Umoja wa Ulaya wazingatia kutumia mali za Urusi inazozizuia
19 Machi 2024Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema atapendekeza katika mkutano wa hapo kesho kwamba umoja huo utumie asilimia 90 ya mapato yatokayo kwenye mali za Urusi zilizozuiwa barani Ulaya ili kununua silaha kwa ajili ya Ukraine.
Borrell ameyasema hayo hii leo mjini Brussels na kusisitiza kuwa fedha hizo ambazo zinaweza kufikia euro bilioni 3 kila mwaka, zingelitolewa kupitia Mfuko wa amani wa Ulaya na kwamba asilimia 10 iliyosalia ijumuishwe kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya ambayo itatumiwa katika kuongeza uwezo wa ulinzi wa Ukraine.
Hayo yanajiri wakati mapambano yakiendelea kati ya Urusi na Ukraine. Urusi imesema inapanga kuwahamisha watoto wapatao 9,000 kutoka eneo la mpakani la Belgorodambalo limekuwa likishambuliwa mno katika siku za hivi karibuni. Marekani kwa upande wake imesema kamwe haitoruhusu Ukraine kushindwa.