Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Makala | DW | 13.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Gazeti la die tageszeitung ambalo limeukariri wito uliotolewa na washindi wa tuzo ya Nobel wa kuwataka wahusika wasinyamae kimya wakati wanawake wanaponyanyaswa kingono na hasa kwenye  maeneo ya migogoro.

die tageszeitung

Mwito huo wa washindi wa tuzo ya Nobel ulitolewa mjini Oslo nchini Norway Jumanne iliyopita na daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Denis Mukwege na Yesidin Nadia kutoka Iraq. Katika hotuba zao za kutoa shukurani kwa tuzo walizotunukiwa wanaharakati hao wameitaka jumuiya ya kimataifa kutonyamaza kimya wakati wanawake wanafanyiwa uhalifu wa kutekwa na kugeuzwa watumwa.

Gazeti hilo la die tageszeitung limemnukulu mwanaharakati Yesidin Nadia kutoka Iraq akisema, wanaopaswa kulaumiwa juu ya mauaji ya wanawake yaliyofanywa nchini Iraq, na magaidi wanaojiita dola la kiislamu, siyo tu magaidi hao, bali pia wale walioangalia kwingineko wakati  uhalifu ulipofanyika. Kwa upande wake Dr Mukwege kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amekaririwa na gazeti hilo la die tageszeitung akiitata jumuiya ya kimataifa iwalipe fidia wanawake waliotendewa uhalifu wa kubakwa nchini mwake, ili waweze kujenga maisha mapya.

Neuer Zürcher

Nalo gazeti la Neuer Zürcher wiki hii limechapisha makala juu ya rais wa Tanzania John Magufuli  ambaye amepewa jina la utani  la tingatinga. Jee kwa nini anastahili kupewa jina hilo. Gazeti la Neuer Zürcher linaeleza kwamba hapo mwanzoni rais Magufuli aliingia madarakani na ilani ya kupiga vita ufisadi, lakini sasa rais huyo anagusa nyanja zote za siasa.  Mara rais huyo anataka wafungwa watumikishwe kazi ngumu na mara anataka watoto wengi wazaliwe nchini.

Katika mwendelezo wa sera yake ya kugusa kila nyanja ya siasa gazeti la Neue Zürcher linasema rais Magufuli safari hii amejitosa katika siasa za zao la korosho bila ya kujali misingi ya  soko. Kiongozi huyo wa Tanzania hivi karibuni aliamrisha bei ya korosho kuwa asilimia 10 juu ya bei ya soko. Na alipobainisha kwamba wanunuzi wa ndani hawakuwa tayari kukubali bei hiyo aliagiza benki ya serikali kununua korosho zote nchini na kazi ya kusafirisha zao hilo ilifanywa na jeshi.

Gazeti hilo  la Neue Zürcher limeusifu uamuzi wa rais magufuli wa kuagiza korosho hizo ziongezwe  thamani  kabla ya kuuzwa nje. Gazeti  hilo linasema uamuzi  huo unastahili kusifiwa kwa sababu  nchi nyingi za Afrika zinategemea kwa kiwango kikubwa, kuuza malighafi ili kuingiza fedha za kigeni.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii linalalamika kwamba mpango wa serikali ya Ujerumani juu ya kulisaidia bara la Afrika umekwama. Gazeti hilo linasema serikali ya Ujerumni imetoa kauli nyingi juu ya mpango wake wa kulisaidia bara la Afrika  mithili ya ule ulioitwa Marshall Plan uliotekelezwa na Marekani barani Ulaya baada ya kumalizika vita vikuu vya pili.  Ni sehemeu ndogo tu ya mradi huo uliotangazwa na waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller unaosonga mbele kwa mwendo wa kusuasua.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Hadi sasa mapatano ya ushirikiano yametiwa saini baina ya Ujerumani na nchi tatu tu za Afrika ambazo ni Tunisia, Ghana na Ivory Coast.. Gazeti  la Frankfurter Allgemeine linafahamisha kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya Ujerumani na nchi nyingine tatu za Afrika Ethiopia, Morocco na Senegal. Gazeti hilo linaeleza kwamba lengo la ushirikiano huo ni kuweka mazingira ya kuiwezesha sekta binafsi kuboresha uwekezaji vitega uchumi barani Afrika.

Gazeti  la Frankfurter Allgemeine linasema serikali ya Ujerumani inatumai ushirikiano huo utaboresha maisha ya watu na hivyo kuweza kuepusha mawimbi ya wakimbizi kutoka Afrika. Hali ya kiuchumi ikiwa bora itawezesha kutenga fursa za ajira kwa vijana, na hivyo vijana hao hawatalihama bara lao. Frankfurter Allgemine limefahamisha kwamba Ujerumani imeahidi kutenga Euro milioni 100 kwa kila nchi iliyofikia nayo mapatano ya ushirikiano, yaani Tunisia, Ghana na Ivory Coast. Fedha hizo zinakusudiwa kutumika kwa ajili ya kuendeleza sekta ya nishati na kuleta mageuzi katika sekta ya fedha.

Hata hivyo gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani  kwamba mpaka sasa wadau wa sekta binafsi nchini Ujerumani hawajajitokeza kwa haja, iliyokusudiwa, kwa sababu hakuna utaratibu mzuri wa kuratibisha juhudi.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo