1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa itikadi kali AfD washika nafasi ya pili Ujerumani

Iddi Ssessanga
7 Julai 2023

Kutoridhika kwa wapiga kura na serikali ya muungano ya Ujerumani kumefikia kiwango cha juu. Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia ndio chama pekee cha upinzani kufaidika na mwelekeo huu, kulingana na utafiti mpya.

https://p.dw.com/p/4Tbgo
Symbolbild Partei AfD | Alternative für Deutschland | Fraktion im Bundestag 2021
Picha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Kuna ushahidi wa mabadiliko ya kisiasa nchini Ujerumani: Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD, ambacho kwa sehemu kinachukuliwa kuwa chama cha itikadi kali za mrengo wa kulia, kilifanikiwa kupata ushindi mara mbili katika uchaguzi wa mashinani ambao haujawahi kushuhudiwa mashariki mwa nchi hiyo na sasa kimepata mkuu wa wilaya na meya kwa mara ya kwanza.

Na katika jimbo la mashariki la Thuringia, kura za maoni hivi karibuni ziliiweka AfD katika asilimia 34, mbele ya vyama vingine vyote.

Lakini chama hicho cha siasa za kizalendo pia kinaendelea kupata mafanikio katika ngazi ya shirikisho: Kura ya hivi karibuni zaidi ya maoni ya Dimap ilitafiti wapiga kura 1,305 wa Ujerumani wanaostahiki kati ya Julai 3 na 5 na kubainisha kuwa AfD inaungwa mkono na asilimia 20 ya wapiga kura nchini kote.

Soma pia: Kushamiri kwa itikali kali za kulia huenda kukazuwia uhamiaji wafanyakazi wenye ujuzi

Hii inawafanya kuwa chama cha pili cha kisiasa cha Ujerumani, nyuma ya muungano wa mrengo wa kulia wa Christian Democrat Union na Christian Social Union, CDU/CSU, ambao walipoteza uungwaji mkono wa asilimia 1 tangu Juni na sasa wanafikia asilimia 28.

Bürgermeisterwahlen in Raguhn - Hannes Loth
Mgombea wa chama cha AfD Hannes Loth ndiye meya mpya wa mji mdogo wa RAguhn-Jeßnitz, katika jimbo la Saxon-Anhalt, mashariki mwa Ujerumani.Picha: Sebastian Willnow/dpa/picture alliance

Wakati huo huo, muungano unaotawala wa vyama vitatu bado hauwezi kudai uungwaji mkono mkubwa kote nchini: Chama cha mrengo wa kushoto cha Kansela Olaf Scholz cha Social Democrats, SPD, kimesalia katika asilimia 18, kile cha walibearali cha Free Democrats, FDP, kiko kwa asilimia 7, na watetezi wa mazingira die Grüne kimeshuka kwa asilimia nyingine hadi 14 tu - kiwango kibaya zaidi katika kipindi cha miaka mitano.

Chama kidogo zaidi cha upinzani bungeni, chama cha mrengo wa kushoto cha kisoshalisti - ambacho kilichowakilisha hisia za kuipinga serikali mashariki mwa nchi kwa miaka kadhaa baada ya kuungana tena kwa Ujerumani - kingeanguka hata chini ya alama 5, kizingiti cha uwakilishi katika bunge la shirikisho, Bundestag.

Uungwaji zaidi wa mitazamo ya mrengo mkali ya kulia

Wapiga kura hawana hofu na AfD na sera zake kuliko walivyokuwa: Asilimia 69 ya waliohojiwa bado wanaamini kuwa kuna watu wengi wenye siasa kali za mrengo wa kulia katika AfD - lakini miaka sita iliyopita, idadi hiyo ilikuwa asilimia 85. Na uidhinishaji wa msimamo mkali wa AfD kuhusu uhamiaji unaongezeka.

Soma pia: Scholz asema umaarufu wa AfD ni "moto wa mabua"

Kuwasili kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi katika mwaka wa 2015 na 2016, wengi wao wakikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, kulichochea kuibuka kwa chama cha AfD katika msingi wa vuguvugu la ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni lililoanza mashariki mwa nchi hiyo.

