1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaituhumu Marekani kwa kuchochea mzozo

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
14 Julai 2020

Wizara ya mambo ya nje ya China imelaani tamko la Marekani la hivi karibuni linalopinga umiliki wa China wa rasilimali zilizoko kwenye bahari ya kusini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3fIyr
Südchinesisches Meer Spratly-Inseln Subi Riff
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Marquez

Wizara ya mambo ya nje ya China imelaani tamko la Marekani la hivi karibuni linalopinga umiliki wa China wa rasilimali zilizoko kwenye bahari ya kusini mwa nchi hiyo. Msemaji wa wizara hiyo ameiita Marekani kuwa nchi inayosababisha matatizo na inayovuruga amani. 

Wizara ya mambo ya nje ya China imesema kuwa Marekani inapuuza ukweli na historia juu ya bahari ya China kusini na kwamba inakiuka wajibu wa serikali ya nchi hiyo juu ya himaya ya China kwenye bahari  hiyo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Liijian ameeeleza kuwa Marekani inachochea utata kwa makusudi juu ya himaya ya China kwenye bahari ya kusini mwa nchi yetu. Marekani inakiuka na kupotosha sheria ya kimataifa, pia inavuruga amani na utulivu wa kanda hii. Kitendo hicho siyo cha busara''.

Soma zaidi: China yaituhumu Marekani kuendesha mazoezi ya kijeshi

Bidhaa zenye thamani ya dola trilioni tatu zinasafirishwa kwenye bahari hiyo

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema China haijatoa maelezo yenye msingi wa kisheria juu ya madai yake ya kumiliki rasilimali za bahari hiyo ya kusini mwa China. Marekani imetoa tamko kuunga mkono uamuzi uliopitishwa miaka minne iliyopita, kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa lililobatilisha madai ya China juu ya umiliki wa bahari ya China Kusini.

China inadai kumiliki asilimia 90 ya bahari hiyo yenye utajiri mkubwa, hata hivyo nchi nyingine pia zinadai  haki juu ya sehemu ya bahari hiyo. Nchi hizo ni pamoja na Brunei, Malaysia, Ufilipino, Taiwan na Vietnam. Bidhaa za biashara zenye thamani ya dola trilioni tatu zinasafirishwa kupitia kwenye bahari hiyo kila mwaka. China imejenga vituo kwenye visiwa kadhaa vya habari hiyo na inadai kuwa malengo yake ni ya amani.

Konflikt Südchinesisches Meer | Küstenwachen-Schiffe Philippinen, Hintergrund China
Meli ya walinzi wa pwani ya Ufilipino (R) ikiipita mel ya China wakati wa zoezi la pamoja la uokozi kati ya Ufilipino na Marekani katika mwambao wa pwani ya Amerika, katika Bahari ya Kusini mwa China.Picha: Getty Images/AFP/T. Aljibe

China imeikosoa Marekani kwa kujaribu kuchochea uadui kati ya nchi za kusini mashariki mwa bara la Asia. Serikali kadhaa za nchi hizo zimeepuka kutoa kauli juu ya tamko la Marekani. Msemaji wa rais nchini Ufilipino ameeleza kuwa jambo la msingi ni kutafuta njia za kuweka utaratibu wa kuepusha mivutano.

Soma zaidi: Trump ataka kupatanisha Bahari ya Kusini ya China

Mchambuzi kutoka Indonesia amesema tamko la Marekani ni la kisiasa, lenye lengo la kufunika udhaifu wa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya ndani ya Marekani. Hata hivyo, Indonesia na Ufilipino zimeungana na waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo katika kuitaka China izingatie usuluhishi wa  kimataifa.

Vyanzo: (AP/DPA)