Bunge la Ujerumani yayatambua Mauwaji ya halaiki ya Waarmenia | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bunge la Ujerumani yayatambua Mauwaji ya halaiki ya Waarmenia

Bunge la Ujerumani limidhinisha takriban kwa sauti moja azimio linalotambua mauwaji ya halaiki ya waarmenia-zoezi la uchaguzi lililokosolewa na uturuki,mshirika muhimu na tete katika mzozo wa wakimbizi barani Ulaya.

Mjadala wa bunge la shirikisho Bundestag kuhusu mauwaji ya halaiki ya waarmenia

Mjadala wa bunge la shirikisho Bundestag kuhusu mauwaji ya halaiki ya waarmenia

Uamuzi wa bunge la Ujerumani Bundestag unaweza kukorofisha uhusiano ambao tokea hapo ni tete pamoja na Ankara,na hasa katika kutekeleza makubaliano yanayozusha mabishano kati ya Umoja wa ulaya na Uturuki,makubaliano yaliyofikiwa kutokana na juhudi za Ujerumani na ambayo yamesaidia kupunguza wimbi la wakimbizi barani Ulaya.

Azimio hilo lenye kichwa cha maneno "Kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya waarmenia na jamii nyengine za wakristo walio wachache,yaliyotokea miaka 101 iliyopita" limeungwa mkono na wabunge takriban wote waliohudhuria kikao hicho (mmoja amepinga na mwengine hakupiga kura upande wowote) . Nje ya jengo la bunge Reichtag, watu waliokuwa wakifuatilizia mjadala bungeni walibeba mabango yaliyoandikwa "miongoni mwa mengineyo "Ahsante."

Bunge la Ujerumani halituvumilia njama za kuzuwiliwa kutoa maoni yao

Deutschland Bundestag Armenienresolution

Waarmenia na wanaowaunga mkono wakibeba mabanga kuwashukuru wabunge wa ujerumani

Akifungua mjadala wa bunge spika wa bunge Prof. Nobert Lammert alisema kikao hicho cha bunge si mahakama na wala si jopo la wanahistoria,ila ni kikao cha wabunge wa Ujerumani wanaowajibika kwa kupitisha uamuzi kama huo.

Spika wa bunge la Ujerumani Prof. Norbert Lammert anasema:"Bila ya shaka tutaridhia aina zote za lawama,hata zile ambazo hazina msingi,lawama za uchokozi na nyenginezo. Lakini upande wa pili unabidi utambue pia kwamba vitisho vilivyolengwa kuzuwia uhuru wa watu kutoa maoni yao katika bunge la shirikisho Bundestag,havikubaliki."

Azimio hilo linakosoa pia jinsi utawala wa wakati ule Ujerumani-Reich,mshirika mkubwa wa kijeshi wa kile kilichokua kikijulikana kama enzi za Ufalme wa Ottoman "ulivyokaa kimya na kutozuwia uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Kansela Angela Merkel,waziri wake wa mambo ya nchi za nje Frank-walter Steinmeier na naibu kansela,ambae ndie mwenyekiti wa chama cha SPD,Sigmar Gabriel hawakuhudhuria kikao hicho cha bunge.

Balozi wa Ujerumani mjini Ankara aitwa na serikali ya UIturuki akajieleze

Deutschland Debatte im Bundestag um Anerkennung des Völkermordes durch die Türkei an den Armeniern

Waandamanaji waliobeba bendera za Uturuki walikusanyika pia Karibu na jengo la Bunge mjini Berlin

Muda mfupi baada ya kura kupigwa bungeni Uturuki iliutaja uamuzi wa bunge la shirikisho la kuyatambua mauwaji ya halaiki ya waarmenia kuwa ni "kosa la kihistoria" na kusema halina maana yoyote kwao. Uturuki imemwita pia balozi wa Ujerumani mjini Ankara akajieleze. Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim alisema hata kabla ya uamuzi wa bunge la shirikisho Bundestag kwamba kura hiyo ni "mtihani wa kweli kwa urafiki kati ya ujerumani na Uturuki". Kwa upande wao serikali ya Armenia mjini Erevan imeusifu uamuzi wa bunge la shirikisho mjini Berlin."Ni mchango wa maana wa Ujerumani katika kutambuliwa na kulaaniwa na jumuia ya kimataifa mauwaji ya halaiki ya waarmenia,na mchango mkubwa pia katika juhudi za kuepukana na mauwaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadam-" imetajwa katika taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje wa Armenia mjini Erevan.

Azimio la Bundestag ni hatua ziada kuelekea kutambuliwa rasmi na Ujerumani mauwaji ya halaiki ya waarmenia yaliyotokea mwaka 1915,baada ya rais wa shirikisho Joachim Gauck kuyataja kuwa ni mauwaji ya halaiki.

Waarmenia wanakadiria watu milioni moja na laki tano waliuliwa mwishoni mwa enzi za ufalme wa Ottoman. Uturuki lakini inasema kwa upande wake vilikuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe,vilivoshajiishwa na njaa na kupelekea waarmenia kati ya laki tatu na laki tano na idadi kama hiyo ya waturuki kuuwawa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com