Abbas ′rais′ wa Palestina huru | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 24.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Abbas 'rais' wa Palestina huru

Mkuu wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amechaguliwa na baraza kuu la chama cha Palestine Liberation Organisation PLO kuwa rais wa taifa lijalo la Palestina.

default

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas

Hata hivyo kundi la Hamas limelaani hatua hiyo likisema kuwa ina nia ya kurefusha muhula wake unaomalizika mapema mwakani.

Takriban wanachama 126 wa baraza kuu la chama cha PLO walikusanyika katika mji wa Ramallah ili kujadilia masuala ya ndani ya chama ya sasa.Mkutano ulikuwa wa siku mbili na ulimalizika jumapili.

Na kabla ya kikao hicho kumalizika, kilimchagua mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas,kuwa rais wa taifa huru la Palestina.

Taifa huru la Kipalestina baado halijapatikana, na hatua hii ya wajumbe baraza la PLO, inaonekana kama jaribio la kumpiga jeki Bw Abbas.

Uongozi wa wapalestina umegawanyika.Ukanda wa Gaza unasimamiwa na kundi la Hamas tangu Juni mwaka jana ilhali mamlaka ya Palestina pamoja na kundi la Fatah yanadhibiti maeneo ya ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Tangu wakati huo kumekuwa na juhudi za kujaribu kuyakutanisha na hivyo kuyapatanisha makundi hayo. Kundi la Hamas lilijiondoa katika mazungumzo na kundi la Fatah mapema mwezi huu,likishutumu majeshi ya usalama ya Fatah kwa kuwakamata wafuasi wa kundi hilo katika eneo la ukingo wa magharibi.

Kabla ya hatua ya wajumbe wa mkutano wa PLO kumchagua Abbas kama rais wa taifa huru la Palestina,kiongozi huyo, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, alikuwa ameonya kuwa angeitisha uchaguzi wa mapema iwapo makubaliano ya kuleta mapatano kati ya makundi ya waPalestina ya Fatah na Hamas hayatafikiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha amesema kuwa atatoa tamko la mapema mwaka ujao iwapo mazungumzo ya umoja wa kitaifa yatashindwa.

Lakini uchaguzi wake pamoja na onyo havijawatisha wa Palestina wa kundi la Hamas,likisema kuwa Abbas hana uwezo wa kulivunja bunge ambalo kundi la Hamas liko na wingi wa viti lililoupata katika uchaguzi wa mwisho wa 2006.Aidha linasema kuwa PLO halina umuhimu wowote sasa na pia kuwa haliwakilishi wapalestina wote.

Mbunge mmoja wa Hamas, Musheer al-Masri,ametoa taarifa akisema kuwa uamuzi huo wa PLO una nia ya kuendeleza muhula wa Abbas kama kiongozi wa Palestina ambao kulingana na sheria zao unamalizika Januari 9 mwaka wa 2009.

Ameongeza kuwa hatua kama hizo zitakwamisha hali ya mambo ndani ya chama pamoja na juhudi za kufanyika mazungumzo yenye nia ya kuleta maridhiano miongoni mwa wa palestina.

Yeye msemaji wa Hamas amesema kuwa rais wa Palestina huchaguliwa na wananchi wala si na kundi moja ambalo halina uhalali wowote kama hilo la baraza kuu la PLO.

Itakumbukwa kuwa Novemba mwaka wa 1988 baraza la kitaifa la Palestina PNC ambalo lilikuwa bunge la uhamishoni lilimchagua marehemu Yasser Arafat kama rais wa taifa la Palestina, na wakati huohuo alikuwa kama mwenyekiti wa PLO na kiongozi wa mamlaka ya Palestina.

Baada ya kifo cha Arafat Novemba 2004,Abbas alichaguliwa kama mwenyekiti wa kamati tendaji ya PLO na Januari 2005 alichaguliwa kama rais wa mamlaka ya Palestina.

.

 • Tarehe 24.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G0se
 • Tarehe 24.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/G0se
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com