1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yakosoa mpango wa kodi ya kaboni ya Umoja wa Ulaya

Josephat Charo
26 Julai 2021

China imesema mpango wa Umoja wa Ulaya kuanzisha kodi ya kwanza ya viwango vya gesi ya kaboni duniani utageuza masuala ya mazingira kuwa ya kibiashara, kukiuka kanuni na kimataifa na kuathiri vibaya ukuaji wa uchumi.

https://p.dw.com/p/3y5VI
Brüssel | PK zur Erreichung der Klimaziele | Frans Timmermans und Ursula von der Leyen
Makamu wa rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Frans Timmermans (kushoto) na rais wa hamashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen wakati wakizindua mpango wa mpito kuelekea uchumi wa kijani, Julai 14, 2021 mjini Brussels.Picha: John Thys/AFP

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya mwezi huu inatarajiwa kuainisha mipango ya kuanzisha kodi ya dunia inayonuiwa kudhibiti utoaji wa gesi ya kaboni au hewa ukaa, kwa bidhaa zinazochafua mazingira kuanzia mwaka 2026, kuzilazimisha baadhi ya kampuni kuagiza bidhaa katika Umoja wa Ulaya, kulipa gharama za utoaji wa gesi ya kaboni maeneo ya mpakani kwa bidhaa zinazotoa kiwango kikubwa cha gesi hiyo kama chuma cha pua.

Liu Youbin, msemaji wa wizara ya ikolojia na mazingira amesema kodi ya CBAM ni hatua iliyochukuliwa bila mashauriano kulitanua suala la mabadiliko ya tabia nchi na kuigeuza kuwa la kibiashara. Linakiuka kanuni za shirika la biashara la kimataifa WTO na itaathiri kwa kiwango kikubwa uaminifu katika jamii ya kimataifa na kuvuruga kabisa matumaini ya ukuaji uchumi.

Liu amesisitiza msimamo wa China kwamba juhudi za kila nchi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinatakiwa zizingatie kiwango cha maendeleo ya uchumi na ameongeza kuwa ushuru kwa bidhaa zinazotoa gesi ya kaboni utaathiri sana utayari na uwezo wa mataifa kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabianchi.

Infografik Karte Import Export CO2 EN
Namna biashara inaathiri kiwango cha kaboni cha matifa.

Waziri wa zamani wa fedha wa Ufaransa, Edmond Alphandery, ambaye sasa ni mwenyekiti wa jopo kazi linaloshughulikia uwekaji wa bei za kaboni barani Ulaya amesema "katika miaka ijayo Umoja wa Ulaya itaweka kodi ya kaboni mipakani inayonuiwa kuweka uwiano katika ushindani na makampuni ya kigeni. China haitaathiriwa sana na kodi hii katika mipaka."

Katika andiko lao lililochochapishwa mwezi Mei mwaka huu watafiti katika kitivo cha Maendeleo ya Viwanda na Usimamizi wa Mazingira katika chuo kikuu cha Tsinghua wamesema kama nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa malighafi duniani kama vile chuma cha pua na sementi, China huenda ikaathiriwa zaidi na mpango wa utozaji ushuru mipakani.

Soma pia: Ulimwengu waadhimisha miaka mitano ya mkataba wa Paris

Hata hivyo watafiti hao walisema athari itapungua katika kipindi kirefu na hakukuwa na ushahidi wowote kwamba utozaji ushuru huo utatoa mchango wa muda mrefu kwa maendeleo ya China.

Guotai Junan Futures lilisema katika taarifa kwamba kodi ya mpakani yumkini ikaishawishi China kuweka bei za gesi ya kaboni katika mpango wake wa kitaifa wa utoaji wa gesi hiyo kwa kuambatana na bei za Umoja wa Ulaya.

Waziri wa zamani wa fedha wa Ufaransa, Edmond Alphandery, na mwenyekiti wa sasa wa jopo kazi linaloshughulikia uwekaji wa bei za kaboni barani Ulaya amesema China ina fursa kubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na mfumo wake wa mpango unaoratibiwa kitaifa.

"Ni nchi ambayo pengine ina vifaa bora kabisa vya kukabiliana na kipindi cha mpito cha nishati. Ongezeko la bei za gesi ya kaboni kwa kasi linaainishwa na hatua kakadhaa kamili linapokuja suala la sheria, miundombinu ya umma, na ufadhili wa uvumbuzi. Mengi yanayofanyiwa kazi yatasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa utoaji wa gesi ya kaboni," aliongeza kusema.

Brüssel | PK zur Erreichung der Klimaziele | Frans Timmermans und Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wakati akizindua mpango wa kusimamia mpito kuelekea utoaji mdogo wa gesi ya kaboni, Julai 14, 2021.Picha: John Thys/AFP/Getty Images

Katika mahojiano maalumu ya mtandaoni na kituo cha televisheni cha China Global, CGNT, Alphandery alisifu kuanza kufanya kazi kwa soko la kaboni la China, akisema uwekaji bei ya kaboni utakuwa chachu ya kipindi cha mpito cha kutafuta nishati mbadala China.

Alphandery aidha alisema uzinduzi wa mpango wa kitaifa wa soko la kaboni wa China Ijumaa iliyopita una umuhimu wa kihistoria katika kupunguza utoaji wa gesi ya kaboni huku ukishirikisha hatua nyingine.

Kwa mujibu wa Alphandery, Umoja wa Ulaya pia umefanya kila juhudi kuhimiza uzalishaji usiochafua mazingira na unaopunguza utoaji wa gesi chafu ya kaboni.

Umoja huo unapanga katika miaka ijayo kuendelea kuitumia kodi ya kaboni itakayotozwa mipakani kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya Umoja wa Ulaya kudhibiti usafirishaji unaofanywa na makampuni kuelekea katika nchi zinazotoa kiwango kidogo cha gesi ili kuepusha kile kinachoitwa "kuvuja kwa gesi ya kaboni".

Tangu mpango wa kitaifa wa China ulipozinduliwa mnamo Julai 16, umerikodi tani milioni 4.83 katika wastani wa bei ya yuan 51.7 ambazo ni sawa na euro 6.8 kwa kila tani moja. Hii ni sawa na wastani wa zaidi ya euro 50 katika soko la kaboni la Umoja wa Ulaya.

Chanzo: Reuters