1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Waasi watumia mbinu mpya za mashambulizi

23 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPY

Maafisa wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq wamesema waasi inaonekana kuwa wanatumia mbinu mpya ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwa kutumia gesi za sumu.

Mkurugenzi wa hospitali moja mjini Baghdad amesema wana tiba wamekuwa wakiwatibu madarzeni ya wagonjwa walioathirika na sumu ya gesi ya chlorine baada ya wanamgambo kushambulia maeneo ya kiraia kwa kuripuwa kwa mabomu magari yenye kubeba gesi hiyo.Mashambulizi hayo mjini Baghdad na katika mji wa jirani wa Taji yameuwa watu wanane na kujeruhi wengine wengi kutokana na gesi hiyo ya sumu.

Wakati huo huo wanajeshi wa Marekani na wale wa Iraq wamekuwa katika hali ya tahadhari katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tokea kuripuliwa kwa msikiti wa Al Askari mjini Samarra.

Shambulio hilo katika mojawapo ya sehemu takatifu kabisa za Waislamu wa madhehebu ya Washia kumechochra wimbi la umwagaji damu wa kimadhehebu ambao umeisukuma nchi hiyo kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.