1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zarif na mawaziri wa Ulaya kuokoa makubaliano ya kinyuklia

Sekione Kitojo
15 Mei 2018

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif amesema juhudi za kuokoa makubaliano ya kinyuklia baada ya Marekani kujitoa, ziko katika njia sahihi alipoanza mazungumzo na mataifa yenye nguvu barani Ulaya mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/2xlRU
Belgien Brussel - Irans Außenminister Javad Zarif und Federica Mogherini
Picha: Reuters/T. Monasse

Zarif  alikutana  na  mkuu  wa  sera  za  mambo  ya  kigeni  wa Umoja  wa  Ulaya  Federica Mogherini  kabla  ya  mazungumzo  jioni ya  leo  na  mawaziri  wenzake  kutoka  Uingereza , Ufaransa na Ujerumani, nchi  tatu  zilizotia  saini  makubaliano  ya  kihistoria mwaka  2015 ambayo  wanajaribu  kuyaendeleza.

Kasachstan Syriengespräche in Astana
Javad zarif (kulia) akizungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov(kushoto)Picha: Reuters/M. Kholdorbekov

Iran  imeonya  kwamba  inajirayarisha  kuanza  tena  urutubishaji  wa kiwango  cha  viwanda  kwa madini  ya  urani , bila  vizuwizi , hadi pale  mataifa  ya  Ulaya  yatakapoweza  kutoa  uhakikisho  kamili kwamba  wanaweza  kuendeleza  maslahi ya  kiuchumi yaliyopatikana  kutoka  katika  makubaliano  hayo  ya  kinyuklia  licha ya  Marekani  kurejesha  vikwazo.

Zarif  ametoa  tathmini  ya  matumaini  baada  ya  mkutano  ambao ulikuwa  mzuri  na  wenye  mwelekeo  pamoja  na  Mogherini.

"Naamini tuko  katika njia  sahihi  kusonga  mbele  ili tuweze kuhakikisha  kwamba  maslahi  ya  washiriki  wote  waliobaki katika mpango  wa pamoja  wa  kuchukua  hatua  JCPA , hususan  Iran , yatalindwa  na  kuhakikishwa,"  aliwaambia  waandishi  habari.

Lakini  wanadiplomasia  wa  Ulaya  hawakutaka  kuonesha matarajio  makubwa  kutoka  katika  mkutano  huo  wa  leo, wakisisitiza  tu  kuhusu  changamoto  kubwa  ya  kutafuta  njia kukwepa  vikwazo  vya  Marekani  vya  biashara  ya  nje  na  Iran, ambayo  inafika  kila  mahali  duniani.

Europäischer Rat in Brüssel | Mohammed Dschawad Sarif, Außenminister Iran & Federica Mogherini
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif (kushoto) akiwa pamoja na mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa EU Federico MogheriniPicha: European Union

Bado kutakuwa  na  utata

"Hakuna  suluhisho moja  la  miujiza, kutakuwa  na  matukio yenye utata, na  magumu  katika  ngazi  ya  Umoja  wa  Ulaya  na  kitaifa, kwa  hiyo  itachukua  muda,"  afisa  mwandamizi  wa  Umoja  wa ulaya  alisema.

Umoja  wa  Ulaya  unasisitiza  kwamba  makubaliano  hayo yanafanyakazi, wakielekeza  katika  uchunguzi  wa  mara  kwa  mara wa  Umoja  wa  Mataifa unaofanya  tathmini  ya  utekelezaji  wa  taifa hilo  la  Kiislamu  kwa  upande  wake  wa  makubaliano, na  msemaji wa  Mogherini Maja Kacijancic akiliambia  shirika  la  habari  la  AFP kabla  ya  kuwasili  kwa  Zarif  kwamba " tunapawa  kufanya  kila linalowezekana  kuulinda  mkataba  huo".

Viongozi  wa  Umoja  wa  Ulaya  wanaonesha  msimamo  wa  pamoja katika  kulinda  makubaliano  hayo  na  Iran wakati  walipokutana kwa  chakula  cha  usiku  kabla  ya  mkutano mjini  Sofia  siku  ya Jumatano, afisa  huyo  alisema.

Mogherini  na  mkuu  wa  halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Jean-Claude Juncker  wanaainisha  kwa  viongozi  hatua  gani  kundi  hilo la  mataifa  linaweza  kuchukua  kukinga  maslahi  yake  ya  kiuchumi nchini  Iran.

Der Präsident der Europäischen Kommission Jean-Claude Juncker kommt im Regierungsgebäude in Skopje an
Jean-Claude Juncker rais wa halmashauri ya Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/R.Atanasovski

Makampuni  ya  Ulaya , hususan  yale  ya  Ufaransa  na  Ujerumani, yalikimbilia  kuwekeza  nchini  Iran kufuatia  makubaliano  hayo  ya mwaka  2015 , ambayo  Tehran  ilikubali  kusitisha  mpango  wake  ili kuondoa  vikwazo vikali  vya  kiuchumi  vya  kimataifa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman