Hatima ya wafungwa wa CIA haijulikani | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hatima ya wafungwa wa CIA haijulikani

Serikali ya Marekani inapaswa kuwajibika na wafungwa wote wasiojulikana walipo ambao walikuwa wakishikiliwa mahabusu na Shirika la Ujasusi la Marekani CIA katika magereza ya siri duniani kote.

Khaled al Masri raia wa Ujerumani wa nasaba ya Lebanone ni mmojawapo wa watuhumiwa wa ugaidi aliewahi kushikiliwa na kudai kuteswa katika magereza ya CIA yalioko nchi za nje.

Khaled al Masri raia wa Ujerumani wa nasaba ya Lebanone ni mmojawapo wa watuhumiwa wa ugaidi aliewahi kushikiliwa na kudai kuteswa katika magereza ya CIA yalioko nchi za nje.

Repoti ya Human Right Watch shirika la haki za binaadamu lenye makao yake mjini New York Marekani inaeleza kwamba hatima ya wafungwa hao wengi waliotoweka bado haijulikani.

Repoti hiyo iliopewa jina Mfungwa Asiejulikana Alipo : Miaka Miwili katika Mahabusu ya Siri ya Shirika la Ujasusi la Marekani CIA ina ufafanuzi wa kina kutoka kwa mahabusu wa Kipalestina juu ya uzoefu wake katika gereza la siri la CIA kabla ya kuachiliwa kwake hapo mwaka jana.

Hapo tarehe 6 mwezi wa Septemba mwaka 2006 Rais George W. Bush wa Marekani amesema kwamba wafungwa wote wa CIA aidha wameachiliwa au kupelekwa kwenye kambi ya Guantanamo nchini Cuba lakini shirika la Human Right Watch linadai kwamba wafungwa wengine wengi wamefanywa waendelee kutoweka na CIA.

Joanne Mariner mkurugenzi wa ugaidi na vita dhidi ya ugaidi wa shirika hilo la kutetea haki za binaadamu amesema katika taarifa suala ni nini kimewatokea watu hao na hivi sasa wako wapi?

Imeoredhesha kundi la watu 16 na wengine 22 ambao hadi hivi sasa hawajulikani walipo.

Marwan Jabour mahabusu wa zamani wa CIA anasema kwamba wengi wa wafungwa hao waliotoweka bado wako kwenye magereza ya CIA na kwamba yeye mwenyewe binafsi alimuona mmojawao mtuhumiwa wa ugaidi wa Algeria Yassir al Jazeeri hapo mwezi wa Julai mwaka 2006 akiwa anashikliliwa na CIA.

Mahala walipo wafungwa hao wasiojulikana walipo hakujulikani lakini uwezekano mmoja ni kwamba wamehamishwa kutoka magereza ya siri ya CIA yanayovuma kuwa yako nchini Thailand,Afghanistan,Jordan,Pakistan,Morocco,Jamhuri ya Czeck, Ujerumani,Hungary,Poland,Romania, Armenia,Georgia,Latvia na Bulgaria hadi kwenye magereza yao yalioko katika nchi za kigeni ambayo yako chini ya udhibiti wa CIA na yumkini wakawa wanateswa na Marekani au na wasaili wa nchi enyeji.

Marwan Jabour alikamatwa nchini Pakistan hapo mwaka 2004 na baada ya kushikiliwa kwa takriban mwezi mmoja alihamishiwa kwenye gereza la siri linaloaminika kuwepo nchini Afghanistan ambapo wafanyakazi wake wote walikuwa ni raia wa Marekani.

Alipowasili kwenye gereza hilo aliwekwa uchi wa nyama kwa mwezi mmoja na nusu na alihojiwa na wasaili wa kike pamoja na kuchukuliwa filamu.Alifungwa mnyonyoro kwenye ukuta wa chumba chake ili kwamba asiweze kusimama na kufanya iwe vigumu kwake kupumuwa na kuelezwa kwamba iwapo hatotowa ushirikiano wake atatiwa kwenye kibanda cha mbwa ambapo atashindwa kupumuwa kabisa.(Mfungwa huyo ameliambia shirika hilo la haki za binaadamu kwamba hali ililuwa mbaya sana na aliuona huo kama vile ni mwisho wa maisha yake.)

Repoti ya Human Right Watch inatowa wito sio tu wa kuweka nadhari kwa kuvurugikiwa akili kwa wafungwa kutokana na uzoefu wao huo bali pia kuangalia shida na kuchangayikiwa kwa familia za wafungwa ambao waume zao,baba zao na watoto wao wametoweka.

Shirika hilo linataka Marekani kujitenganisha na matumizi ya magereza ya siri na usaili wa kushurutisha kama mbinu za kupambana na ugaidi na kuachana moja kwa moja na mipango ya mahabusu na usaili ya CIA pamoja na kutangaza majina,hatima na mahala walipo wafungwa wote wale waliokuwa wakishikiliwa huko nyuma na vituo vilivyokuwa vikiendeshwa au kudhibitiwa na CIA tokea mwaka 2001.

Kutolewa kwa repoti hiyo kumeandamana na baruwa kwa Rais George W. Bush ikielezea wasi wasi wa shirika hilo juu ya matumizi ya magereza ya siri kushikilia watu wanaotuhumiwa kuhusika katika ugaidi.

 • Tarehe 02.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJ6
 • Tarehe 02.03.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJ6

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com