1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaituhumu Marekani kuendesha mazoezi ya kijeshi

Saleh Mwanamilongo
7 Julai 2020

China inaituhumu Marekani kuendesha mazoezi ya kijeshi kwenye Bahari ya China ya Kusini. Msemaji wa mambo ya nje wa China anasema kwamba vitendo hivyo vya Marekani vitazidi kuzorotesha hali ya kanda hilo. 

https://p.dw.com/p/3eu0T
Taiwan | USS Antietam im Südchinesischen Meer
Picha: picture-alliance/AP Photo/U.S. Navy/M. L. Stanley

Manowari mbili za kubeba ndege za kijeshi za Marekani zinashiriki mazoezi kwenye Bahari ya China Kusini,wakati ambapo China pia ikifanya mazoezi kwenye eneo hilo hilo. Zhao Lijian, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China anasema kwamba mazoezi hayo yamefanyika kwa agenda ya siri ya Marekani na yanatishia usalama wa kanda hiyo.

Zhao alisema kwenye mkutano wa kila siku na wandishi habari mjini Beijing, kwamba lengo la Marekani kuendesha mazoezi hayo kwenye bahari ya China ya Kusini ni kutaka kuonyesha nguvu yake ya kijeshi.

Maafisa wa jeshi la wanamaji la Marekani walitangaza Jumapili kwamba manowari mbili zinazoendeshwa na nishati ya nyuklia za kubeba ndege za kijeshi, yaani USS Ronald Reagan na USS Nimitz, zilianza mazoezi kwenye bahari hiyo Jumamosi. Taarifa ilielezea kwamba mazoezi hayo yalilenga kubainisha uwezo wa vifaa vya kijeshi vya Marekani na vile vile dhamira thabiti ya nchi hiyo katika kusimamia hali ya kila taifa kutumia anga, bahari na kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Konflikt Südchinesisches Meer | Küstenwachen-Schiffe Philippinen, Hintergrund China
Meli ya walinzi wa pwani ya Ufilipino ikiipita meli ya walinzi wa pani wa ChinaPicha: Getty Images/AFP/T. Aljibe

China imekuwa ikidai kwamba takriban eneo zima la Bahari ya China ya Kusini ni eneo lake, na inapinga hatua yoyote ya jeshi la Marekani kwenye eneo hilo. Nchi zingine tano pia zimedai sehemu ya maji ya bahari hiyo, ambayo bidhaa za thamani ya dola trilioni 5 husafirishwa kila mwaka.

Südchinesisches Meer | Spratly Islands
Picha inayoonyesha bahari ya kusini ya ChinaPicha: Reuters/U.S. Navy

China inajaribu kudhibiti eneo hilo kwa kujenga kambi za kijeshi kando ya bahari ya China Kusini, jambo ambalo lilisababisha Marekani kupeleka manowari zake za kivita. Marekani haijachukuwa msimamo wa wazi kuhusu mzozo wa maji ya bahari ya China kusini, lakini inasisitiza kuhusu uhuru wa bahari hiyo kwa kila nchi.

Wiki iliyopita wabunge wa Marekani walipitisha muswada wa sheria ya vikwazo dhidi ya uongozi wa China baada ya kupitishwa kwa sheria tata ya usalama kwa ajili ya Hong Kong.

Miongoni mwa vikwazo hivyo ni kuzuia biashara za benki zinazoshirikiana na maafisa wa China. Kwa upande wake pia China iliabaini kwamba inataka kuchukuwa vikwazo vya kuwanyima visa baadhi ya maafisa wa Marekani baada ya uamzi kama huo uliochukuliwa na Marekani dhidi ya maafisa kadhaa wa Chama cha Kikomunisti cha China.