Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 07.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kufurika kwa majeshi ya nje barani Afrika, juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuenea kwa maradhi ya saratani katika nchi za Afrika

Wakufunzi wa kijeshi wa Marekani barani Afrika

Wakufunzi wa kijeshi wa Marekani barani Afrika

Gazeti hilo linasema mauaji yanayotokea takriban kila siku,yanathibitisha kwamba maisha ya raia wa kawaida bado yamo hatarini licha ya kuwapo kwa majeshi ya Ufaransa nchini humo. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba watu wengi wanauawa kwa sababu tu ya kuwamo katika dini fulani.

Majeshi ya nje yajazana barani Afrika

Gazeti la "Berliner Zeitung" linazungumzia juu ya kusongamana kwa majeshi ya nchi za nje barani Afrika. Gazeti hilo linasema sasa imekuwa kana kwamba mtindo mpya wa kukata nywele umeingia mjini, jinsi Marekani,Ufaransa na nchi nyingine zinavyoyapeleka majeshi yao barani Afrika. Gazeti la "Berliner Zeitung" limearifu kwa kuzikariri duru za Marekani kwamba, maalfu ya wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwapo Iraq,au Afghanistan sasa wanatayarishwa kupelekwa Afrika. Askari wa Marekani sasa wako katika nchi 49 za Afrika.

Gazeti la "Berliner Zeitung" pia limefahamisha kwamba Ufaransa kwa sasa imewaweka jumla ya wanajeshi wake alfu 10 katika nchi nane za Afrika.Gazeti "Berliner Zeitung" linasema na sasa Ujerumani nayo inawapeleka wanajeshi wake barani Afrika.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine"pia linauzungzumia mgogoro wa Jamhuri ya Kati. Linasema katika makala yake kwamba kutokana chuki ya kidini iliyopo sasa katika nchi hiyo ni vigumu kuamini iwapo siku moja itawezekana tena kwa watu wa nchi hiyo kuishi pamoja kwa amani.

Hata hivyo gazeti la "Rheinische Post" linahoji kwamba migogoro ya barani Afrika haitokani na sababu za kidini au za ukabila. Gazeti hilo linaeleza kuwa migogoro ya barani Afrika haizuki tu kutokana na sababu za ukabila au udini.Bali pana ushahidi wa kuthibitisha kwamba migogoro hiyo inatokana na sababu za kisiasa na kiuchumi. Na ndiyo sababu kwamba anaetaka kusaidia katika juhudi za kuitatua migogoro ya bara hilo asikurupuke tu na kujiingiza kijeshi.

Maradhi ya saratani yaenea Afrika vile vile

Gazeti la "Die Zeit" linazungumzia juu ya kuenea kwa maradhi ya saratani katika nchi zinazoendelea ,ikiwa pamoja na barani Afrika. Gazeti hilo limeinukuu ripoti ya Shirika la Afya Duniani, WHO ikisema kuwa hali ni ya kutisha.

Kwa mujibu wa utabiri wa Shirika la WHO, hadi utakapofika mwaka wa 2030, idadi ya watu watakaogua maradhi ya kansa itaongezeka mara mbili katika nchi zinazoendelea. Gazeti la "Die Zeit" linasema kuongezeka kwa hali bora ya maisha pia kunachangia katika kuongezeka ,kwa idadi ya watu wanaopatwa na maradhi ya kansa. Gazeti hilo linatanabahisha kwamba barani Afrika,Asia na katika sehemu za Amerika ya kusini,watu wanaishikilia mitindo ya maisha ambayo madaktari katika nchi zilizoendelea wamekuwa wanatahadharisha juu yake.

Gazeti hilo linatoa mfano wa vyakula vyenye sukari nyingi vinavyosababisha uzito mkubwa na hivyo kuleta msangamano wa mafuta mwilini. Gazeti la "Die Zeit" limemnukuu daktari mmoja kutoka Uingereza anaefanya kazi barani Afrika ,akisema kuwa aghalabu wanawake wengi wanaenda kwake wakati tayari wakiwamo katika hatua za mwisho za maradhi ya saratani; ndiyo kusema hawaendi kuchunguzwa mara kwa mara.

Mlinzi wa uhai anuai ateketeza uhai

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeripoti juu ya mkasa unaomhusu afisa moja wa ngazi za juu kwenye wizara ya ulinzi wa mazingira katika jimbo la Thuringia mashariki mwa Ujerumani. Afisa huyo alifanya safari nchini Botswana ambako aliwinda na kumuua ndovu. Gazeti hilo limearifu kuwa licha ya kitengo chake pia kuhusika na ulinzi wa wanyama waliomo hatarini kutoweka,afisa huyo amepandishwa cheo.!

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu