1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara ya madawa ya kulevya yatishia utulivu Afrika Magharibi

Mohmed Dahman21 Agosti 2008

Magharibi ambapo wataalamu wa madawa ya kulevya wanasema magenge ya Amerika Kusini yanatishia kuzigeuza nchi hizo ndogo kuwa mataifa ya madawa ya kulevya.

https://p.dw.com/p/F26S
Ghana licha ya kuwa na demokrasia thabiti pia ni uchochoro wa kupitishia madawa ya kulevya

Kukamatwa kusikotarajiwa kwa madawa hayo kuanzia Guinea- Bissau na Mauritania hadi Siera Leone na Senegal kunaonyesha jinsi hatua zilivyo ovyo katika kukabiliana na mashirika ya madawa ya kulevya ambayo yanaendesha magenge yenye mawasiliano ya karibu na idara za usalama licha ya kupatiwa msaada kutoka Marekani na nchi za Ulaya.

Hatari hiyo inakuja katika wakati muhimu kwa Afrika Magharibi ambapo mataifa kadhaa yamekuwa yakijijenga upya baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na eneo hilo limevuta utashi mkubwa wa wawekezaji.

Emmanuelle Bernard wa mchambuzi wa masuala ya Afrika Magharibi katika jopo la ushauri la kimataifa la International Crisis Group anasema hatari ni kubwa sana kwamba fedha kutoka biashara ya madawa ya kulevya zimekuwa zikishindana na ujenzi wa asasi jambo ambalo mataifa hayo yanatakiwa yafanye hivi sasa.

Lakini anasema inakuwa vigumu kufanya hivyo wakati wale walioko madarakani wanapohusika na biashara ya madawa ya kulevya.

Hakuna mahala penye kuonyesha vizuri zaidi hatari ya kuchanganya fedha hizo za madawa ya kulevya na taifa dhaifu kuliko Guinea- Bissau. Vitisho vya kifo dhidi ya waziri mmoja aliekuwa akipiga vita biashara ya madawa ya kulevya vilifuatiwa na jaribio la mapinduzi na kukamatwa kwa mkuu wa wanamaji.

Anthonio Mazitteli mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Ofisi ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi anakubali kwamba askari na mafunzo ni mambo mazuri lakini pia wanatakiwa watu waje na bunduki magari ya deraya na fedha kwa ajili ya watu wanaotowa habari kwa siri kwa polisi.

Waziri wa sheria wa Guinea Bissau amesema ataendelea kupambana na biashara ya madawa ya kulevya lakini polisi wake wa sheria wakiwa na silaha chache au magari,risasi chache au mafuta wanashindwa kukabiliana na mtandao wa uhalifu wa kimataifa.Licha ya kuungwa mkono na mashushu wa Shirika la Upelelezi la Marekani FBI na DEA wamezuiliwa na majeshi kuipekua jeti iliokuwa ikitiliwa mashaka ambayo iilitua Bissau mwezi uliopita.

Wakati waliporuhusiwa kufanya upekuzi mbwa wanaonusa harufu walithibitisha kwamba unga wa madawa ya kulevya ulikuwemo ndani ya ndege lakini ndege hiyo ilikuwa tupu.

Siera Leone imepongezwa kwa ujenzi mpya wa nchi hiyo baada ya vita lakini waziri wake wa uchukuzi anachunguzwa na polisi baada ya kaka yake kukamatwa kufuatia kukamatwa kwa kilo 700 za unga wa madawa ya kulevya mwezi uliopita katika uwanja wa ndege mkuu wa nchi hiyo.

Hapo mwezi wa Januari meli yenye bendera ya Liberia ilikamatwa nje ya mwambao ikiwa na tani 2.5 za unga wa madawa ya kulevya.

Ghana ambayo inaonekana ni taifa thabiti la demokrasia barani Afrika na kipenzi cha wawekezaji pia imekuwa sehemu kuu ya kupitishia madawa ya kulevya kama ilivyothibitishwa na kukamatwa kwa wasichana wawili wa Uingereza kwa magendo ya madawa ya kulevya mwaka jana.

Wafanya biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya wanatumia fursa ya serikali dhaifu na ulinzi dhaifu wa mipakani kusafirisha unga wa madawa ya kulevya wenye thamani ya mamilioni ya dola kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya.