El – Fasher, Sudan. Marekani yailaumu Sudan kwa kushindwa kusitisha mauaji katika jimbo la Dafur.
22 Julai 2005Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameilaumu serikali ya Sudan jana kwa kushindwa kusitisha mauaji katika jimbo lililokumbwa na machafuko la Dafur lakini ameashiria uwezekano wa kupunguza vikwazo vya Marekani kwa misingi ya kibinadamu.
Katika ziara yake ya kwanza katika nchi hiyo ya Afrika , Rice amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Sudan , alidai na kupata kuombwa msamaha kutokana na kutokuelewana kati ya wajumbe wa msafara wake na viongozi wa masuala ya kiusalama wa Sudan, pamoja na kulitembelea jimbo la Dafur.
Maafisa wa Marekani wamesema Rice amesema wazi kuwa Marekani haiwezi kuimarisha uhusiano na Sudan kabla ya kupata ufumbuzi wa mzozo wa Dafur, ambapo watu 300,000 wameuwawa katika mapigano yaliyoanza miezi 29 iliyopita na kuelezwa na Marekani kuwa ni mauaji ya maangamizi.
Wakati huo huo raia mmoja wa Sudan ameachwa huru kutoka katika jela iliyoko katika kituo cha kijeshi cha Guantanamo Bay , Cuba , zimeeleza duru za serikali jana.
Duru katika wizara ya mambo ya kigeni zimesema Hammad Amnu Jadala alisafirishwa siku ya Jumatano hadi Khartoum na viongozi wa Marekani , na kuongeza kuwa viongozi wataongeza juhudi ili kuachiwa kwa raia wengine tisa wa Sudan.