HARARE : Balozi wa Marekani ashutumiwa kujaribu kuzusha mfarakano wa kidiplomasia
14 Oktoba 2005Zimbabwe imemshutumu balozi wa Marekani nchini humo Christopher Dell kwa kujaribu kwa makusudi kuzusha mzozo wa kidiplomasia baada ya kuingia kwenye eneo lililopigwa marufuku karibu na makao makuu rasmi ya Rais Robert Mugabe mapema wiki hii.
Dell alishikiliwa kwa mtutu wa bunduki kwa kama nusu saa hapo Jumaatatu na walinzi wa Rais.Gazeti linalomilikiwa na serikali la The Herald limekariri duru za serikali leo zikisema kwamba kioja hicho ni sehemu ya mpango wa Marekani kuchochea mabadiliko ya utawala nchini Zimbabwe.Wizara ya mambo ya nje ya Zimbabwe imesema katika taarifa kwamba Dell alikusudia kuchochea mzozo wa kidiplomasia usiohitajika.
Msemaji wa rais George Charamba amesema balozi huyo anapaswa ajione kuwa ana bahati kuwa hai kwa sababu angeliweza kupigwa risasi na kuuwawa.
Hadi sasa ubalozi wa Marekani nchini humo umekataa kuzungumzia tukio hilo.