Umoja wa Afrika kuitaka NATO kuwacha mashambulizi dhidi ya Libya | Matukio ya Afrika | DW | 26.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Umoja wa Afrika kuitaka NATO kuwacha mashambulizi dhidi ya Libya

Viongozi wa Afrika leo wanajiandaa kusisitiza matakwa yao ya kuitaka Jumuiya ya Kujihami ya NATO kusitisha mashambulizi yake ya anga nchini Libya, huku wakiendelea kuzishutumu nchi za magharibi kupuuza jitihada zao.

default

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Mapema jana Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping alisema baadhi ya washiriki wa kimataifa katika migogoro ya sasa wanaonekana kama hawakubali kwamba Afrika inaweza kuwa na umuhimu katika utatuzi wa mgogoro kama wa Libya.

Aliongeza kwa kuonya kwamba Afrika haiwezi kutengwa katika uangalizi wa matatizo yanayoihusu.

Viongozi wa Afrika wamekutana katika mkutano maalumu mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili migogoro iliyopo kwa hivi sasa barani humo na hasa ikizingatiwa ya Libya na Sudan.

Bwana Ping, alisisitiza kwamba mkutano huo lazima upeleke ujumbe ulio wazi kwa wadau wengine duniani kwamba kuna haja ya kulitambua bara la Afrika katika jitihada zake za kustawisha amani katika mipaka yake.

Mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Afrika, unatarajiwa kufanya majumuisho yake baadae leo.

Siku chache zilizopita wapatanishi wa Afrika walitoa wito wa kusitishwa mapigano na kuandaa timu ya upatanishi, lakini hata hivyo jitihada zao zilikuwa na mchango mdogo sana ambapo majeshi ya nchi za magharibi yaliendelea na mashambulizi ya anga dhidi ya utawala wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

Awali katika hotuba yake kwa viongozi wa Afrika, Ping alikiri pia kwamba " ni suluhu ya kisiasa tu ambayo inaweza kufanikisha amani nchini Libya" na kusisitiza kwamba hali ilivyo nchini humo ni jambo linalowahusu sana, kwa mustakabali wa nchi hiyo pamoja na nchi za kanda hiyo.

Mpango wa kusitishwa mapigano ambao uliandaliwa na Umoja wa Afrika ulijumuisha kipindi cha mpito cha kuandaa uchaguzi, ulikubaliwa na Gaddafi mwenyewe lakini ulikataliwa na upande wa upinzani ambao ulisisitiza kiongozi huyo aondoke kwanza nchini humo.

Mapendekezo hayo ya Umoja huo yenye lengo la kumaliza mgogoro uliodumu kwa miezi kadhaa nchini Libya, yaliyojumisha timu ya upatanishi iliyoundwa na viongozi wa nchi za Afrika, yalibezwa kwa kiasi kikubwa na hata hivi karibuni, na Afrika Kusini.

Kabla ya mkutano wa viongozi wa Afrika kufunguliwa huko mjini Addis Ababa taarifa kutoka Afrika kusini zilisema Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo anatarajiwa kwenda mjini Tripoli wiki ijayo kuzungumza na Gaddafi.

Taarifa hiyo inatanabahisha kwamba mazungumzo hayo yatahusu majadiliano ya namna ya kuondoka kwake nchini humo.

Majeshi ya nchi za magharibi yaliingilia kati mgogoro wa Libya Machi 19, mwaka huu kwa kufanya operesheni ya mashambulizi ya angani, kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la kuwalinda raia wa nchi hiyo dhidi ya majeshi ya Gaddafi.

Lakini Ping aliendelea kusisitiza kwamba mapendekezo ya Umoja wa Afrika yana vigezo vyote vya kufikiwa kwa amani nchini Libya na kuongeza kuwa kinachohitajika ni upatikanaji wa fursa za utekelezaji wake.

Mwandishi: Sudi Mnette//AFP

Mhariri: Josephat Charo