. Na ukweli, hata hivyo, ni kwamba propaganda inayopigiwa upatu na chama cha FDP za kutia njiani mfumo mwepesi ,wa haki, na nafuu wa kodi za mapato utagharimu fedha.Na hapo ndipo kizungumkuti cha serikali ya muungano wa nyeusi na manjano kilipo.

Iran Beerdigung von Hossein Ali Montaseri in Ghom

Mazishi ya Ayatollah Hossein Ali Montasseri huko Ghom

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameishughulikia pia hali nchini Iran kufuatia kifo na mazishi ya Ayatollah mkuu-Montaseri.Gazeti la LANDESZEITUNG linaandika:

Maziko ya Montazeri ni hatua ya mwanzo kuelekea mwisho wa enzi za utawala wa Teheran. Kwa sababu umati wa watu walioandamana wakati wa maziko ya Ayatollah Mkuu umedhihirisha kwamba vuguvugu la upande wa upinzani nchini Iran halijadhoofika, kinyume na vichwa mchungu wanaomuunga mkono rais Ahmadinedjad wanavyotarajia. Kinyume kabisa, moyo wao wa kijasiri umezidi kupata nguvu na madai yao yanazidi kuwa makali. Kifo cha mkosoaji wa utawala wa Teheran-Montaseri-kiongozi mkuu wa kidini nchini humo, ingawa kinaufanya upande wa upinzani upwaye kidogo, lakini nguvu zao hazikutetereka. Kwa jinsi gani utawala wa Ahmadinedjad unahofia umma wake, hali hiyo imedhihrika kufuatia marufuku yaliyowekewa vyombo vya habari vya kigeni kuripoti kuhusu mazishi ya Montaseri.Hata Miito ya kutaka Chamenei aiage dunia haijakosekana.Kwamba kiongozi huyo wa mapinduzi ya kiislam, hatukuzwi tena, hali hiyo pekee inabainisha,upande wa upinzani umepania kuyazika mapinduzi ya kiislam.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Inlandspresse)

Mhariri:Othman Miraji

 • Tarehe 22.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LAbY
 • Tarehe 22.12.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LAbY
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com