Ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mashariki ya Kati | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 12.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mashariki ya Kati

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan amesema mpango wa Israel wa kujenga makaazi mapya unatishia juhudi za amani na unaweza ukasababisha vurugu zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden

Mfalme Abdullah wa Pili ameitoa kauli hiyo mbele ya Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, aliyeko Jordan, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya Mashariki ya Kati.

Taarifa ya kasri ya kifalme huko Jordan imemnukuu Mfalme Abdullah wa Pili akirudia kumwambia Bwana Biden kuwa analaani uamuzi huo wa Israel wa kujenga makaazi mapya katika eneo la Jerusalem Mashariki. Mfalme huyo wa Jordan amesema uamuzi huo unatishia mpango mzima wa amani na unaliweka eneo hilo katika hatari ya kuingia katika mzunguko mpya wa vita. Siku ya Jumanne Israel ilitangaza ujenzi wa makaazi mapya 1,600 ya Walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Waarabu katika Jerusalem Mashariki.

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan amesema ili amani iweze kupatikana katika eneo la Mashariki ya Kati, kunahitajika muongozo na msaada wa Marekani. Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, jana alimuomba radhi hadharani Bwana Biden

Joseph Biden und Benjamin Netanyahu Flash-Galerie

Benjamin Netanyahu pamoja na Joe Biden

katika harakati za kutatua mzozo juu ya ujenzi wa makaazi uliosababisha Palestina kususia mazungumzo ya amani ya ana kwa ana. Makamu huyo wa Rais wa Marekani alikubali msamaha huo, lakini aliukosoa uamuzi wa Israel wa kupitisha ujenzi mpya wa makaazi ya walowezi.

Katika hatua nyingine, Bwana Biden ametaka kuanzishwa haraka kwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina, licha ya Palestina kusisitiza kuwa Israel iachane kwanza na mpango wake huo, ambao umelaaniwa vikali na Marekani.

Akizungumza jana katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv, Bwana Biden alisema kitu muhimu ni mazungumzo hayo yasonge mbele katika hali nzuri. Aliongeza kuwa uamuzi huo wa Israel unakwamisha juhudi za amani. Naye katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu- Arab League- Amr Moussa, alisema Israel lazima iachane na mpango wake huo kwa ajili ya Wapalestina kushiriki katika mazungumzo ya amani.

Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas, alimwambia Amr Moussa kwamba hatoshiriki katika mazungumzo hayo ambayo yamekwama tangu Israel ilipovamia eneo la Ukanda wa Gaza linalodhibitiwa na kundi la Hamas Desemba mwaka 2008. Wakati huo huo, ndege za Israel leo zimerusha maroketi katika maeneo mawili katika eneo la kusini mwa Ukanda wa Gaza. Maeneo yaliyolengwa ni kiwanda cha kutengeneza hewa ya Oxygen na moja ya mahandaki ya chini ya ardhi yanayotumiwa kupitishia biashara za magendo katika mpaka wa Ukanda baina ya Ukanda wa Gaza na Misri. Roketi hizo zimerushwa kwa mara ya kwanza katika mpaka huo tangu mwanzoni mwa mwezi huu, hasa wakati huu ambao Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, akiwa anamalizia ziara yake ya Mashariki ya Kati. Leo Bwana Biden pamoja na mkewe watautembelea mji wa Petra uliopo kusini mwa Jordan kabla ya kurejea Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri: Miraji Othman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com