Al Ahly yashinda duru ya kwanza ya finali | Michezo | DW | 03.11.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Al Ahly yashinda duru ya kwanza ya finali

Al Ahly yatamba mbele ya Conton Sports ya kamerun katika duru ya I ya kombe la klabu bingwa.

Chinedu Ogbuke Obasi wa Hoffenheim.

Chinedu Ogbuke Obasi wa Hoffenheim.

Hoffenheim,klabu iliopanda msimu huu kutoka daraja ya pili yaendelea kuzusha maajabu katika Bundesliga-Katika La liga-ligi ya Spain,Real Madrid imekosa nafasi ya kuparamia kileleni na bao la dakika za mwisho dhidi ya Napoli jana limeipeperusha kileleni mwa Serie AC Milan. Young Africans baada ya kunguruma mbele ya simba mwishoni mwa wiki iliopita imekamilisha awamu ya kwanza ya Ligi ya Tanzania-bara kileleni. Paul Tergat na Cathrine Ndereba washindwa kuwika katika mbio za New York marathon nchini Marekani.Paul atokea 4.

Na Lewis Hamilton,ameibuka bingwa wa kwanza chipukizi katika umri wa miaka 23 kutwaa ubingwa wa mbio za motokaa za fomular one.

hayo na mengineo, ndio niliowaandalia jio ni hii:

Katika Bundesliga,Hoffenheim ilitamba tena mwishoni mwa wiki ilipoizaba Karlsruhe mabao 4-1 na hivyo imeparamia tena kileleni baada ya Leverkusen muda mfupi ijumaa kutwaa uongozi.Hoffenheim inaongoza kwa pointi moja ikiwa na jumla ya pointi 25.Leverkusen i ilitamba mbele ya Wolfsburg.

Mabingwa Bayern Munich walipanda hadi ngazi ya tatu ya Ligi wakiwa sasa na pointi 21 baada ya kuikandika Armenia Bielefeld 3-1.Schalke wana pointi 20 na wamesogea hadi nafasi ya 4. FC Cologne, iliwasangaza mashabiki wake ilipotamba kwa mabao 3:1 mbele ya Stuttgart nyumbani mwa Stuttgart.

Eintracht Frankfurt ilitoka nyuma jana na kuizaba Borussia Monchengladbach mabao 2:1.Borussia Dortmund walimudu suluhu tu ya bao 1:1 na Bochum.

Kwa ufupi, chipukizi waliotoka daraja ya pili Hoffenheim wanaendelea kugonga vichwa vya habari ,kwani kila mmoja anajiuliza chipukizi hawa wanatumia uchawi gani wa dimba hata kuzipiku klabu maarufu na kuongoza Bundesliga ?

Kocha wao Ralf Reinicke baada ya ushindi wa timu yake hapo jumamosi wa mabao 4-1 dhidi ya Karlsruhe, alieleza:

"Tumeridhika mno na mchezo wetu ukichukulia leo ulikuwa mchezo wetu watatu mnamo siku 6."

Kocha wa Hoffenheim akaendelea:

"Na sio tu ni kutokana na pointi 3 tulizoshinda lakini zaidi na kwa namna chipukizi wetu walivyotia fora usoni tena dakika zote 90 za mchezo."

Chipukizi wengine waliowasangaza mashabiki wao ni FC Cologne iliopanda daraja ya kwanza msimu huu kama Hoffenheim.Baada ya kuichapa stuttgart mabao 3-1, kocha wao Christoph Daum ambae zamani alikuwa pia kocha wa Stuttgart alisema:

"Kwetu sisi ushindi una maana ni pointi 3 zaidi mfukoni na kwetu ni muhimu sana kuelekea shabaha yetu ya kusalia daraja ya kwanza na kati kati mwa orodha ya Ligi."

Ama kocha wa mabingwa Bayern Munich, Jurgen klinsmann ameanza kuvuta pumzi ,kwani sasa mabingwa hao wakinza kuja juu.Klinsmann alisema,

"Sijui nafasi ngapi za kutia mabao tulizipata na kushindwa kuingiza.Hatahivyo, tumeridhika kuondoka uwanjani na pointi 3 na sasa tunaendelea na mlolongo wa ushindi tulioanza nao karibuni ."

Bayern Munich inarejea kati ya wiki hii katika champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya wakati klabu nyengine kama Hamburg zitaania kombe la ulaya la UEFA.

Huko Itali, AC Milan imechukua uongozi wa Serie A baada ya bao la dakika za mwisho dhidi ya Napoli iliocheza na wachezaji 10.

Udinese imetoka sare 2:2 na Genoa wakati Inter Milan iliondoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Reggina.

Ama katika La Liga-Ligi ya Spain ,Real Madrid imekosa nafasi nzuri kuparamia kileleni . Walimudu sare tu ya bao 1-1 na Almeria.Zikisalia dakika 8 kabla ya firimbi ya mwisho kulia,Real ikiongoza kwa bao 1:0, lakini Almeira iliambia Real kutangulia si kufika.Real sasa iko nafasi ya tatu-pointi 1 nyuma ya Villareal. Timu 4 za la Liga ziko sare kila moja ikiwa na pointi 12-nazo ni Deportivo la Coruna,Espanyol,Almeira na Sporting Gijon.

Katika Ligi ya Brazil,Sao Paulo ikijaribu kutwaa ubingwa kwa mara ya 3 mfululizo, iliparamia kileleni jana baada ya bao maridadi alilochapa wavuni Dagoberto kukamilisha ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Internacional.

Katika Kombe la klabu bingwa barani Afrika,Al Ahly ya Misri yatamba mbele ya Conton Sports Garoua ya Kamerun mjini Cairo. Conton yaahidi kutoroka na kombe nyumbani.

Na nchini Tanzania, awamu ya kwanza ya Ligi ya Tanzania bara imekamilika mwishoni mwa wiki huku Young Africans ilionguruma mbele ya Simba spots club mwishoni mwa wiki iliopita walipoendelea kushika usukani.

Mbio za magari za Formular One ambazo jana zilimtawaza bingwa mpya-nae chipukizi wa Uingereza mwenye umri wa miaka 23 Lewis Hamilton akiendesha motokaa ya McLaren-Mercedes. Hamilton alimpiku Felipe Massa sekunde za mwisho na kumpokonya taji alilodhani tayari ni lake kufuatia ushindi wake jana wa Brazilian Grand Prix.

Masa alibidi kufuta machozi kwa kukaribia tu kuwa bingwa wa kwanza kutoka Brazil tangu Ayrton Senna kutwaa taji hilo hapo 1991.Lewis Hamilton amemaliza akiwa na pointi 98 kufuatia mbio 18 katika miji mbali mbali.