Afrika Kusini: Kuuliwa kwa Terre′Blanche | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.04.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Afrika Kusini: Kuuliwa kwa Terre'Blanche

Taifa la rangi za upinde wa mvua liko mashakani? Kuuliwa Jumamosi iliopita kwa Terre'Blanche, aliyekuwa anafuata siasa za mrengo wa kulia sana, kulikuwa sawa na kama kumetokea mtikisiko wa ardhi huko Afrika Kusini.

default

Eugene Terre'Blanche(katikati), mkuu wa chama cha mrengo wa kulia sana cha AWB, akiongozwa na walinzi nje ya mahakama kuu ya Rand, mjini Johannesburg, baada ya kusikilizwa kesi ya wafuasi wake

Kwa haraka Rais Jacob Zuma alitoa mwito kwa wananchi wa Afrika Kusini wasizushe mzozano wa kikabila. Miaka 16 baada ya kumalizika mfumo wa siasa za ubaguzi wa rangi, bado havijaondoka vizingiti vyote vinavowatenganisha watu wa makabila mbali mbali ya nchi hiyo. Na watu wa siasa kali wanaitumia hali hiyo.

"Nimepigana dhidi ya ubwana wa watu weupe."

Huo ndio mwito wa Nelson Mandela baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani mwaka 1994."

"Nami nimepigana dhidi ya ubwana wa watu weusi. Nina ndoto ya kuishi katika jamii ya kidemokrasia ilio huru, ambao watu wote wataishi pamoja kwa masikilizano."

Nelson Mandela alikuwa na ndoto. Baada ya kuwa gerezani kwa miaka 27 na kuweko ukandamizaji wa miongo ya miaka, alitaka kuikomesha kabisa mitengano ya kikabila, pia kuiondosha mitengano hiyo katika vichwa vya watu. Ndoto yake haijaweza kutekelezeka hadi leo, kama vile anavofahamu mkurugenzi wa Taasisi juu ya Usawa na Masikilizano ilioko mjini Cape Town, Fanie du Toit...

" Tulifikiri kwamba nguvu za mwenendo wa masikilizano, ambao katika wakati ule ulikuwa wenye nguvu sana, utaweza, kwa muda mfupi, kuukiuka mfumo wa ubaguzi wa rangi. Lakini sasa tunaona kwamba haya ni mapambano ambayo ni lazima tuyaendesha kwa miongo fulani ya miaka."

Fanie du Toit lazima afahamu. Taasisi yake mwaka jana iliendesha uchunguzi wa maoni ya watu. Wanne kati ya Waafrika Kusini kumi hawawaamini watu wa rangi nyingine. Nusu ya Waafrika Kusini hawana uhusiano wa kijamii na watu wa rangi nyingine.

Watu wengi pia baada ya kumalizika siasa rasmi ya ubaguzi bado wanaishi katika mazingira yale yale, kama zamani. Kuna mitaa ya Wazungu na ile ya watu Weusi; pia tafauti za kijamii na za kiuchumi baina ya makundi hayo mawili zimezidi kuwa kubwa. Mzungu wa Afrika Kusini leo analipwa mshahara kwa kiwango cha mara kumi zaidi kuliko vile anavopata mtu Mweusi.

Umaskini na kutokuweko usawa kunapelekea kutokea mizozo, na mizozo hiyo inatumiwa na baadhi ya wanasiasa. Kiongozi wa jumuiya ya vijana ya chama tawala cha African national Congress, ANC, Julius Malema, mara nyingi anachochea na hadharani huimba ile nyimbo ya zamani ambayo inatoa mwito wa kuuliwa makaburu. Kwa Moeletsi Mbeki hilo ni jaribio la kubadilisha dira juu ya masuala muhimu. Moeletsi Mbeki ni ndugu wa rais wa zamani , Thabo Mbeki, na anaongoza Taasisi ya Afrika Kusini juu ya Masuala ya Kimataifa:

"Chama cha ANC hakijaweza kutimiza ahadi ilizotoa juu ya uchumi, na ambazo kimekuwa kikihubiria kwa miaka 16 iliopita. Kwa hivyo, Afrika Kusini inamtafuta mchawi ili kumfanya dhamana wa kushindwa ANC kufanya kitu. Wazungu wanafanywa kuwa dhamana juu ya kuzorota kwa siasa za kiuchumi za chama ANC."

Na hivyo ndivyo ndugu yake Moeletsi, yaani Thabo Mbeki, alivotamka mwaka 1998 mbele ya bunge, akizungumzia juu ya kuweko mataifa mawili ambayo yameigawa Afrika Kusini, lile la Wazungu walio matajiri na lile la watu Weusi walio maskini. Wakati huo, Mbeki alilaumiwa vikali kwa matamshi yake hayo. Wakati huo huo, baadhi ya Waafrika Kusini waliziona ishara kwamba mapengo baina ya watu Weusi na Wazungu yatapunguwa na kuwa madogo zaidi. Kwa mfano, Christopher Till, mkuu wa Makumbusho ya Enzi ya Siasa za Ubaguzi, ansema:

" Katika shule zetu unaona kwamba kuingiliana pamoja watu kunakwenda vizuri sana. Tunafurahi kuwaona watoto wa shule wakija katika jumba letu la makumbusho kama walio na haki sawa na marafiki. Katika mazingira yao wamechanganyika pamoja. Ni wazee wao waliokulia katika mazingira mengine kabisa."

Hamna shaka: Afrika Kusini inajifungua, japokuwa polepole. Ili kwamba watu wenye siasa kali wasiweze tena kupata usemi, wanasiasa sasa wanaingilia kwa nguvu. Masaa machache baada ya kuuliwa Terre'Blanche, aliyekuwa na siasa za mrengo wa kulia sana, Rais Jacob Zuma alitoa mwito kwa Waafrika Kusini watulie, na kwamba kisa hicho kisitumiwe kuchochea chuki. Wiki ijayo watahukumiwa hao wanaosemwa kwamba wamefanya mauaji hayo. Naye Julius Malema amefungwa mdomo na chama chake. Anatakiwa asiimbe tena nyimbo za kibaguzi. Lakini hiyo ni hatua ndogo tu kuelekea njia ndefu ya kuelekea taifa la kweli lenye rangi za upinde wa mvua.

Mwandishi: Kriech, Adrian/ZR/Othman,Miraji

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com