Duisburg yaingia fainali ya kombe la Ujerumani | Michezo | DW | 02.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Duisburg yaingia fainali ya kombe la Ujerumani

MSV Duisburg jana usiku ilifanikiwa kuingia fainali ya kombe la Ujerumani -DFB-kwa mara ya kwanza tokea mwaka 1998 baada ya kuifunga Energie Cottbus mabao 2-1.Timu zote ziko daraja la pili.

default

Wachezaji wa MSV Duisburg wakishangilia ushindi dhidi ya Energie Cottbus na kuingia fainali ya kombe la Ujerumani.

Duisburg sasa inasuburi mshindi kati ya Bayern Munich na Schalke 04 zinazopambana hii leo katika nusufainali nyingine ya michuano hiyo.

Mabao ya Duisburg iliyokuwa nyumbani yaliwekwa wavuni na Stefan Maierhofer na Srdjan Baljak, huku lile la Cottbus likifungwa na Nils Petersen.

Kuweza kuingia nusufainali Duisburg iliziondoa timu za daraja la kwanza FC Cologne na Kaiserslautern.

Kocha wa Duisburg Milan Sasic ambaye aliingia Ujerumani mwaka 1991 akikimbia vita, na kufanyakazi za kawaida kwa muda wa miaka mitatu, alisema kuwa ushindi huo ni kama ndoto iliyokuwa kweli.

´´Baada ya kazi ya kuijenga timu, sikuwahi kufikiria, kitu kama hiki kinaweza kutokea, kamwe sitoweza kusahau wapi mwanzoni nilipokuwa.Tumemudu kuifanya ndoto yetu kuwa kweli na  kupiga hatua kubwa´´alisema kwa furaha

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Mohamed Abdulrahman