1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya mseto Ujerumani yazozana kuhusu uraia

Saumu Mwasimba
28 Novemba 2022

Chama cha FDP kilichoko kwenye serikali ya mseto pamoja na SPD na Kijani,kinapinga mpango wa kulegezwa sheria ili kurahisisha wageni kupata uraia wa Ujerumani ndani ya kipindi kifupi cha kuishi nchini

https://p.dw.com/p/4KC8x
Berlin Bundestag | Generaldebatte in der Haushaltswoche | Christian Lindner und Robert Habeck
Picha: Christian Spicker/IMAGO

Wanachama wa ngazi za juu wa chama kidogo kilichoko kwenye serikali ya muungano ya Ujerumani wanataka kuuzuia mpango wa kulegeza sheria za kupata uraia nchini Ujerumani,mpango unaopigiwa upatu na washirika wao wakubwa serikali chama cha Social Democratic SPD.

Chama cha Free Democratic FDP kinasema kwamba serikali inapaswa kwanza kuchukua hatua zaidi kuhakikisha watu wanaoishi nchini Ujerumani kinyume cha sheria wanarudishwa katika nchi zao. Kansela Olaf Scholz na waziri wake wa mambo ya ndani Nancy Faeser wote ni kutoka chama cha SPD chama amacho kinafuata siasa za wastani za mrengo wa shoto,katika siku za hivi karibuni wameonesha nia ya kuwa tayari kuendelea haraka na hatua ya kulegeza sheria.

Na hatua hiyo kimsingi ni moja kati ya msururu wa mageuzi ambayo serikali ya mseto inayoongozwa na Kansela huyo ya vyama vitatu ilikubaliana kuyashughulikia pindi itakapochukua madaraka kiasi mwaka mmoja uliopita. Hata hivyo hivi sasa wabunge kutoka kambi ya chama cha Free Democratic ambao walionesha huko nyuma kushirikiana zaidi na kambi ya siasa za wastani za mrengo wa kulia kabla ya kujiunga na muungano huu unaoongozwa na Kansela Scholz,wanaupinga mpango huo na kuuwekea kizingiti.

Deutschland Migration l Einbürgerung
Picha: Inga Kjer/photothek/imago Images

Chama hicho cha FDP kwa hivi sasa kinajikokota katika uchunguzi wa  maoni ya wananchi nchini Ujerumani. Kinashikilia kwamba ahadi iliyotolewa kwenye serikali ya muungano kuhusu mageuzi hayo ilitakiwa kwanza kupunguzwa kwa idadi ya wahamiaji wasiokuwa wahalali na kufikia sasa chama hicho kinatowa hoja kwamba ni hatua ndogo sana iliyochukuliwa katika suala hilo.

Katibu mkuu wa FDP Bijan Djir Sarai ameliambia gazeti la hapa Ujerumani la Rheinische Post kwamba huu sio wakati wa kulegeza sheria za kupata uraia nchini Ujerumani kwasababu hakuna hatua hadi sasa iliyopigwa katika suala la kuwarudisha makwao wahamiaji wasiokuwa halali  na pia katika suala la kukabiliana na uhamiaji haramu.

ARCHIV | Deutschland Dresden | Demonstration "Refugees Welcome"
Picha: Jens Meyer/AP Photo/picture alliance

Katibu mkuu huyo wa FDP ameongeza kusema kwamba serikali ya mseto haipaswi kuchukua hatua ya pili kabla ya kushughulikia ya kwanza. Kwa upande mwingine kiongozi wa kamati ya ulinzi bungeni Marie- Agnes Strack-Zimmermann kutoka chama hicho cha FDP amesema ni sawa kwa watu walioishi muda mrefu na kufanya kazi nchini Ujerumani kujumuishwa haraka.

Kwahivyo anasema kabla ya waziri wa mambo ya ndani Faeser kulifanya suala la kulegeza sheria ya kuomba uraia nchini Ujerumani kuwa kipaumbele chake,anabidi kwanza ahakikishe watu wanaoishi Ujerumani kinyume cha sheria,wale ambao pia wanamulikwa na vyombo vya sheria,wanarudishwa walikotoka kama inavyotakiwa.

Mpango wa Faeser unataka watu kuwa na haki ya kupata uraia wa kijerumani baada ya kukaa kihalali  katika nchi hii miaka mitano au mitatu kwa wale watakaokuwa wamefanikiwa kujijumuisha kwenye jamii ipasavyo,badala ya watu kusubiri miaka minane au sita kama ilivyo sasa. Kadhalika serikali ya Muungano katika ahadi zake ilizotowa mwaka jana walikubaliana kuondowa vikwazo  kuhusu suala la uraia pacha.