Mnamo mwaka wa 2017, zaidi ya theluthi moja ya wapiga kura kote nchini Ujerumani walisema kuwa wanafikiri ni vyema AfD ilitaka kupunguza wimbi la wageni na wakimbizi zaidi ya vyama vingine. Lakini sasa, takwimu hii zimeongezeka hadi asilimia 42.

Koalitionsgespräche zwischen SPD, Grünen und FDP in Berlin
Viongozi wa vyama vitatu vinavyotawala Ujerumani kwa sasa: Kansela Olaf Scholz wa SPD, katikati (aliesonga kidole), Annalena Baerbock, kushoto kabisaa, waziri wa mambo ya nje kutoka chama cha Kijani, Robert Habeck, wa pili kushoto, naibu kansela na waziri wa uchumi, Christian Linder, wa pili kulia, waziri wa fedha na mwenyekiti wa FDP, na Volker Wissing wa FDP.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Sasa, asilimia 55 wanasema wanathamini msimamo wa wazi wa AfD katika masuala mengi na ailimia 53 wanasema AfD ina ufahamu bora wa mahitaji ya usalama ya watu kuliko vyama vingine. CDU/CSU pekee ndivyo vilivyopata alama bora zaidi kwenye sera ya usalama.

Je, kizuwizi dhidi ya AfD kinaporomoka?

Idadi kubwa ya wafuasi wa AfD wanasema wangepigia kura chama cha mrengo wa kulia hasa kutokana na kutoridhishwa na vyama vingine, na si kwa sababu wanakubaliana na imani zake za mrengo mkali wa kulia. Lakini asilimia 77 ya wafuasi wa AfD wanasema kwamba misimamo ya chama ni "karibu" au hata "karibu sana" (asilimia 20) na misimamo yao wenyewe.

Soma pia: Chama cha AFD kinaweza ushtakiwa kwa siasa za chuki

Kufikia sasa, vyama vingine vyote vikuu vya Ujerumani vimekataa kabisa ushirikiano wowote na AfD, na asilimia 43 ya wapiga kura wanakubaliana na msimamo huu. Lakini wengi sasa wanasema wanaunga mkono uamuzi wa hali ya juu zaidi, wa kesi kwa kesi.

Zaidi ya chama kingine chochote, AfD inanufaika kutokana na kutoridhika kwa wapiga kura na serikali ya shirikisho. Kwa ujumla, ni takribani asilimia 25 tu ndio wanaridhishwa na utendaji wa serikali kwa sasa.

Hata miongoni mwa wafuasi wa SPD na Greens, makadirio ya kukubalika kwa serikali ni takriban asilimia 50 tu, na wafuasi wa FDP kwa muda mrefu wamekuwa wakizidi kukosoa.

Ukoloni wa Ujerumani na athari zake kwa sasa

Wachunguzi wa kura za maoni wa shirika la infratest waligundua hali ya kutokuwa na uhakika nchini Ujerumani. Ingawa hali ya hewa si mbaya kama ilivyokuwa msimu uliopita wa mapukutiko, asilimia 77 ya waliohojiwa wanasema wana wasiwasi kuhusu hali ya jumla nchini.

Soma pia: Maoni: Manifesto ya AfD ni hatari kwa Ujerumani

Mfumuko wa bei, mabadiliko ya hali ya hewa na uhamiaji vinaongoza orodha ya wasiwasi, wakati asilimia 16 tu bado wanataja vita vya Ukraine, asilimia 15 wana wasiwasi juu ya kuongezeka kwa umaarufu wa AfD na asilimia 11 kuhusu hali ya uchumi wa Ujerumani.

Ingawa wengi wanasema mabadiliko ya hali ya hewa ni suala muhimu, wachache wanataka kuona hatua kali za kukabiliana nayo. Wapiga kura wanaonekana kukosoa sera za chama cha Kijani na majaribio yao ya kuharakisha sheria ya mazingira.

Na asilimia 80 ya wafuasi wa AfD, asilimia 74 ya wafuasi wa FDP, na asilimia 64 ya wafuasi wa CDU/CSU wanakataa dhana ya marufuku na vikwazo vikali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Makala hii ilitafsiriwa kutoka Kijerumani