CAF-shirikisho la dimba la Afrika miaka 50 leo. | Michezo | DW | 07.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

CAF-shirikisho la dimba la Afrika miaka 50 leo.

Shirikisho la kabumbu la Afrika lililoundwa mwaka 1957 na nchi 4 linaadhimisha leo alhamisi miaka 50 likiwa sasa na wanachma 53.

Sherehe hizo zilianza kwa changamoto mjini Cairo baina ya mabingwa wa Afrika-Misri na Sweden na baadae mwezi huu tafrija nyengine za kuadhimisha mwaka wa 50 wa dimba la Afrika zitafanyika nchini Sudan na Ethiopia kukumbuka kuasisiwa kwa CAF-shirikisho la dimba la Afrika,1957-miaka 50 kamili iliopita.

Mwanachama wa 4 aliehusika na kuundwa kwa CAF-Afrika Kusini,anapanga maadhimisho yake hapo Oktoba mwaka huu.

Shirikisho la dimba la Afrika-CAF-ambalo linaadhimisha sasa miaka 50 tangu kuasisiwa ndilo la pili kwa ukubwa duniani au ndani ya FIFA baada ya UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya lenye wanachama 55 .CAF ina wanachama 53 –mbali sana na pale ilipoasisiwa na mataifa 4:Misri-kwenye makao makuu yake mjini Cairo,Ethiopia,Sudan na Afrika Kusini iliorudi katika dimba la Afrika 1994 baada ya kitambo kirefu cha kususiwa kutokana na siasa zake za ‚aparthied’-ubaguzi na mtengano.

Kinyume na UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya,ambalo ndilo tajiri kabisa duniani,CAF ni masikini na linategemea sana ruzuku kutoka mfuko wa hazina ya FIFA kwa kima cha dala milioni 2.5 kwa mwaka.

Mavuno ya CAF kutoka kombe la Africa Cup,linalogombewa kila baada ya miaka 2,hayatoshi kuendesha shughuli zake ,lakini kabla ruzuku kutoka FIFA,fedha hizo zikichangia 80% ya mfuko wake.

Kwa klabu zake barani Afrika,pia hazina zao si nzuri na mara nyingi zategemea kuuza wachezaji wake n’gambo kujaza mifuko yao.Afrika bado haijaendelea kutumia TV kuuza haki za dimba na kuvuna mapato kama ilivyo Ulaya,Amerika,Asia,New Zealand na Australia.

Ama kuhusu maendeleo yake ya dimba mnamo nusu karne iliopita,hakuna shaka, bara la Afrika limetoa mastadi wakubwa:akina Abedi Pele na Michael Essien(Ghana),George Weah (Liberia);Roger Milla na Samuel Eto’o (Kamerun); J.J.Okocha (Nigeria) na chipukizi wa leo Didier Drogba wa Cort d’Iviore.

Timu zake za taifa lakini, hazikufua dafu katika Kombe la dunia na kinyume na alivyobashiri Pele (mfalme wa dimba duniani) kwamba Afrika ingelivunja ungo na kutoroka na Kombe la dunia kabla kumalizika karne ya 20 iliopita,hatua ya mbali kabisa ni robo-finali kwa simba wa nyika-Kamerun,Itali,1990 na Senegal huko Korea ya kusini na Japan 2002.

Lakini, Afrika imepiga hatua kiuwakilishi katika Kombe la dunia-baada ya kuwa na timu 1 tu-Morocco, 1970 huko Mexico na Zaire, 1974 hapa Ujerumani, Afrika leo ina timu 5 na katika kombe lijalo la kwanza barani Afrika 2010, itakuwa na timu 6-pamoja na wenyeji „Bafana Bafana“ au Afrika Kusini.

Katika FIFA-shirikishbo la kabumbu duniani,bado Afrika haina sauti na ushawishi mkubwa na jaribio la mkamerioun Issa HaYATOU KUMUANGUSHA KITINI Sepp Blatter kama rais wa FIFA 2002 lililishindwa.

Hayatou anasalia kuwa makamo-rais wa FIFA na rais wa CAF na hana azma ya kuna’gatuka hata baada ya kupita miaka 20 kitini.Wadhifa huo utagombewa tena 2009.

Kuandaliwa kwa Kombe la dunia la FIFA 2010 nchini Afrika Kusini, kunatoa changamoto kwa CAF na kwa kabumbu la Afrika linyanyue heba yake na kutamba katika dimba la dunia.Hongera basi,kabumbu la Afrika na hongeza CAF-shirikisho lake -siku hii ya kuzaliwa-miaka 50 iliopita!

 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHci
 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHci
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com