1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WieczorekZeul na Benn watilia mkazo juu ya kuisaidia Afrika

Mohammed Abdul-Rahman18 Januari 2007

Walikubaliana kwamba juhudi za wakati huu za kulisaidia bara la Afrika hazina budi kurefushwa.

https://p.dw.com/p/CHll

Mawaziri hao wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani na Uingereza walikutana mjini Berlin Jumatano kwa lengo la kushajiisha sera zao za maendeleo, wakati wa Uwenyekiti wa Ujerumani wa Umoja wa Ulaya na kundi la mataifa 8 yalioendelea kiviwanda–G8 .

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Heidemarie Wieczorek-Zeul na mwenzake wa Uingereza anayehusika na maendeleo ya kimataifa Hilary Benn, walikumbusha juu ya juhudi za Ujerumani za kupigania ufutaji madeni na tija zake kwa mataifa mengi masikini duniani. Mawaziri wote wawili walikubaliana kwamba panapaswa kufanyika kila liwezekanalo, kudumisha moyo wa kundi la mataifa manne tajiri G8 kutokana na yalioafikiwa katika mkutano wao wa Gleneagles-Scotland na kuona kama ahadi za msaada wa fedha kwa Afrika zinatimizwa bila ya masharti yoyote.

Hilary Benn alilipongeza atangazo lililotolewa mjini Berlin kwamba sera za maendeleo zitabakia kuwa kipa umbele wakati wa kipindi chote cha Uwenyekiti wa Ujerumani wa umoja wa Ulaya na kundi la mataifa manene tajiri-G8

Alisema,“Ikiwa tunajali mustakbali wa sayari hii ndogo na tete, basi lazima tuguswe na hali za binaadamu wenzetu, watoto wasioweza kwenda shule mwanzoni mwa karne ya 21, watoto wanaokufa kutokana na magonjwa ambayo hayawauwi watoto wetu katika nchi tapiri. Nasi sote tuna wajibu wa kutoa mchango wetu.”

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani bibi Heidemarie Wieczorek –Zeul alionya juu ya mabadiliko ya hali ya hewa akisema yanaweza kuwa na athari kubwa mno kwa Afrika, na kufuta tija zote za awali na za wakati huu, za kulisaidia bara hilo. Akarejea tena wito wake kuzitaka nchi za viwanda ziwajibike.akaongeza kuwa ,“ Tutapaswa kutumia kwa gharama ya mara 20 zaidi katika kukabiliana na badiliko la hali ya hewa mnamo siku za usoni, kama hatutachukua hatua hivi sasa. Ndiyo maana kukuza matumizi ya nishati mbadala na kujitosheleza kwa nishati, ndiyo masuala makuu ya sera zetu wakati wa kipindi hiki cha Uwenyekiti wa Umoja wa ulaya na G8.

Suala jengine lililozingatiwa na usawa katika biashara ya kimataifa. Upande huo waziri Benn alisema ,“Hatuna budi kuwa tayari kutovunjika moyo, katika kupata makubaliano ya biashara yatakayoziruhusu nchi zinazoendelea kujiondoa kwenye umasikini. Kwa sababu hatimae hazitaki kupewa sadaka badala yake zinataka kuwa na nafasi ya kuendesha mambo zenyewe.”

Waziri huyo wa maendeleo ya kimataifa wa Uingereza alisema kuna kambi tatu-ulaya, Marekani na nchi zinazoendelea China, India na Brazil, na kila moja inamwambia mwenzake” Nafikiri tumetoa fursa nzuri ni juu yako kuchukua hatua.” Waziri Benn alisema nafasi hii muhimu haipaswi kupotezwa kwani mwishowe faida zake ni pamoja na Afrika na sehemu nyengine za ulimwengu wa tatu kuweza kujipatia fedha za kujiendeleza wenyewe kwa kuhakikisha watoto wana kwenda shule na kununulia madawa ili watu wao wasifariki kutokana na Ukimwi, kifua kikuu au malaria.

Hilary Benn na Heidemarie Wieczorek-Zeul walidokeza kwamba mkutano wa kilele wa mataifa ya G8 katika mji wa Ujerumani wa Heiligendamm mwezi Juni mwaka huu, utakua na kitu mahsusi kwa nchi zinazoendelea. Hata hivyo walikataa kufafanua hadharani, kwani maandalizi ya mkutano huo ndiyo kwanza yameanza.