1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma atafuta suluhu ya Libya, NATO yazidisha mashambulizi

30 Mei 2011

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anawasili mjini Tripoli kuzungumza na Muammar Gaddafi kuhusiana na mpango wa Umoja wa Afrika kumaliza mgogoro wa Libya huku NATO ikiendelea kuishambulia nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/11QZu
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Rais Zuma anafanya mazungumzo na Kanali Gaddafi katika wakati ambao wito wa kumtaka kiongozi huyo wa Libya aondoke madarakani ikiendelea kutolewa na jamii ya kimataifa.

Lakini ofisi ya Rais Zuma imesema kwamba lengo kuu la mazungumzo haya si kuandaa mkakati wa Gaddafi kuondoka, kama ilivyokuwa imevumishwa hapo mwanzoni.

Badala yake, ofisi hiyo imesema kwamba lengo la ziara hii ni usitishaji wa haraka wa mapigano, kuruhusu kusambazwa kwa misaada ya kibinaadamu na kujadiliana namna ya kufanya mageuzi ambayo yataondosha vyanzo vya mgogoro unaoendelea sasa.

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika ya Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, amesema kwamba Rais Zuma anakwenda Libya akiwa na viongozi wenzake kwa kutafuta suluhisho la amani la mgogoro wa Libya, maana vita haviwezi kamwe kuutatua mgogoro huu.

"Ziara hii ni ya kufuatilia pendekezo la mpango wa amani la Umoja wa Afrika, ambalo linasema kwamba tatizo tunalokabiliana nalo Libya ni la kisiasa. Kwa hivyo, hatuamini kuwa suluhisho la kijeshi linaweza kutatua matatizo ya kisiasa." Amesema Nkoana-Mashabane.

Msimamo huu wa Umoja wa Afrika, ambao anakwenda nao Rais Zuma nchini Libya, unatafautiana kivitendo na ule wa nchi za Magharibi na waasi, ingawa unafanana kimaneno.

Mara kadhaa, Katibu Mkuu wa NATO, Anders-Fogh Rasmussen, amenukuliwa akisema kwamba anaamini kuwa suluhisho la Libya linatakiwa liwe la kisiasa, ingawa kivitendo mashambulizi ya vikosi vyake dhidi ya Libya yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Hapo jana (29.05.2011) maafisa wa serikali ya Libya waliwaonesha waandishi wa habari skuli iliyoshambuliwa kwa kile wanachosema ni maroketi ya NATO kwenye makaazi ya Gaddafi ya Bab al-Aziziyah.

Kulikuwa na ushahidi mdogo wa madhara ya mashambulizi hayo, lakini mwalimu mkuu wa skuli hiyo, Hamid Miftar, amesema kwamba madirisha yalivunjwa na kusababisha wanafunzi waliokuwa wakijiandaa kwa mitihani yao "kukimbia kwa fadhaa".

Leo hii Rasmussen amenukuliwa akisema kwamba zama za utawala wa kiimla wa Gaddafi zinakaribia kwisha.

"Operesheni yetu nchini Libya inafanikisha malengo yake. Kwa kiasi kikubwa, tumempunguzia Gaddafi uwezo wa kuwauwa watu wake. Utawala wake wa kikatili unamalizika. Sasa anazidi kutengwa ndani na nje ya nchi yake. Hata wale waliokuwa karibu yake sasa wanakimbia, wanamuasi au wanamtenga." Amesema Rasmussen kwenye jukwaa la NATO mjini Varna, Bulgaria.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kulia) na Rais wa Marekani, Barack Obama
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kulia) na Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Katika hatua nyengine, Uingereza imetuma silaha zake nzito zenye uwezo wa kuripua mahandaki, na hivyo kuimarisha operesheni ya NATO nchini Libya. Silaha hizo, Enhanced Paveway III, zina uwezo wa kupenya kwenye hata majengo madhubuti.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Liam Fox, amesema kwamba hawakusudii kuwalenga watu mahsusi wa Gaddafi, lakini wanajaribu kutuma kile alichokiita "ujumbe mzito".

Katika hatua nyengine, wanasheria wawili nchini Ufaransa wanapanga kuanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya Rais Nikolas Sarkozy kwa uhalifu dhidi ya binaadamu nchini Libya, kutokana na ushiriki wake kwenye operesheni hiyo ya NATO.

Wizara ya Sheria ya Libya imewaambia waandishi wa habari hivi leo kwamba wanasheria hao, Jacques Verges na Roland Dumas, pia wamejitolea kuziwalikisha familia za wahanga wa mashambulizi ya NATO mahakamani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji