EU yataka kupiga vita mabadiliko ya hali ya hewa | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

EU yataka kupiga vita mabadiliko ya hali ya hewa

Umoja wa Ulaya unataka kuwa mfano mzuri katika juhudi za mapambano dhidi ya mabadiliiko ya hali ya hewa. Hilo ndilo lengo lake Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambaye kwa miezi hii sita ni mwenyekiti wa Umoja huu.

Upepo ni njia moja ya kutengeneza nishati endelevu

Upepo ni njia moja ya kutengeneza nishati endelevu

Kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi 25 wanachama wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika kesho na keshokutwa, Merkel anaungwa mkono na mkurugenzi wa halmashauri kuu ya Umoja huu, José Barroso ambaye pia analipa kipaumbele suala la ulinzi wa hali ya hewa.

Kwa wiki kadhaa sasa, rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, José Barroso, anafanya bidii kubwa kuiendeleza sera ya Umoja huu kuhusu ulinzi wa hali ya hewa. Mkakati mpya ni kuundwa kamati maalum ya wanasayansi wanaotarajiwa kuushauri Umoja wa Ulaya katika suala hilo. Wajumbe katika kamati hiyo ni wanasayansi 11 kutoka nchi mbali mbali ambao ni wataalamu katika masuala ya hali ya hewa na nishati. Mmojawao ni Nicolas Stern, mtoaji ushauri wa serikali ya Uingereza ambaye amepata umaarufu kwa kuchapisha ripoti juu ya maafa na matokeo mengine mabaya yanayoweza kutokea kutokana na kubadilika kwa hali ya hewa.

Mwanasayansi mwingine katika kamati hiyo ni Joachim Schellnhuber wa Ujerumani. Kwa miaka mingi, Bw. Schellnhuber aliwataka wanasiasa kuweka sera za ulinzi dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa: “Tumepoteza miaka kumi katika kujadiliana ikiwa mabadiliko ya hali ya hewa kweli yako na iwapo ni kosa la binadamu. Sasa inabidi tuchukue hatua haraka!”

Kulingana na mwanasayansi Joachim Schellnhuber, mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wiki hii unaweza kuleta maamuzi muhimu sana. Alisema: “La muhimu ni kuweka masharti ya kulazimika kuhusiana na matumizi ya nishati endelevu. Kuna mjadala mzito sasa hivi na ninatumaini Ulaya itafikia matokeo muhimu.”

Kuweka masharti kamili pia ni lengo la José Barroso na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Katika mahojiana aliyofanyiwa na gazeti la “Financial Times”, Angela Merkel alisema ilikwishakubaliwa kupunguza utoaji wa gesi ya Carbon Dioxid kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020. Vile vile, lengo la kuongeza matumizi ya nishati endelevu hadi asilimia 20 ya nishati yote inayotumika ni lengo linalokubaliwa na wengi. Kansela huyu alisisitiza kuwa ni hatua ya kihistoria kwa vile ni mkakati wa kwanza kuhusiana na nishati wa Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Bi Merkel anataka kushawishi nchi kama Ufaransa ambazo zina mashaka juu ya mkakati huo kwa kuahidi kugawana mzigo huu.

Kwa kuimarisha mkakati wa pamoja wa Umoja wa Ulaya, Angela Merkel anataka kusukuma mazungumzo juu ya mkakati wa kimataifa wa kulinda hali ya hewa. Kabla ya mkutano wa nchi zilizostawi zaidi kiviwanda duniani, G8, utakaofanyika baadaye mwaka huu nchini Ujerumani, Kansela Merkel, ambaye mwaka huu si tu mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya bali pia wa G8, anataka kuweka ishara kwa viongozi wa nchi hizo.

 • Tarehe 07.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHIm
 • Tarehe 07.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHIm

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com