1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya2 Mei 2014

Wiki hii magazeti hayo yameandika juu ya ziara ya Waziri Kerry barani Afrika na juu ya mtazamo wa vijana milioni 2 wa Afrika Kusini watakaopiga kura kwa mara ya kwanza nchini mwao

https://p.dw.com/p/1Bt0d
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akisalimiana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry akisalimiana na Rais Salva Kiir wa Sudan KusiniPicha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Gazeti la "die tageszetung" limeandika juu ya ziara ya barani Afrika ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba Waziri Kerry ameenda Afrika wakati mujarabu .Kwani amewasili wakati ambapo mazungumzo yanafanyika mjini Addis Ababa juu ya kuutatua mgogoro wa Sudan Kusini.

Gazeti hilo linasema Waziri Kerry anawasili barani Afrika wakati ambapo mgogoro wa Sudan Kusini unapamba moto. Mazungumzo juu ya kuleta amani Sudan na Sudan Kusini yanafanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika na kwa hivyo siyo sadfa kwamba Kerry ameenda Afrika wakati huu. Lengo la ziara ya Waziri huyo kwa jumla ni kusisitiza umuhimu wa haki za binadamu na demokrasia.

Marekani yashiriki moja kwa moja barani Afrika

Gazeti la " der Freitag" wiki hii limechapisha makala juu ya sera mpya ya Marekani barani Afrika. Gazeti hilo linasema hapo awali Marekani iliziunga mkono serikali za Afrika kutokea mbali, lakini sasa imeamua kuwapeleka wanajeshi wake barani Afrika.Kulingana na sera yake, Marekani inasema "yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo".

Kwa Marekani migogoro ya Iraq na Afghanistan imeshapita.Macho sasa yanapaswa kuangaziwa barani Afrika.Gazeti la "der Freitag" linasema katika kuitekeleza sera hiyo, Marekani inalenga shabaha mbili, kwanza kuwa tayari kushiriki kijeshi na pili kutumia diplomasia kwa njia ya busara.Lakini katika utekelezaji wa shabaha hizo mbili, Marekani inabana matumizi kwa kadri inavyowezekana.

Wanajeshi 5000 wa Marekani wapo barani Afrika

Gazeti la "der Freitag" linaeleza kuwa nchi za Ulaya zitashiriki pia moja kwa moja katika harakati za kijeshi kwa kushirikiana na nchi Afrika. Lakini gazeti hilo limefahamisha katika taarifa yake kuwa Marekani tayari inao wanajeshi 5000 barani Afrika.

Watapiga kura kwa mara ya kwanza Afrika Kusini


Gazeti la "Die Zeit" linawazungumzia vijana milioni 2 wa Afrika Kusini watakaopiga kura kwa mara ya kwanza tokea kuondolewa mfumo wa kibaguzi nchini humo.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba tofauti na wazazi wao,waliopambana na utawala wa makaburu, vijana hao hawaziamini tena ahadi zinazotolewa juu ya demokrasia. Ni thuluthi moja tu ya vijana hao waliojiandikisha kupiga kura, licha ya wazazi wao kujitoa mhanga katika kuipigania haki ya kupiga kura.


Gazeti la "Die Zeit" limeandika katika makala yake kwamba vijana wengi wanakiunga mkono chama kinachoitwa Economic Freedom Fighters, EFF kilichoanzishwa na Julius Malema ambae hapo awali alikuwa mpambe madhubuti wa Rais Jacob Zuma. Malema aliefukuzwa chama tawala, ANC anataka migodi itaifishwe na wamiliki wakubwa wa ardhi wanyang'anywe sehemu ya utajiri wao.

Madhara ya mbung'o kupatiwa dawa karibuni

Gazeti la "Die Zeit" wiki hii pia limeripoti juu ya mafanikio yaliyopatikana katika juhudi za kupambana na madhara yanayosababishwa na mbung'o.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba watafiti wameutambua mpangilio wa visadifu(genes) vya mbung'o .Mdudu huyo ananyonya damu ya binadamu na ya wanyama kadhalika na kusababisha maradhi ya kusinzia. Gazeti hilo limearifu katika makala yake kuwa watafiti wameweza kubainisha kwamba mbung'o ana mpangilio wa visadifu na alama milioni 366 zinazoonyesha jinsi mpangilio huo ulivyojengeka katika mwili wa mbung'o.

Gazeti la "Die Zeit" limemnukuu mtaalamu Christian Meyer kutoka chuo cha Bernhard Nocht cha magonjwa ya nchi za joto, akisema kwamba utafiti huo utasaidia katika juhudi za kutengeneza dawa ya kuviulia vidudu hivyo. Hata hivyo amesema itachukua miaka kadhaa kabla ya kufikia kwenye lengo hilo. .

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo